Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa kazini. (Picha kutoka Maktaba)
Askari mmoja wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mkoani
Kilimanjaro, Fidelis Mwaliyatabu, amefariki dunia papo hapo na wengine
tisa akiwamo Mkuu wa Kikosi hicho kujeruhiwa vibaya baada ya gari lao
kupinduka katika kijiji cha Kilingi, wilaya ya Siha, wakati wakienda
kuzima vurugu za wananchi.
Ajali hiyo ilitokea wakati kikosi hicho kikielekea katika kijiji cha
Karansi kwa ajili ya kukabiliana na wananchi waliokuwa wakiandamana
kupinga wenzao waliokamatwa usiku wa manane baada ya kuvamia mashamba
mali ya Shirika la Roho Mtakatifu-Kilasara.
Taarifa kutoka kijijini humo zilieleza kwamba wanakijiji waliamua
kuandamana baada ya wenzao watano kukamatwa na Jeshi la Polisi nyakati
za usiku kwa mahojiano kutokana na kukabiliwa na tuhuma za kushawishi
wanakijiji wenzao kuvamia maeneo ya Shule ya Kilasara na kusababisha
hasara kubwa kwa shule hiyo.
Kufuatia kukamatwa kwa watuhumiwa hao, wanakijiji waliamua
kuandamana hadi katika kituo cha polisi ili kuwatoa wenzao hali
ilisababisha jeshi hilo kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya, jambo
ambalo lilishindikana kutokana na wingi wa watu walikuwa wanaandamana.
Inadaiwa kuwa wananchi hao walijikusanya na walianza kuandamana
kuanzia majira ya saa 7 usiku kuelekea kituo cha polisi ili kuwatoa
wenzao walikuwa wanashikiliwa.
Wananchi wanaoshikiliwa na jeshi hilo ni John Sokoine, Abeli
Solomoni, Christopher Solomon na aliyetambuliwa kwa jina moja tu la
Julius. Wote walikamatwa usiku wa kuamkia jana.
Mnamo Juni 11, mwaka huu majira ya mchana wananchi wa kijiji hicho
walivamia eneo lenye ukubwa wa hekta mbili na kufyeka mazao mbalimbali
yaliyokuwa shambani hapo kwa madai kuwa wamiliki wa shule hiyo
wamechukua eneo hilo kinyume cha taratibu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shirika la Roho Mtakatifu, Kanda ya Afrika,
Padri Jerome Okama, aliushutumu uongozi wa kijiji hicho kwa kuvifumbia
macho vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi wakati wakitambua
kuwa eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 8.9 linamilikiwa na shirika hilo
kihalali.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Robert Boaz, akizungumza na mwanahabari wetu
kwa njia ya simu kutoka wilayani humo jana jioni, alisema askari hao
walipata ajali hiyo majira ya saa 6.45 mchana katika kijiji cha Kilingi
nje kidogo ya mji wa Sanya Juu.
Alisema askari hao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC na
wengine wamelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu ya
Kibong'oto ilioyopo wilayani Siha na kwamba watano kati yao hali zao ni
mbaya.
Alitaja gari la Polisi lililopinduka na kuua kuwa ni Toyota Land
Cruiser lenye namba PT 2070 lililokuwa likiendeshwa na Sajenti Herman
Dancan. Chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na kuacha njia na
kupinduka.
Aliwataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni Mkuu wa FFU mkoani
hapa, ASP Nonino, Renatus Misigalo, Alfonce Joseph, Koplo Elifuraha
Lenare, Peter Albert, Bashiri Yusuph, George Mwakyusa na Gaspar
Mwapunda.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Kibong'oto.