WASOMI watakaohitimu vyuo vya elimu ya juu nchini kuanzia mwaka huu watakopeshwa mabilioni ya fedha ili waanzishe miradi itakayowawezesha kujiajiri. Hatua hiyo ni matokeo ya Programu ya Wizara ya Kazi na Ajira inayolenga kukuza ajira kwa vijana wahitimu wa vyuo hivyo, kwa kushirikiana na vya elimu ya juu, taasisi za fedha na wabia wa maendeleo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa Wizara hiyo, Ridhiwani Wema alisema, Sh bilioni 54 zitahitajika kufanikisha miradi 1,000 itakayotekelezwa kwa awamu tatu kwa miaka mitatu ya utekelezaji. Kwa mujibu wa Wema, kati ya fedha hizo, Sh bilioni 4.4 ni za mafunzo na kuandaa vijana ili wakopesheke na Sh bilioni 50 zitakuwa dhamana.
"Lengo la kuanzisha programu hii ni kuongeza fursa za ajira 30,000 za moja kwa moja kwa wasomi hao kwa kipindi hicho. Tunaamini miradi watakayoanzisha itafanya wajiajiri na kuajiri wengine.
"Katika kuhakikisha programu hii inafanikiwa, Serikali imekubaliana na Benki ya CRDB kutoa mikopo kwa vijana, mara utekelezaji utakapoanza rasmi. Utaanza kwa kuendeleza programu ya mfano iliyoanzishwa na Idara ya Kilimo, Uchumi na Biashara katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)," Wema alisema.
Alisema, baada ya hapo, wahitimu wa vyuo vingine vya elimu ya juu nao watafikiwa na kuandaliwa vizuri kwa mafunzo ili wawe wajasiriamali kupitia miradi watakayoianzisha kwa kutumia mikopo watakayopewa. Wema alifafanua kuwa wahusika watalazimika kuandika mapendekezo ya miradi yao ambayo yataangaliwa na kupangiwa kiasi cha fedha, ili waweze kukopeshwa tayari kwa kuanza kuitekeleza.
"Miradi itakayoanzishwa itatoa mnyororo mzima wa thamani, kwa mfano mradi wa alizeti na ukamuaji mafuta. Tumejiridhisha kuwa miradi hiyo itapunguza wimbi la vijana kukimbilia mijini, kwa sababu itakuwa ikitekelezwa katika maeneo watakakokuwa wahitimu hao ambayo si ya mjini pekee," alisema.
Wema alifafanua kuwa katika awamu ya kwanza vijana 600 kutoka SUA watahusika kumiliki miradi 200 ya kujiajiri na kuajiri wahitimu wengine 5,400, wakati katika awamu ya pili, vijana 900 kutoka vyuo vingine wataanzisha miradi 300. Kwa maelezo yake, awamu ya tatu itahusisha wahitimu 1,500 wa vyuo vingine ikiwamo VETA itakayokuwa na miradi 500 itakayozalisha ajira 13,500.
"Hivyo ndivyo tutakavyotumia programu hii kupunguza tatizo la ajira na kuhakikisha wanaoandika mapendekezo yenye ushawishi na yanayoelezea miradi inayotekelezeka watakopeshwa," alisema na kuongeza kuwa muda utakapofika, wahitimu wataandikishwa na kutambuliwa kupitia mikoa na wilaya wanamoishi.
Watapeliwa ajira Wakati mikakati ya ajira ikiwekwa ili kukomboa vijana wasomi nchini, Jeshi la Polisi Dodoma linamshikilia Mariam Tawakali (28) akidaiwa kutapeli wahitimu wa vyuo vikuu kwa ahadi ya kuwapa kazi ya kuandikisha wananchi wanaotarajiwa kupewa vitambulisho vya uraia chini ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Hayo yalithibitishwa jana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime akisema Mariam alikamatwa juzi katika Barabara ya Sita, Dodoma, baada ya Polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema.
Alisema mtuhumiwa alikutwa na vitambulisho vitano vyenye majina tofauti ya Mariam Tawakali na Monica Emmanuel Ngaso (28), mkazi wa Nkuhungu, Dodoma.
Miongoni mwa vitambulisho hivyo ni cha Mkutano Mkuu wa CCM, wa Novemba 11-13, mwaka jana ambapo kazi yake ilionesha kuwa ni mhudumu.
Kingine ni cha kampuni ya Thaker Singh Coast Action chenye jina la Monica Emmanuel Ngaso, kazi Katibu Muhtasi, nacho kitambulisho cha New Dodoma Hotel chenye jina la Mariam Tawakal kazi yake Katibu Muhtasi na cha Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima chenye jina la Mariam Tawakali, kikionesha ni mwalimu wa taasisi hiyo kijijini Chamwino.
Kamanda Misime alisema Mariam alitangazia wananchi, kwamba kazi ya kuandikisha vitambulisho vya uraia kwa Dodoma itaanza mwezi ujao.
Pia waliwaeleza kuwa atakayehitaji kazi hiyo awasilishe maombi kwake akiambatanisha vyeti vya elimu ya sekondari au chuo, picha za vitambulisho na fedha taslimu Sh 110,000 za kiingilio. Aidha, aliwaambia atakayepata nafasi atalipwa mshahara wa Sh 400,000 kwa mwezi kwa miezi mitatu ambapo kazi hiyo itakuwa imekamilika.
Alisema mtuhumiwa huyo alifanikiwa kukusanya vyeti, picha na fedha kwa wananchi 29 wengi wao wakiwa wahitimu wa vyuo vikuu mwaka huu.
Kamanda Misime alisema Polisi inatoa hadhari kwa wananchi kuwa makini na wanaofanya vitendo hivyo na kuwataka kutoa taarifa mapema wanapotilia shaka watu wa aina hiyo ili hatua za kuwadhibiti zichukuliwe mapema.
Alitaka wananchi kuelewa kuwapo matapeli wanaobuni miradi ya kujipatia fedha kwa udanganyifu na kuwataka kuchukua hadhari mapema kwa kukataa kurubuniwa ajira na kutoa fedha bila kuthibitisha.
Alisema Polisi inafuatilia kuona uhalali wa vyeti vya wanafunzi hao wa vyuo vikuu na kuona ni kosa gani Mariam atashitakiwa nalo. Pia alitaka waliotapeliwa kufika Polisi kutoa ushahidi kabla ya kesi haijafikishwa mahakamani.