Kwa mujibu wa taarifa za benki, mtuhumiwa huyo
ambaye hakutajwa jina lake alikamatwa baada ya kamera maalumu
zilizowekwa kwenye ATM za BOA, kumtambua kuwa ni mwizi sugu wa benki
hiyo anayetafutwa.
Mmoja wa wafanyakazi wa benki hiyo ambaye
hakupenda kutajwa jina kwa kuwa si msemaji, alisema tukio hilo lilitokea
jana saa 12 asubuhi baada ya mtuhumiwa huyo kuwekewa mitambo maalumu ya
kumnasa.
Alisema benki hiyo ilipelekewa malalamiko na
baadhi ya wateja kwamba wakienda kutoa fedha kwenye ATM wanakuta akaunti
zao hazina salio wakati wanaamini zilikuwa na fedha.
Chanzo hicho cha habari kilidai kuwa baada ya
kupelekewa malalamiko hayo, waliweka mitambo maalumu ya kuwawezesha
walinzi wa maeneo ya ATM za BOA kumbaini mtu atakayetoa fedha kwa njia
ya wizi.
“Kama Benki tuliweka mtambo maalumu na mtuhumiwa
huyo alionekana kwenye mtambo wetu, hivyo tuliwaagiza walinzi wetu
watakapomwona mtu huyo wamkamate haraka sana,”alisema.
Alisema mtuhumiwa huyo alianza mchezo huo kwa muda
mrefu ambapo kwa kutumia kadi za ATM zisizojulikana idadi yake, alikuwa
anakwenda kwenye ATM mbalimbali za benki hiyo na kutoa fedha hadi Sh10
milioni.
Kuhusu tukio la jana, mmoja wa walinzi wa BOA
aliyejitambulisha kwa jina moja la Frenky alisema mtuhumiwa huyo
alipofika kwenye ATM hiyo aliingia na kuchukua fedha ambazo alizipeleka
kwenye gari lake. Frenky alisema baada ya kupeleka fedha hizo, alirudi
kwa mara ya pili ili achukue fedha nyingine ndipo walinzi hao
walimkamata na kumfunga pingu.
“Huyu mtuhumiwa mwenye asili ya Kiarabu alifika na
gari lake saa 12 asubuhi, aliingia kwenye ATM na kutoa fedha ambazo
hazikujulikana ni shilingi ngapi na kuzipeleka kwenye gari lake, baadaye
alirejea tena kwa ajili ya kutoa fedha zingine, wakati anaingia ndipo
alipokamatwa na mlinzi aliyekuwa analinda hapo,” alisema Frenky.
Kamanda wa Polisi Kinondoni, Camilius Wambura
alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na
jeshi hilo huku uchunguzi dhidi yake ukiendelea.
“Ni kweli taarifa nimezipata, mtuhumiwa
amekamatwa, bado hatujajua ni kiasi gani ambacho ameiba kwa kutumia
mtandao, tunaendelea na uchunguzi,” alisema Wambura.
Tukio kama hili lilishawahi kutokea mkoani Mwanza
Februari 19 mwaka huu na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kwa kushirikiana
na maofisa ya Benki ya NMB liliwatia mbaroni watu watatu ambao walidaiwa
kuiba kiasi cha Sh700 milioni kwa nyakati tofauti.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi, Christopher Fuime alisema
watuhumiwa hao walinaswa baada ya kuwekewa mtego na maofisa wa benki na
polisi saa 6 usiku wa Februari 19, mwaka huu na mtuhumiwa mmoja
alibambwa akichukua fedha kwenye ATM ya NMB kwenye Tawi la PPF Plaza
Mwanza.
Vifaa walivyokutwa navyo ni kadi bandia 194 za
kuchukulia fedha katika ATM za NMB na kati yake kadi 95 zilikuwa na
namba 0225152975 zilizotumia namba ya akaunti ya 2258103695 zenye jina
na picha ya mtu anayedaiwa kuwa ni Moley L.P.
Kadi nyingine 99 zilikuwa na namba 0506056317 za akaunti namba 5068000322 zikitumia jina moja la Mnuo Z.E na picha moja.
Mbali na kadi hizo waliweza kunasa kadi 36 za
Benki ya DTB ambazo kati yake kadi 18 zilikuwa na jina moja la Kelvini G
Gratias na namba 20497883, kadi 12 zilitumika jina la J.Paul zenye
akaunti namba 2049783 huku kadi sita zikitumia jina moja la Joseph
Donald akaunti namba 2049783.
Kadi nyingine tatu zenye maandishi ya Download
list na nyingine ikiwa ni kadi ya Visa ya Benki ya KCB yenye namba
413546040003827 zilitumia jina la Elikana Zacharia.
chanzo:Gazeti la Mwananchi
chanzo:Gazeti la Mwananchi
No comments:
Post a Comment