Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amewatolea uvivu
wanasiasa na kuwaambia wao ndiyo wanaokuza suala la mgogoro wa mpaka wa
Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi.
Dk. Mwakyembe alitoa kauli hiyo jana baada
ya kutembelea bandari ya Kiwira iliyopo wilayani Kyela kukagua shughuli
za ujenzi na kukuta meli kubwa ya mizigo ijulikanayo kama Katundu mali
ya serikali ya Malawi ikiwa imetia nanga katika ardhi ya Tanzania
ikipakia shehena ya mbolea katika bandari hiyo.
Dk. Mwakyembe alisema toka zamani
watumiaji wa ziwa hilo wanafahamu kwamba ukifika eneo fulani ndani ya
ziwa hilo unakuwa eneo la Tanzania au Malawi na hivyo chombo husika
kikifika katika nchi husika kinalazimika kupeperusha bendera ya nchi
hiyo. Alisema haiingii akilini kama wanasiasa wanawapotosha wananchi wa
nchi hizo kwa manufaa yao binafsi kwani suala la mgogoro wa mpaka huo
halijaathiri sekta ya usafirishaji.
Akizungumza na wafanyakazi wa bandari
hiyo, aliwahakikishia watumiaji wa Ziwa Nyasa kuwa sekta ya usafirishaji
haijakumbwa na tofauti hizo za mipaka ndani ya ziwa hilo na hivyo
shughuli za usafirishaji zinaendelea kama kawaida.
Kwa upande wake nahodha wa meli ya
Katundu, Kapteni Mponda alipongeza juhudi zinazofanywa na serikali ya
Tanzania kujenga bandari ya Kiwira ambayo inakuwa bandari ya pili kubwa
kwa upande wa Tanzania ikiwemo bandari ya Itunge.
Mgogoro wa mpaka kati ya Malawi na
Tanzania umedumu kwa muda mrefu hivi sasa unasuluhishwa na marais
wastaafu, Joachim Chisano wa Msumbiji na Thabo Mbeki wa Afrika Kusini.
Mwezi uliopita, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, wakati akizungumza na waandishi
wa habari jijini Dar es Salaam, alisema marais hao wastaafu walienda
Malawi kukutana na Rais Joyce Banda.
No comments:
Post a Comment