Serikali ya Tanzania imewarejesha kwao kwa hiari wakimbizi wapatao569,018 toka nchi za Maziwa Makuu waliokuwa wamehifadhiwa hapa nchini kutokana na machafuko katika nchi zao. Kati ya hao 502,358 walitoka nchini Burundi na 66,660, Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo. Wakimbizi hawa wamerejeshwa kwao kufuatia
zoezi lililoanzishwa rasmi mwaka 2002 kwa wakimbizi toka Burundi na
mwaka 2005 kwa wakimbizi toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRS),
baada ya usalama katika nchi zao kuimarika.
Sambamba na mafanikio haya, pia kambi 12 kati ya 13 zilizokuwa
zikitumika kuwahifadhi wakimbizi hawa zimefungwa, na hadi sasa ni kambi
moja tu ya wakimbizi ya Nyurugusu, wilayani Kasulu mkoani Kigoma ndiyo
iliyobakia ikiwahifadhi wakimbizi kutoka DRC (63,728), Burundi (4,153) na nchi nyingine mchanganyiko za Kiafrika (212).
Tanzania
inajulikana kimataifa kama nchi mojawapo ambayo imechangia kwa kiasi
kikubwa kutoa hifadhi kwa wakimbizi wanaokimbia nchi zao kutokana na
machafuko ya kiaiasa ambapo mwaka 1995 idadi yao ilifikia zaidi ya
milioni moja.
Lengo
la Serikali ni kuona kuwa suala la kuhifadhi wakimbizi hapa nchini
linafikia ukomo na juhudi zinaendelea kuona kuwa hata Kambi ya Nyarugusu
ambayo ndiyo kambi pekee iliyobakia inafungwa baada ya wakimbizi walio
katika kambi hiyo kurejeshwa kwao, pale hali ya usalama nchini DRC
itakapokuwa imeimarika.
Kuondoka
kwa wakimbizi hawa sasa kunatoa nafasi kwa Serikali na wananchi kutumia
kwa shughuli nyingine za kimaendeleo maeneo makubwa yaliyokuwa
yanatumika kuhifadhi wakimbizi, lakini pia kunatoa nafasi nzuri ya
kuweza kukabiliana na changamoto za kiusalama katika maeneo hayo ambayo
yapo katika mikoa ya mpakani mwa nchi.
Serikali
inapenda kuishukuru Jumuiya ya Kimataifa kupitia Shirika la Umoja wa
Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), kwa misaada ya hali na mali
waliyotoa na wanayoendelea kutoa kusaidia hifadhi ya wakimbizi hapa
nchini. Pia Watanzani wote na hasa wale wa mikoa ya Katavi, Kigoma na
Kagera kwa ushirikiano waliotoa kwa wakimbizi waliokuwa wamehifadhiwa
katika maeneo yao, na nchi za Burundi, Congo kwa ushirikiano wao
uliowezesha kuwarejesha raia wao waliokuwa wamehifadhiwa hapa nchini.
Mashirika
mengine ambayo pia yalihusika na yanaendelea kutoa huduma za kibinadamu
kwa wakimbizi ni pamoja na Shirika la Chakula Duniani (WFP), Mfuko wa
Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF), Kamati ya Kimataifa ya
Uokozi (IRC), na Shirila la Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS).
Imeandaliwa na Felix Mwagara
KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
No comments:
Post a Comment