WACHEZAJI WAPYA WA SIMBA KAZE GILBERT NA KHAMIS TAMBWE WAZUIWA NCHINI BURUNDI..!!
NYOTA wapya wawili wa Klabu ya Simba, straika Khamis Tambwe na beki Kaze
Gilbert, watachelewa kujiunga na timu hiyo baada ya klabu yao ya
Vital’O ya Burundi kuwazuia kwa muda.
....SOMA ZAIDI.....
Nyota hao tangu waliposaini
mikataba Msimbazi na kurejea kwao hawajarudi na juzi hawakuonekana
katika Tamasha la Simba Day kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, licha
ya Simba kuwa na utaratibu wa kulitumia kwa ajili ya kuwatambulisha
wachezaji wake wote kabla ya msimu kuanza.
Awali, wachezaji hao
walitarajiwa kutua nchini mwishoni mwa wiki iliyopita, lakini haikuwa
hivyo, hali iliyowalazimu Simba kuanza kuwafuatilia kwa haraka.
Joseph
Itang’are, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Simba, ameliambia Championi
Jumatatu kuwa, nyota hao wameshindwa kuwasili kwa wakati, baada ya klabu
yao kuwazuia kwa muda, ikitaka wamalizie michezo iliyobaki ya Ligi Kuu
ya Burundi kabla haijaachana nao rasmi.
Itang’are, maarufu kama Mzee Kinesi, alisema vital’O ilikuwa imebakiza michezo miwili, mmoja ukichezwa juzi.
Mzee
Kinesi alisema Vital’O imepanga kuwapa baraka za kuja Tanzania katikati
ya wiki hii, tayari kwa kuanza maisha mapya na Wekundu hao.
“Tulilazimika
kuwasiliana nao haraka baada ya kuona kimya, lakini hata klabu yao nayo
imeonyesha uungwana wa kutupigia na kutueleza kuwa wachezaji hao ni
muhimu sana kwao wakati huu ligi yao ikielekea ukingoni,” alisema Mzee
Kinesi.
“Kwa shingo upande ilibidi tuwakubalie kwa kuwa sisi bado
hatujaanza ligi ya huku kwetu, ingawa tunajua kuchelewa kwao kunaweza
kumchelewesha kocha wetu kutengeneza kikosi chake, tunaamini mpaka
kufikia katikati ya wiki ijayo (wiki hii), watakuwa wameshafika nchini.”
Nyota
hao wanatarajiwa kuongeza nguvu katika kikosi cha Simba. Tambwe alikuwa
mfungaji bora kwenye michuano ya Kombe la Kagame iliyomalizika hivi
karibuni nchini Sudan, wakati Kaze alikuwa mhimili mkubwa katika kikosi
chao cha Vital’O kilichotwaa ubingwa wa michuano hiyo.
No comments:
Post a Comment