|
Bratislav akitoka ndani ya makazi yake yaliyoko kwenye kaburi. |
Mtu asiye na makazi ameeleza jinsi alivyoanza kulala na wafu wakati alipohamia kwenye kaburi miaka 15 iliyopita.
Bratislav
Stojanovic, 43, anachangia eneo hilo la kuzikia wafu na mavumbi ya
familia moja ambayo ilifariki zaidi ya miaka 100 mjini Nis, Serbia.
Lakini baada ya kulibadilisha kaburi hilo na kulipamba, mfanyakazi huyo wa zamani wa ujenzi alisema anajisikia yuko nyumbani.
Alisema: "Ni pakavu na kuna joto. Nina taa kadhaa na mali zangu mwenyewe.
"Sio hekalu lakini ni raha zaidi kuliko mtaani."
Stojanovic, ambaye hakuwahi kuwa na kazi ya kawaida, alipoteza makazi yake mjini humo baada ya kuzidiwa na madeni.
Alihamia
kwenye kaburi hilo baada ya kutangatanga kwenye mitaa kwa miezi na sasa
anatumia muda wake kujimulikia kwa mishumaa kwenye makaburi hayo.
Bratislav
alisema kwamba kuishi na wafu sio jambo la kutisha kama ambavyo wengi
wanaweza kufikiri. Alisema: "Nilikuwa nikiogopa mwanzoni, lakini
nimezoea kwa sasa. Sasa ninahofia zaidi maisha kuliko hawa wafu.
"Wakati
wowote ninapotaka kutoka nje kwanza nahakikisha hakuna mtu yeyote eneo
hilo, vinginevyo ninaweza kumtisha mtu hadi akafa.
"Watu ni wakarimu mno kwangu, wakati mwingine huniletea chakula au nguo.
Wakati
mwingine ninalazimika kupata chakula changu kwenye mapipa ya taka
lakini kinaweza kuwa na lishe bora. Inashangaza vitu ambavyo watu
wanavitupa," alielezea.
"Hainiogopeshi mimi kulala kwenye kaburi. Wafu wamekufa. Ninaogopeshwa zaidi kuwa na njaa.
"Na kama nakufa usiku, angalau niko kwenye sehemu sahihi."
Stojanovic
anaishi kwa vyakula vye lishe bora anavyokusanya kutoka kwenye takataka
na kukusanya vipisi vya sigara anavyookota chini.
Pango lake lina ukubwa wa yadi mbili za mraba na paa lake liko umbali wa yadi moja kwenda juu.
Maofisa
wa eneo hilo la makaburi wamesema mpangaji wao huyo anaweza kuishi hapo
kwa kipindi chochote atakavyo kama tu habughudhi wageni wengine.
"Familia
iliyokuwa ikimiliki kaburi hilo ilishatoweka kitambo hivyo kwa sasa
halina mwenyewe. Kama atakuwa mstaarabu hakuna mipango ya kumwondoa,"
alieleza msemaji.
Jina la familia iliyokuwa ikimiliki kaburi hilo haijafahamika kufuatia majina hayo kufutika kwenye jiwe lililowekwa hapo.