Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Saidi Meck Sadiki akiongea na waandishi wa
habari Ofisini kwake kuhusu Usafi wa Jijinla Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam Mhe.Saidi Meck Sadiki Ofisini kwake leo katika mkutano wake na
waandishi wa habari. Amesema katika taarifa yake aliyoisoma kwa Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Mohamed Gharib Bilal katika ziara yake
ya siku moja katika Mkoa wa Dar es Salaam tarehe 21/07/2013 katika ukumbi wa
Karimjee alisisitiza kuwa zoezi la usafi wa Jiji la Dar es Salaam ni endelevu
mpaka tutakapofika wakati wa kuridhisha kuwa JIJI LETU SASA NI SAFI.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
amesisitiza kuwa jukumu hili la usafi katika Jiji letu hili litafanikiwa ikiwa
mambo makubwa matatu yatazingatiwa:
1.Ushiriki wa Wakazi wa Dar es Salaam
(Wana Dar es Salaam) kikamilifu katika kufanikisha zoezi hili.Hii inaonekana
kuwa kama wakazi wa Dar es Salaam tutakuwa na utamaduni wa kupenda usafi na
kuchukia uchafu basi tutafanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani sisi tutakuwa askari
wa sisi kwa sisi. Hata hivyo ikitokea umemuona mwenzako amepanga biashara
sehemu isiyotakiwa au ametupa takataka ovyo tutakuwa wa kwanza kukemeana sisi
kwa sisi na kuacha kufanya hivyo sambamba na kuacha kununua bidhaa hizo katika
maeneo yasiyofaa.
2.Viongozi/Wanasiasa kukemea suala hili
la uchafu katika Jiji la Dar es Salaam: Hii imeonekana kuwa Jitihada, Juhudi na
Nguvu nyingi zimekua zikifanywa na Serikali yetu ili kuhakikisha Jiji letu
linakua safi,lakini kwa bahati mbaya imeripotiwa/imeonekana kuwa kuna viongozi/Wanasiasa
wengine wametumika katika kuwapa viburi baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es
Salaam kufanya biashara katika maeneo yasiyotakiwa hivyo kusababisha hasara ya
kutupa takataka ovyo na kukwepa kulipa ushuru wa bidhaa wanazoziuza ili hali
wamepangiwa maeneo yao husika kwa ajili ya kufanya shughuli zao.
3.Wanahabari/Waandishi wa Habari:
Jukumu la waandishi wa habari ni kubwa sana katika kufanikisha kampeni hii
kwani wao ndio wamekuwa wakitupatia habari mbalimbali za kuhusu uchafu wa Jiji
la Dar es Salaam hivyo ninawaomba kuendelea kushirikiana katika kuibua sehemu
ambazo zimekaidi katika kufanikisha zoezi hili na kuziripoti/kukemea na
kuelimisha moja kwa moja kwa kutumia vyombo mbalimbali vya
habari ili Jamii kwa ujumla ipate kujua hali ilivyo na kuacha tabia hiyo.
WITO
Mhe.Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
ametoa wito kuwa Wana Dar es Salaam tujenge utamaduni wa kuchukia uchafu na
kulitunza na kulilinda Jiji letu la Dar es Salaam,aidha wamachinga wafanye
biashara zao katika maeneo yao waliyotengewa ili kuepusha uchafuzi wa mazingira
pamoja na usumbufu wa hapa na pale na sheria na taratibu zitachukuliwa kwa
yeyote atakaesababisha uchafu katika Jiji letu la Dar es Salaam.
TUKIAMUA TUNAWEZA KWA PAMOJA
TUSHIRIKIANE KATIKA KUWEKA MAZINGIRA YA JIJI LA DAR ES SALAAM KUWA SAFI.
Imetayarishwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.