Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Dk Gervas Mbasa

KWA UFUPI
“Alinieleza kwamba kwa niaba ya Airtel yupo katika zoezi la kuhakiki namba zote zilizosajiliwa zamani na yangu ilikuwa ni ya miaka 10 na akaniuliza namba ya mwisho kuwasiliana na mtu kupitia simu yangu.

SAKATA la wizi wa fedha katika akaunti za wateja wa benki, sasa limeingia katika sura mpya baada ya Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Dk Gervas Mbasa (Chadema) naye kuibuka na kudai kuwa ameibiwa Sh6 milioni kutoka kwenye akaunti yake.


Akizungumzia wizi huo, mbunge huyo alisema fedha zake ziliibwa kwa nyakati tofauti kati ya Desemba 20 mwaka jana na Januari 3, mwaka huu.
Alisema kitendo hicho kilifanywa na mtu mmoja aliyempigia simu na mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa ni mfanyakazi wa Makao Makuu ya Kampuni ya Airtel na kwamba alikuwa katika zoezi la kuhakiki namba zote za zamani.


“Alinieleza kwamba kwa niaba ya Airtel yupo katika zoezi la kuhakiki namba zote zilizosajiliwa zamani na yangu ilikuwa ni ya miaka 10 na akaniuliza namba ya mwisho kuwasiliana na mtu kupitia simu yangu. Nilimtajia namba ya mke wangu na baada ya maelezo hayo aliniomba nisizime simu yangu wakati wakiwa wanashughulika na kuisajili na kwamba muda wowote nitapatiwa maelekezo,” alieleza mbunge huyo.


Kilichotokea baada ya muda ni kwamba simu yangu, haikuweza kufanya kazi, hatua hiyo iliyonilazimisha kuwasiliana na watoa huduma wa kampuni hiyo huko jimboni ili kujua tatizo ni nini, lakini kila aliyejaribu kuirejesha katika mawasiliano alinijibu kuwa haiwezekani mpaka makao makuu,” alisema Mbasa.


“Kila wakala wa Airtel niliyemfuata na kumweleza kuwa simu yangu haifanyi kazi, alipoingia kwenye mtandao wao kwa ajili ya kuirejeshea mawasiliano alinijibu kuwa hiyo haiwezekani mpaka makao makuu ya kampuni hiyo,” alisema.


Mbunge huyo alisema majibu hayo yalimlazimisha kutulia bila mawasiliano hadi Januari mwaka huu alipokwenda katika Makao Makuu ya Aritel na kufanikiwa kuirejeshea simu yake mawasiliano.


Dk Mbasa alisema baadaye aligundua kuwa wakati simu yake ikiwa imekosa mawasiliano watu hao walikuwa wakishughulikia kuhamisha fedha zake kutoka katika akaunti yake.


Alisema Januari 6, mwaka huu alifanikiwa kwenda Tawi la Benki ya NMB la Mazengo ambapo baada ya kuangalia salio katika akaunti yake, alibaini kuwapo kwa wizi huo na baadaye aliwasiliana na maofisa wa benki hiyo ambao walimthibitishia kuwa ameibiwa.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, maofisa hao walimpatia fomu za kujaza, ili kusitisha kutumia huduma ya `Sim Banking’ katika akaunti yake.


Dk Mbasa alisema baadaye aliwasiliana na meneja wa benki hiyo na kutakiwa kuandika maelezo ya wizi ikiwa ni pamoja na kukabidhiwa kwa wataalamu wa masuala ya ufuatiliaji wa uhalifu kwa njia ya mitandao.


Alisema baada ya kuangalia katika mtandao, wataalamu hao walibaini kuwa fedha zake zilitolewa na wahusika katika kipindi cha kati ya Desemba 20 mwaka jana na Januari 3, mwaka huu.


“Kwa mujibu wa mtandao wa Benki inaonyesha fedha zangu zilitolewa kwa kutumia huduma ya `Sim Banking’ ya NMB Mobile ambapo zilikuwa zikihamishwa kutoka katika akaunti yangu kwenda `Pesa Faster Collection’ na kwa watu wengine wawili,” alifafanua.


Alisema kutokana na maelezo hayo ya NMB, alilazimika kufungua jalada katika Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Wizi kwa Njia ya mtandao lakini, hadi sasa hakuna lolote lililofanyika. Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, David Misime alisema hana kumbukumbu kuhusu madai ya mbunge huyo kuibiwa na kuomba muda ili afuatilie kwa maofisa wake.

Meneja wa Kanda ya Ziwa wa Kampuni ya Simu ya Mkononi Airtel, Ally Maswanya alisema hakuna zoezi la uhakiki wa namba lililoendeshwa na kampuni yake na kwamba anavyotambua kuna watu wahuni ambao wamekuwa wakijifanya kuwa ni maofisa wa kampuni na kisha kuziingilia namba za wateja wao.