Denis Goldberg akishuka kwenye gari hospitalini alikolazwa Mandela Jumatatu iliyopita alipokwenda kumtembelea. Rafiki
mmoja wa karibu wa Nelson Mandela jana alidai kwamba rais huyo wa
zamani wa Afrika Kusini anayeumwa alikuwa 'mwenye fahamu zake kamili'
wakati alipomtembelea hospitalini wiki hii.
Denis
Goldberg, mwanaharakati mweupe wa kupinga ubaguzi wa rangi na mfuasi wa
chama tawala cha African National Congress (ANC), alihitilafiana na
maoni ya kitabibu yaliyowasilishwa mahakamani wiki hii, ambayo yanaeleza
kwamba Mandela amekuwa kwenye 'hali ya kulala tu' kwa siku tisa
zilizopita na familia yake ilikuwa ikijadiliana kuhusu kuzima mashine
zake za kuokolea maisha. Ripoti hizo za kitabibu juu ya hali ya
Mandela zimeibuka wakati wa kesi ya mahakamani wiki hii kati ya
wanafamilia ya Mandela wanaovutana wakigombea kuhusu wapi atakapozikwa
mshindhi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel. Goldberg, ambaye alifungwa
jela kwa miaka 22 wakati wa mashitaka maarufu ya Rivonia ya mwaka 1964
ambayo yalishuhudia Mandela akihukumiwa kifungo cha maisha, alisisitiza
kwamba alimtembelea Mandela Jumatatu na kwamba alimwona 'dhahiri ni mtu
anayeumwa sana, lakini alizisikia sauti na kujaribu kuongea." Aliongeza:
"Alikuwa amelala fofofo wakati nilipoingia pale. Nilizungumza na
kumweleza mimi ni nani na akafungua macho yake na kunitazama. Niliongea
naye kwa takribani dakika kumi na alionesha kuelewa nilichokuwa
nikiongea. Alinitambua mimi ni nani." Goldberg, ambaye alitumikia
hukumu yake kwenye gereza la wazungu mjini Pretoria wakati Mandela
alisafirishwa kwa meli kwenda Kisiwa cha Robben, alisema Mandela mwenye
miaka 94 'alikuwa hana nguvu lakini alikuwa mwenye fahamu zake kamili." Aliongeza:
"Hakuweza kujibu sababu hawezi kuongea, akiwa na mipira kwenye koo
lake, lakini alikuwa akitingisha taya lake kana kwamba anataka kuongea.
Hakika nilishangaa sana - baada ya taarifa nilizokuwa nimezisikia." Huku
wengi wa watu wa Afrika Kusini wamekata tamaa kwenye ukweli kwamba
Mandela hawezi kupona, taarifa zinazokinzana kuhusu afya yake
zimesababisha hofu kuu, huku mmoja wa watangazaji akiishutumu serikali
ya ANC kwa kupotosha umma. |
No comments:
Post a Comment