facebook likes

Saturday, August 3, 2013

Tume: Hakuna gharama kuendesha Serikali tatu


Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole akizungumza jambo.

Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, imewabeza watu, hususan wanasiasa wanaosimama majukwaani kueleza Muundo wa Muungano wa Serikali tatu utaongeza gharama za kiuendeshaji kuwa ni uongo na sababu hizo hazina tija.
Mjumbe wa Tume hiyo, Humphrey Polepole alisema hayo jana wakati wa mkutano wa kuijadili Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba Mpya mbele wa Wajumbe wa Baraza la Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara.
Alisema Muundo wa Serikali tatu hauna gharama zozote kwani chanzo cha mapato cha kuongoza Serikali ya Muungano kuwa tayari kimebainishwa.
Polepole alisema gharama za kuongoza Serikali hiyo zitatokana na Kodi ya Ushuru wa Bidhaa ambapo jumla yake zinazokusanywa si chini ya  Sh1 trilioni.
 “Mpaka sasa Serikali ya Muungano inakusanya zaidi ya Sh3 trilioni hivyo kama itatumika  Sh1 trilioni na zitakazobaki zitaelekezwa katika shuguli zingine, fedha zitakuwepo,” alisema Polepole na kuongeza:
 “Nashangaa wanasiasa wanaosimama majukwaani kueleza wananchi kuwa kutakuwa na mzigo wa gharama, hii si kweli kwani Tume tumekwisha bainisha chanzo chake cha mapato na hao wanaozungumza hayo hawafuatilii mchakato kwa umakini.”
 Alisema uchambuzi walioufanya juu ya kodi inayokusanywa mwaka 2003/04 zilikusanywa jumla ya Sh500 bilioni na mwaka 2011/12 zilikusanywa Sh1 trilioni ambapo kila mwaka mapato hayo yanaongezeka.
 “Uzoefu unaonyesha kila mwaka mapato yanaongezeka hivyo uwepo wa Muungano wa Serikali tatu ni dhahiri hautaathiri kitu chochote na utasaidia kutatua kero zilizopo zinazojitokeza kila mwaka kila kukicha,” alisema Polepole
 Polepole aliwataka Wananchi kutokuwa na shaka na mapendekezo hayo ya Tume juu ya Muundo wa Muungano kuwa wa Serikali tatu kwani utapunguza malalamiko ya muda mrefu yaliyopo.
 “Hivi sasa kuna kero zaidi ya 47 na kwa Muungano huu uliopo hautamaliza na wala hauwezi kuyafanyia kazi lakini kutokana na mapendekezo ya Tume ya Serikali tatu ninahakika yatapungua na kila upande kutokuwa na  malalamiko,” alisema Polepole.
Polepole amesisitiza kwa kuwaomba wananchi kuendelea kutoa maoni katika hali ya kutoshinikizwa kwa namna yoyote.
“Kila mtu anapaswa kuwa huru kutoa maoni yake bila kuogopa chochote. Lengo la uwepo wa katiba mpya ni kujua hitaji hasa la wananchi ni nini na kwamba katika kutoa maoni wananchi wanapaswa kufanya hivyo bila woga,” alisisitiza Polepole.
chanzo;mwananchi.

No comments:

COMMENTS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...