facebook likes

Monday, August 12, 2013

Polisi yashikilia wawili mauaji ya bilionea Moshi.


???????????????????????????????Marehemu Erasto Msuya enzi za uhai wake
Wakati bilionea mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite yanayopatikana Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, marehemu Erasto Simon Msuya (43) akitarajiwa kuzikwa kesho nyumbani kwao mtaa wa Kairo,

....SOMA ZAIDI.....
Mji mdogo wa Mirerani, polisi imewatia mbaroni watu wawili wakihusishwa katika mtandao uliofanya mauaji ya mfanyabiashara huyo.
Mfanyabiashara huyo anayemiliki vitega uchumi kadhaa katika miji hiyo, aliuawa Agosti 8, mwaka huu katika eneo la Mjohoroni wilayani Hai baada ya kumiminiwa risasi zaidi ya 20 za bunduki ya kivita aina ya SMG.
Habari zilizopatikana jana Arusha, zilidokeza kuwa washukiwa hao walikamatwa siku ya tukio huko Sanyajuu wilayani Siha, kilomita chache kutoka mahali ilipotelekezwa pikipiki iliyotumika katika mauaji hayo.
Pikipiki hiyo mpya ilitelekezwa katika Kijiji cha Olkolili baada ya kupata pancha gurudumu la mbele na watu waliokuwa wakiitumia waliiacha na kuamua kutembea kwa miguu.
Habari zinadai kuwa watu hao wawili sio waliomfyatulia risasi mfanyabiashara huyo bali wana ‘taarifa muhimu’ zinazohusiana na mpango mzima wa mauaji hayo na mtandao wa watuhumiwa waliohusika.
Inadaiwa kuwa baada ya wauaji wa mfanyabiashara huyo kutelekeza pikipiki hiyo, ‘waliwezeshwa’ kutoroka kupitia Wilaya ya Simanjiro na baadaye kuingia jijini hapa ingawa hawajulikani mahali waliko.
“Ni kweli kuna watu wawili walikamatwa na wanashikiliwa kule Makao Makuu ya Polisi Moshi na kila siku wanaletwa hapa Arusha kwa ajili ya uchunguzi wa kuwatafuta wahusika hasa,” alidokeza polisi mmoja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas hakupatikana jana kuelezea zaidi baada ya simu yake kutokupatikana.
Ofisa huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema hata hiyo jana, timu ya wapelelezi kutoka Moshi wakiongozwa na RCO Kilimanjaro, Ramadhan Ng’anzi walikuwapo jijini hapa na watuhumiwa hao.
Uchunguzi zaidi wa polisi kuhusu mmiliki halali wa pikipiki iliyokuwa ikitumiwa na vijana wawili waliotekeleza mauaji hayo, zimebaini kuwa bado inamilikiwa na kampuni moja ya Dar es Salaam iliyouza pikipiki hiyo.
Habari zaidi zinadai kuwa pikipiki hiyo ilinunuliwa mahususi kwa ajili hiyo na mwanamke mmoja ambaye hafahamiki na ilinunuliwa katika duka ambalo ni tawi la kampuni iliyoingiza pikipiki hiyo lililopo Arusha.
Mfanyabiashara huyo ambaye anatarajiwa kuzikwa kesho, huko Mirerani, aliuawa baada ya kuitwa kwa simu na wauaji waliojifanya ni vijana wenye madini ya Tanzanite waliotaka kumuuzia marehemu. Hata hivyo, marehemu alipofika eneo hilo akiwa na gari lake la kifahari aina ya Range Rover toleo jipya, alishuka kwenda kuzungumza na vijana hao mita kama 70 kutoka kwenye gari lake na ndipo alipomiminiwa risasi.
Inadaiwa kuwa baada ya vijana hao kumuua, walichukua begi jeusi lililokuwa na fedha ambazo angezitumia kununulia madini hayo lakini hawakuchukua simu wala bastola ya marehemu anayoimiliki kihalali.
Kumekuwapo na taarifa zinazotatanisha kuhusu kiasi hasa kilichoibwa huku taarifa zikidai ni Sh50 milioni na nyingine zikidai ni Sh120 milioni.
Wiki iliyopita, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alikaririwa na gazeti hili akikanusha taarifa kuwa ndani ya gari la marehemu kulikuwapo na kiasi cha fedha Sh150 milioni kilichokutwa.
Mazishi kufanyika kesho
Akizungumza na gazeti hili jana, Shujaa Godfey ambaye ni shemeji wa marehemu Msuya, alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (Seliani) na mazishi yatafanyika kesho.
Shujaa alisema mtoto mkubwa wa marehemu, Simon Erasto ambaye anasoma nchini Australia, aliwasili jana Jumapili kwa ndege baada ya kutua Dar es Salaam na kupanda tena ndege iliyomshusha Kia kwa ajili ya kushiriki mazishi kesho.
“Kabla ya kifo chake, marehemu Msuya aliacha wosia kuwa azikwe mtaa wa Kairo na misa ya mazishi yake ifanyike kwenye Kanisa la Lutherani lililopo Kairo ambalo alichangia nguvu kubwa katika kulijenga,” alisema Shujaa.
Kifo cha Msuya kilichotokea Jumatano iliyopita ya Agosti 7 mwaka huu, kwa kuuawa kwa kupigwa risasi zaidi ya 20, kiliacha gumzo kwenye miji ya Arusha Moshi na Mji mdogo wa Mirerani ambapo ndipo nyumbani kwao.
Katika mazishi ya kesho, watu mbalimbali maarufu nchini wanatarajia kushiriki wakiwamo wa chama na Serikali, wabunge na viongozi wa vyama vya kisiasa kwani enzi za uhai wake Msuya alikuwa kada maarufu wa CCM.
Shujaa alisema marehemu Msuya alizaliwa mwaka 1970 huko Shighatini wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro na alipata elimu ya msingi shule ya Shighatini mwanzoni mwa miaka ya 80 na mwanzoni mwa miaka ya 90 akajiunga na Shule ya Sekondari Makumira iliyopo mji mdogo wa Usa River wilayani Arusha kwa kidato cha nne na kisha akajiunga na Shule ya Sekondari Tanga kwa kidato cha sita.
“Mwishoni mwa miaka ya 90 alichaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu Dar es salaam kusomea Shahada ya Uchumi ila aliacha kwenda na akawa anajishuhulisha na uchimbaji na ununuzi wa madini,” alisema Shujaa.
Alisema ameacha mke na watoto wanne, wawili wa kike na wawili wa kiume na ameacha rasilimali nyingi zikiwamo nyumba ya kifahari,migodi,hoteli maarufu za SG Resort na Mezza Luna zilizopo Arusha.

Pia, ameacha magari mengi ya kifahari ikiwemo Range Rover Vogue (New Model) ambalo alikuwa nalo wakati akipigwa risasi kwenye eneo la mijohoroni (kwa wasomali) kati ya Boma ng’ombe wilayani Hai na uwanja wa ndege wa Kia.

Chanzo: mwananchi .

No comments:

COMMENTS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...