facebook likes

Saturday, August 3, 2013

USAJILI WA WACHEZAJI SASA MWISHO AGOSTI 5


Usajili wa wachezaji kwa hatua ya kwanza msimu huu (2013/2014) sasa utafungwa Jumatatu (Agosti 5 mwaka huu) badala ya Agosti 3 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa awali.Uamuzi wa kusogeza mbele umetokana kuchelewa kupata disc ya usajili msimu huu ambayo ndiyo inayotumika kwa usajili wa elektroniki unaofanywa kwa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom. Disc hiyo ambayo hutolewa na kampuni ya NAS Technology ya Tunisia tayari imeshawasili.
Kutokana na mabadiliko hayo, sasa kipindi cha pingamizi kitakuwa kati ya Agosti 6 na 12 mwaka huu wakati Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji itakutana Agosti 13 na 14 mwaka huu kupitia na kufanyia uamuzi usajili wa wachezaji wenye matatizo.
Hatua ya pili ya usajili itaanza tena Agosti 15 mwaka huu ikihusisha wachezaji ambao watakuwa hawajasajiliwa katika Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu. Timu zitakazoruhusiwa kusajili ni zile ambazo zitakuwa hazijajaza nafasi zote za usajili. Dirisha dogo za usajili litafunguliwa kuanzia Novemba 15 mwaka huu hadi Desemba 15 mwaka huu.
Pia klabu za Ligi Kuu ya Vodacom zinapowasilisha usajili wao zinatakiwa kuambatanisha nyaraka zinazoonesha viwanja vyao vya mazoezi, nakala za bima kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi. Masuala hayo yameelezwa kwenye Kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom
KAMISHNA RWIZA KUSIMAMIA MECHI YA CHAN
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Alfred Rwiza wa Tanzania kuwa kamishna wa mechi ya raundi ya pili ya michuano ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).
Rwiza atakuwa kamishna katika mechi ya kwanza ya raundi hiyo itakayohusisha mshindi wa mechi kati ya Msumbiji na Namibia dhidi ya Angola itakayochezwa kati ya Agosti 9 na 11 mwaka huu. Mechi hiyo itachezeshwa na refa Noram Matemera kutoka Zimbabwe.
Matemera atasaidiwa na Wazimbabwe wenzake Tapfumaney Mutengwa atakayekuwa mwamuzi msaidizi namba moja, Ncube Salani ambaye ni mwamuzi msaidizi namba mbili wakati mwamuzi wa mezani (fourth official) ni Ruzive Ruzive.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

COMMENTS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...