|
Waziri Mkuu Mizengo Pinda. |
Serikali imeunda Kamati maalumu ya
kitaifa kuchunguza na kubaini majina ya Watanzania wanaodaiwa kuficha
fedha nje ya nchi kinyume na sheria na kanuni za nchi.
Pamoja na kuchunguza, Kamati hiyo yenye wajumbe wanane iliyoundwa Januari 9, itachunguza iwapo fedha hizo ni haramu au la.
Hayo yalisemwa bungeni jana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alipokuwa anatoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa 10 wa Bunge mjini hapa.
Hatua
ya kuundwa Kamati hiyo ilitokana na Azimio namba 9/2012 likiitaka
Serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania hao. Azimio hilo lilizaliwa
na hoja binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto.
Kwa
mujibu wa Azimio hilo, Serikali inatakiwa kuwasiliana na Benki ya Dunia
kupitia kitengo cha urejeshaji mali, ili mabilioni yanayomilikiwa na
Watanzania katika benki za nje ambako hufichwa kwa kukwepa kodi,
yarudishwe nchini.
Lakini pia Watanzania wote wenye akaunti za fedha
nje ya nchi waeleze wamezipataje ili Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) ichukue hatua za kisheria dhidi ya wamiliki wa fedha
na mali kinyume na mapato yao halali.
Serikali ilikubali, kwamba
katika Mkutano wa Bunge wa 11 itawasilisha taarifa ya hatua
iliyochukuliwa ili kuziba mianya ya utoroshaji wa fedha nje ya nchi.
Mbali
na kuchunguza uhalali wa fedha hizo, Kamati hiyo ambayo wajumbe wake
hawajatajwa kwa majina, pia itatakiwa kutambua benki na nchi
zilikofichwa fedha hizo na pia kuandaa mashitaka dhidi ya Watanzania
watakaobainika kuficha fedha haramu nje ya nchi; na kuishauri Serikali
jinsi ya kuzuia uhalifu wa makosa ya fedha.
“Ili kuiwezesha Kamati
hii kufanya kazi yake kwa ufanisi, ni wazi kwamba itahitaji ushirikiano
mkubwa kutoka kwa wananchi kwa kutoa taarifa kuhusu suala hili. Hivyo,
wananchi wote wenye taarifa sahihi na za ukweli zinazoweza kuisaidia
Kamati kutekeleza kazi hii, wajitokeze kutoa maoni yao kupitia Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kushirikiana kwa karibu na Kamati
…waheshimiwa wabunge nao nawaomba kutoa ushirikiano wa kufanikisha kazi
za Kamati hii,” alisema Waziri Mkuu.
Kuhusu hali ya amani nchini,
Waziri Mkuu alielezea kuwapo hivi karibuni dalili za kupoteza sifa ya
umoja wa kitaifa na amani ambavyo vimedumu kwa miaka mingi, kwa wananchi
kushuhudiwa wakishindwa kuvumiliana, japo kwa tatizo dogo tu miongoni
mwao.
Vyama vya siasa vimeonesha dalili ya kuhamasisha wanachama
kuingia kwenye malumbano ya siasa baina yao wenyewe kwa wenyewe au
baina ya chama na kingine na baadhi ya wanachama kushikana mashati na
kujeruhiana.
“Napenda kutumia fursa hii, kuasa viongozi wa vyama vya
siasa kuepuka kutumia majukwaa ya siasa kuvuruga amani na utulivu
uliopo. Waepuke matamko ya vitisho na kuhamasisha wanachama kuendeleza
vitendo vya uvunjifu wa amani na kujenga chuki na uhasama miongoni mwa
jamii na kwa Serikali halali iliyoko madarakani,” alisema Pinda.
Aliongeza
kuwa pamoja na kutofautiana kwa mawazo na sera za vyama vya siasa, ni
muhimu kujenga mazingira ya kuvumiliana kwa hali ya juu katika kujenga
demokrasia ya kweli nchini.
“Viongozi wa vyama wanatakiwa kueleza
sera zao badala ya kutukanana, kubezana, kushutumiana na kuzomeana.
Tujenge nchi yetu kwa amani na utulivu ndipo tutapata maendeleo
endelevu,” aliasa.
Alisema kumeibuka pia chokochoko za kidini; baadhi
ya waumini wa dini wamekuwa wakikashifu dini nyingine kwa kejeli na
vitendo vingine visivyostahili, ambapo pia baadhi ya viongozi wa
madhehebu ya dini wamekuwa wakiwaingiza waumini wao katika migogoro
isiyokwisha, ikiwa ni pamoja na kufungiana milango na kuzuia waumini
kuabudu siku za ibada.
“Napenda kusisitiza, kuwa madhehebu ya dini
yana nafasi kubwa ya kujenga umoja wa kitaifa, amani na mshikamano.
Nawaomba viongozi wa madhehebu ya dini kutatua kwa amani migogoro
iliyopo na kuelimisha waumini wao kuthamini, kujenga na kuenzi amani na
utulivu uliopo.
“Serikali imetoa uhuru wa wananchi kuabudu, kila mtu
kwa dini anayoitaka. Hivyo, hakuna sababu ya dini moja kukashifu
nyingine. Aidha, tupinge kwa nguvu zetu zote chokochoko za kidini ambazo
zimeanza kujitokeza sehemu mbalimbali nchini,” alisema.
Aliyagusa
pia mashirika yasiyo ya serikali (NGOs) akisema baadhi yao yamekuwa
yakihusishwa kuwa mstari wa mbele kurubuni wananchi kufanya vurugu
zinazolenga uvunjifu wa amani wakati yana jukumu kubwa la kuelimisha
wananchi kuhusu umuhimu wa kujenga umoja wa kitaifa.
“Viongozi wa mashirika haya waepuke kutumiwa na baadhi ya viongozi, kupanda mbegu mbaya kwa wananchi kuvuruga amani,” alisema.
Kwa
upande wa vyombo vya habari, alisema kumekuwa na kutiliana shaka kwa
baadhi ya vyombo hivyo kuandika habari za uchochezi, hivyo kuashiria
uvunjifu wa amani na mshikamano wa kitaifa.
“Vyombo vya habari vina
wajibu mkubwa wa kuelimisha umma na kuhabarisha kuhusu masuala ya
maendeleo, kama wafanyavyo jirani, hususan vyombo vya habari vya Rwanda.
Aidha, vyombo hivi vina fursa nzuri ya kutumia uhuru uliopo kudumisha
amani na utulivu nchini,” alisema.
Kuhusu nini kifanyike, Waziri Mkuu
aliitaka Serikali, wananchi na wadau wote vikiwamo vyama vya siasa,
madhehebu ya dini, vyombo vya habari, mashirika yasiyo ya serikali, n.k.
wakae wazungumze na kutafakari kuhusu hali hiyo.
“Tunapaswa kwa
namna zote tuvumiliane na kuheshimiana kwa kuzingatia utamaduni wa
kitanzania na misingi ya amani na utulivu tuliojijengea kwa muda mrefu;
na wananchi wote tuzingatie na kuheshimu utawala bora wa sheria, kanuni
na taratibu zilizopo,” alishauri Waziri Mkuu.
Akizungumzia hali ya
chakula nchini, Waziri Mkuu alisema tathmini iliyofanyika hivi karibuni
juu ya chakula na athari za mvua zinazoendelea kunyesha, inaonesha kuwa
maeneo mengi hasa yanayopata mvua za msimu, ya Mbeya, Ruvuma, Rukwa,
Iringa, Tabora na Mtwara, mazao mengi yako katika hatua mbalimbali za
ukuaji na kama mvua zitaendelea vema, upatikanaji wa chakula katika
maeneo hayo utakuwa mzuri.
Hata hivyo, alisema kuna upungufu wa
chakula katika wilaya 47 katika mikoa 15 ambazo zitahitaji msaada wa
chakula katika vipindi tofauti ambapo inakadiriwa kuwa jumla ya watu
1,615,445 watahitaji jumla ya tani 32,870 za chakula.
“Kutokana na
matarajio hayo ya uhaba wa chakula, Serikali itahakikisha Kitengo cha
Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kinaendelea kusambaza mahindi katika
maeneo yenye uhaba. Hadi sasa jumla ya tani 20,000 zilishatolewa kwa
mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma, Singida, Morogoro, Lindi,
Tanga, Mtwara, Pwani, Dar es Salaam, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara na
Tabora,” alisema. Bunge liliahirishwa hadi Aprili 9, Dodoma.