PATRICK Ochan na Emmanuel Okwi wamefanya uamuzi wa kushangaza
baada ya wote wawili kuomba kurudi kuichezea Simba ya jijini Dar es
Salaam.
Ochan, kiungo aliyeuzwa na Simba kwenda TP Mazembe
ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kiasi cha dola 100,000
anataka kurudi Msimbazi haraka iwezekanavyo kwa uhamisho wa mkopo baada ya kuchoshwa na maisha ya Lubumbashi.
anataka kurudi Msimbazi haraka iwezekanavyo kwa uhamisho wa mkopo baada ya kuchoshwa na maisha ya Lubumbashi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na
Mwanaspoti, Ochan mwenye umri wa miaka 27, ameonyeshwa kukerwa na lundo
la wachezaji mahiri na wasio mahiri ndani ya TP Mazembe ambalo
limesababisha akose namba ya kudumu klabu hapo.
“Nataka kurudi Simba kwa mkopo, nimechoshwa na
maisha ya Mazembe. Tajiri (Moise Katumbi) anarundika wachezaji wengi
hapa na nafasi ya kucheza imekuwa ngumu. Waambie watu wa Simba nataka
kurudi klabuni kwangu kwa mkopo. Mwambie Kaburu (Geofrey-aliyekuwa
Makamu Mwenyekiti wa Simba) nataka kurudi Simba,” alisema Ochan.
Ochan amekiri kwamba mara kadhaa amejaribu kuihama
Mazembe ikiwemo kutaka kutimkia Afrika Kusini kuichezea timu ya Golden
Arrows, lakini Katumbi ametia ngumu.
“Kuhama kwa mkopo inawezekana. Nitazungumza na
viongozi huku nadhani inawezekana kabisa kwa sababu watataka nipate muda
wa kucheza. Baada ya wiki mbili nitakuja Uganda. Kwa kweli nataka
kurudi zangu Simba,” alisema Ochan ambaye aliuzwa pamoja na Mbwana
Samata wakitokea Simba.
Katika hatua nyingine, Emmanuel Okwi naye amempigia simu mmoja ya viongozi wa Simba na kuomba arudi Msimbazi.
Okwi, ambaye yupo jijini Kampala akiwa amesusa
kwenda Etoile du Sahel kwa mwezi moja sasa, ameomba kurudi Simba kwa
madai kuwa amekuwa hapewi nafasi ya kucheza, lakini mbaya zaidi amekuwa
halipwi mshahara na hajamaliziwa fedha zake za kusaini mkataba wa miaka
mitatu.
“Ni kweli amepiga simu kuomba tumrudishe Simba,
lakini tukifanya hivyo tutakosa Sh 480 milioni ambazo tunawadai
Etoile,”alisema kiongozi mmoja wa Simba. Kiongozi huyo alisema
kinachoweza kufanyika ni klabu hiyo ya Tunisia angalau iwalipe Sh 300
milioni halafu Okwi aje Simba kucheza kwa mkopo.
Mwanaspoti ilimtafuta Okwi kwa simu jana Ijumaa, lakini simu yake ya mkononi ilikuwa inaita bila kupokewa.
source mwanaspoti
source mwanaspoti