Utangulizi
Ndugu wananchi;
Kama ilivyo ada naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa
rehma, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kwa mara nyingine tena
kutekeleza utaratibu wetu huu mzuri tuliojiwekea wa Rais kuzungumza na
taifa kila mwisho wa mwezi.
Ndugu Wananchi;
Mwezi Julai, 2013 ulikuwa wa neema kubwa ya wageni kwa nchi yetu
wakiwemo watu na viongozi mashuhuri duniani. Natoa shukrani nyingi kwa
Watanzania wenzangu kwa jinsi tulivyowapokea wageni wetu zaidi ya 1,700.
Wamefurahi kuwepo kwao nchini na wameondoka wakiwa na kumbukumbu nzuri
ya nchi yetu. Wageni wetu wamekuwa wa manufaa makubwa kwa nchi yetu.
Wamesaidia kuitangaza Tanzania duniani na kuendeleza fursa za kukuza
utalii, biashara na uwekezaji nchini na kwingineko katika Afrika.
Mkutano wa Smart Partnership
Ndugu wananchi;
Wageni wetu wa kwanza ni wale waliokuja kuhudhuria Mkutano wa Global
2013 Smart Partnership Dialogue uliofanyika Dar es Salaam tarehe 28 Juni
hadi 1 Julai, 2013. Mkutano huo ulihudhuriwa na watu zaidi ya 800
kutoka mabara yote duniani wakiwemo Watanzania. Miongoni mwa
waliohudhuria ni pamoja na wakuu wa nchi na Serikali, viongozi wastaafu,
wanadiplomasia, wawakilishi wa mashirika na taasisi za kimataifa,
makampuni ya ndani na nje, wafanyabiashara, wasomi, asasi za kijamii na
watu wa makundi mbalimbali katika jamii. Makampuni yetu 21 nayo
yaliungana na makampuni mengine 28 kutoka nje ya nchi kushiriki kwenye
maonesho ya matumizi ya sayansi na teknolojia yaliyofanyika sambamba na
mkutano huo.
Ndugu Wananchi;
Agenda kuu ya majadiliano ya mwaka huu ilikuwa ni “Matumizi ya
teknolojia kama nyenzo ya kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi Barani
Afrika (Leveraging Technology for Africa’s Social-Economic
Transformation: The Smart Partnership Way). Tuliichagua mada hii kwa
kuwa ni ukweli ulio wazi kuwa matumizi ya sayansi na teknolojia ndiyo
chachu kubwa iliyoleta mageuzi na maendeleo ya kiuchumi na kijamii
katika nchi. Ndiyo siri ya mafanikio katika nchi zilizoendelea na
zinazopiga kasi kubwa ya maendeleo duniani.
Bahati
mbaya sana kumekuwa na maendeleo na matumizi madogo ya sayansi na
teknolojia katika Afrika. Ndiyo maana nchi za Afrika ziko nyuma
kimaendeleo ukilinganisha na zile zilizoendelea. Katika mkutano huo
umuhimu wa kuendeleza na kuongeza matumizi ya sayansi na teknolojia kwa
ajili ya maendeleo Barani Afrika ulitambuliwa na kusisitizwa.
Mkutano
ulihimiza na kusisitiza kuwa sera, mikakati na mipango ya maendeleo ya
nchi za Afrika zitoe kipaumbele kwa kuendeleza matumizi ya sayansi na
teknolojia. Nchi zetu zimehimizwa kuwekeza katika elimu ya sayansi na
teknolojia pamoja na kujenga uwezo wetu wa ndani wa uvumbuzi, ubunifu,
umiliki na uendelezaji wa sayansi na teknolojia. Aidha, imesisitizwa kwa
nchi zetu ziongeze kasi ya kutumia sayansi na teknolojia katika
shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii ili kuongeza ufanisi na kasi
ya maendeleo.
Ndugu Wananchi;
Jambo la kutia faraja kwetu nchini ni kwamba mambo yote hayo
tunayafanya. Tunachotakiwa sasa ni kufanya vizuri zaidi na kuongeza
uwekezaji na kasi ya kuendeleza matumizi ya sayansi na teknolojia katika
shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Tutaendelea
kuboresha sera, kuboresha mazingira ya uwekezaji na kwa ajili ya
maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini.
Ziara ya Rais wa Marekani Nchini Tanzania
Ndugu wananchi;
Mgeni wetu wa pili alikuwa Rais wa Marekani, Mheshimiwa Barack Obama,
aliyefanya ziara nchini kwetu kati ya tarehe 1 - 2 Julai, 2013. Lengo la
ziara yake ilikuwa kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya
Marekani na Tanzania. Kama mjuavyo, nchi zetu mbili zina uhusiano wa
kibalozi tangu Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 na Mapinduzi Matukufu ya
Zanzibar mwaka 1964.
Uhusiano
wetu umepita katika vipindi mbalimbali na kwamba hivi sasa umekuwa mzuri
zaidi kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi zetu mbili.
Kumekuwepo na ongezeko kubwa la misaada ya maendeleo kutoka Marekani na
uwekezaji wa vitega uchumi na biashara navyo vinakua. Pia ziara za
kiserikali za viongozi wa nchi zetu kutembeleana zimeongezeka. Kama
mtakavyokumbuka, mwaka 2008 aliyekuwa Rais wa Marekani Mheshimiwa George
W. Bush alifanya ziara ya siku nne nchini. Pia Mawaziri mbalimbali wa
Serikali ya Marekani wametembelea Tanzania akiwemo Mheshimiwa Hilary
Clinton akiwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani aliyekuja mwaka 2011.
Ndugu Wananchi;
Nchi ya Marekani imekuwa mshirika wetu muhimu wa maendeleo katika nyanja
mbalimbali. Kwa upande wa afya kwa mfano, tunapata msaada mkubwa katika
mapambano dhidi ya malaria na UKIMWI. Katika maendeleo ya elimu, nako
wanatusaidia katika mafunzo ya wataalamu mbalimbali pamoja na
upatikanaji wa vitabu vya sayansi na hisabati kwa ajili ya shule za
sekondari. Kupitia Mfuko wa Changamoto za Milenia, Marekani inatusaidia
katika kuimarisha miundomuinu ya barabara, umeme na maji. Ujenzi wa
barabara za Tanga – Horohoro, Namtumbo – Songea – Mbinga; Tunduma –
Sumbawanga na baadhi ya barabara za Pemba, ujenzi wa njia ya pili ya
kupeleka umeme Unguja kutoka Dar es Salaam, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa
Mafia na usambazaji wa umeme katika Mikoa 10 ya Tanzania bara ni
miongoni mwa matunda ya msaada wa Mfuko huo. Pamoja na hayo, ipo miradi
ya kuongeza maji katika jiji la Dar es Salaam na Manispaa ya Morogoro
ambayo inaendelea kutekelezwa.
Ndugu Wananchi;
Wakati wa ziara yake, Rais Obama alielezea na kusisitiza dhamira yake na
ya Serikali yake ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri
uliopo kati ya nchi zetu. Alielezea kuridhika na hatua tuliyofikia ya
kukuza demokrasia nchini, utawala bora na kuwekeza katika maendeleo ya
watu wetu. Aliahidi kuendelea kuunga mkono juhudi zetu. Katika hili
ameahidi kuongeza misaada ya maendeleo na kiufundi katika sekta za afya,
elimu, kilimo, barabara, nishati na maendeleo ya vijana. Pia,
alithibitisha kwamba nchi yetu itaendelea kunufaika na ufadhili wa Awamu
ya Pili ya Mfuko wa Changamoto za Millenia. Katika awamu hii, maeneo
yatakayopewa kipaumbele hapa kwetu ni umeme na barabara za vijijini.
Mazungumzo ya miradi itakayotekelezwa katika awamu hiyo yanaendelea
vizuri.
Power Africa
Ndugu Wananchi;
Rais Obama alitumia fursa ya ziara yake nchini kuzindua mpango wa
Serikali yake wa kusaidia maendeleo ya sekta ya umeme katika Bara la
Afrika. Mpango huu unaoitwa “Power Africa Initiative” umetengewa kiasi
cha dola za Marekani bilioni 7 na Serikali ya Marekani na makampuni
binafsi ya nchi hiyo yameahidi kuwekeza dola bilioni 9 katika mpango
huo. Kwa kuanzia, nchi sita za Afrika (Ethiopia, Ghana, Nigeria,
Tanzania, Liberia na Kenya) ikiwemo Tanzania zitahusishwa.
Bila ya
shaka Mpango huo ukikamilika utasaidia sana kuimarisha upatikanaji wa
umeme barani Afrika ambayo ni nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo ya
kiuchumi na kijamii. Ni ukweli ulio wazi kuwa ukosefu wa umeme wa
kutosha na wa uhakika ni sababu kubwa inayokwamisha maendeleo ya haraka
katika nchi za Afrika. Hivyo basi, msaada huu ni muhimu sana kwetu. Kwa
ajili hiyo nimeagiza Wizara ya Nishati na Madini iandae mkakati
madhubuti wa namna Tanzania itakavyoshiriki na kufaidika na mpango huo.
Nataka mpango huo utakapoanza kutekelezwa utukute sisi tupo tayari
kutumia fursa zake.
Vile
vile, ndugu wananchi, katika ziara hiyo Rais Obama alielezea nia ya
Serikali yake kutaka kuwepo mpango wa kukuza ushirikiano wa biashara na
uwekezaji baina ya nchi yake na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Nimeelekeza Wizara husika yaani Wizara ya Ushirikiano wa Afrika
Mashariki na Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko nao watengeneze
mkakati utakaoonesha jinsi tulivyojipanga kufaidika na mpango huo.
Lazima tujiandae vyema na mapema tunufaike saiwa na mpango huo.
Ziara ya Rais Mstaafu wa Marekani Nchini
Ndugu Wananchi;
Sambamba na ziara ya Rais Obama, nchi yetu ilipata bahati ya kutembelewa
tena na Rais Mstaafu wa Marekani, Mheshimiwa George W. Bush na mkewe
Laura Bush, tarehe 1 hadi 3 Julai, 2013. Kwa udhamini wa asasi ya George
W. Bush Foundation waliandaa Mkutano wa Wake wa Marais wa Afrika
uliofanyika hapa Dar es Salaam, tarehe 2 na 3 Julai, 2013. Mama Michelle
Obama naye alishiriki mkutano huo uliozungumzia kuimarisha maendeleo na
afya ya wanawake Barani Afrika.
Katika
mkutano huo, pia, Mheshimiwa George W. Bush alizindua mpango wa
kuimarisha mapambano dhidi ya kansa ya shingo ya kizazi na matiti barani
Afrika. Kufuatia Mpango huo, Serikali ya Marekani imetoa dola milioni 3
na mashine 16 za Cryo Therapy zinazotumia baridi kali kuua chembechembe
za kansa. Msaada huo ni muhimu hasa ukizingatia kuwa kila mwaka hapa
nchini zaidi ya Watanzania 21,000 wanapata maradhi ya kansa. Kati ya hao
asilimia 29.4 ni wanawake wanaopata magonjwa ya kansa ya shingo ya
uzazi na asilimia 6.2 wanapata kansa ya matiti. Naamini Mpango huu
utatusaidia sana katika kuimarisha mapambano dhidi ya maradhi haya
yanayowasumbua na kuua kina mama wengi nchini. Nimeitaka Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii kuweka utaratibu mzuri ili msaada huo utumike
ipasavyo na kuwanufaisha walengwa.
Ziara ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Nchini
Ndugu Wananchi;
Tarehe 23 mwezi Julai, 2013 pia tulitembelewa na Waziri Mkuu Mstaafu wa
Uingereza, Mheshimiwa Tony Blair. Katika mazungumzo yetu Mheshimiwa
Blair aliahidi kuisaidia nchi yetu kupitia taasisi yake ya Africa
Governance Initiative kusaidia kusambaza umeme wa jua katika shule zetu
za sekondari vijijini, maboresho ya shirika letu la umeme (TANESCO) na
kusaidia uanzishaji na uimarishaji wa Kitengo cha Rais cha Ufuatiliaji
Utekelezaji wa Programu za Maendeleo (Presidential Delivery Bureau -
PDB). Tunamshukuru kwa ahadi yake hiyo itakayochangia katika jitihada za
kujiletea maendeleo.
Ziara ya Waziri Mkuu wa Thailand Nchini
Ndugu Wananchi;
Tarehe 30 Julai, 2013 tulimpokea Mheshimiwa Yingluck Shinawatra, Waziri
Mkuu wa Thailand aliyefanya ziara ya siku tatu nchini. Lengo la ziara
yake ni kuimarisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Thailand na Tanzania.
Katika ziara hiyo, tumezindua Jukwaa la Wafanyabiashara wa Thailand na
Tanzania (Thai-Tanzania Business Forum) ili kukuza biashara na uwekezaji
baina ya nchi zetu. Waziri Mkuu Yingluck Shinawatra alitumia fursa hiyo
kufafanua sera ya Thailand kwa Afrika inayosisitiza kukuza ushirikiano
wa karibu wa kiuchumi na kibiashara. Pia amepata nafasi ya kutembelea
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kujionea mwenyewe jinsi nchi yetu
ilivyobarikiwa kwa kuwa na kivutio hicho cha aina yake. Alipokuwa kule
nchi zetu zilitiliana saini maelewano ya ushirikiano katika kulinda na
kuhifadhi wanyama pori.
Katika
mazungumzo yangu na yeye, tumekubaliana kuchukua hatua thabiti kukuza
ushirikiano katika nyanja mbalimbali. Tumetiliana saini mikataba mitano
ya ushirikiano kwa mambo yafuatayo: Kukuza na kulinda vitega uchumi;
kubadilishana wafungwa; ushirikiano wa kiufundi; na ushirikiano kwa
masuala ya madini. Aidha, Waziri Mkuu huyo ameahidi kuwahimiza
wawekezaji wa nchini mwake kuja Tanzania kuwekeza katika sekta
mbalimbali za uchumi ikiwemo kilimo, utalii, viwanda nakadhalika. Pia,
Waziri Mkuu wa Thailand ameahidi kuwa Serikali yake itatoa ufadhili kwa
vijana 10 kusoma Shahada ya Uzamili nchini humo. Vile vile, nchi hiyo
itaanza kuleta wataalamu wa afya wa kujitolea kuja kushirikiana na
wataalam wetu kuimarisha huduma ya afya nchini.
Ziara
hizi zinaonesha utayari wa dunia kuunga mkono jitihada zetu za kujiletea
maendeleo. Naomba Watanzania wenzangu tutumie vizuri utayari huo wa
dunia kuongeza kasi ya maendeleo yetu. Tusijikwaze wenyewe.
Ziara ya Kagera
Ndugu wananchi;
Kuanzia tarehe 24 hadi 29 Julai, 2013, nilifanya ziara Mkoani Kagera.
Nilishiriki kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa na kuzindua jengo
jipya la Mahakama Kuu. Pia niliweka jiwe la msingi la upanuzi wa kiwanja
cha ndege cha Bukoba na kuweka mawe ya msingi ya ujenzi wa kiwango cha
lami kwa barabara za Kigoma – Lusahunga na Kyaka – Kayanga – Bugene.
Vile vile nilizindua Wilaya mpya ya Kyerwa na kukagua shughuli za
maendeleo pamoja na kuona na kusikiliza changamoto mbalimbali
zinazowakabili wananchi ili kuzitafutia majawabu.
Sherehe
za Kumbukumbu ya Mashujaa zilifana sana. Niliwapongeza viongozi wa Jeshi
na wa Mkoa kwa maandalizi mazuri ya sherehe hizo. Pia nilirudia
kumpongeza Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange, kwa uamuzi wake
wa busara wa kufanya sherehe za kumbukumbu za mashujaa wetu pale Kaboya
badala ya kufanyikia Dar es Salaam tu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Ni
uamuzi muafaka na wa busara kwani pale Kaboya ndipo walipolala mashujaa
wetu waliopoteza maisha yao kutetea mipaka na uhuru wa nchi yetu dhidi
ya Nduli Iddi Amin. Hali kadhalika, kule Naliendele, Mtwara ambapo
sherehe za mashujaa zilifanyika mwaka wa juzi, ndipo walipozikwa
mashujaa wetu waliopoteza maisha kuisaidia nchi jirani na rafiki ya
Msumbuji kutetea Uhuru wake dhidi ya wakoloni, makaburu na vibaraka wao
wa ndani ya Msumbiji.
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu pale Kaboya niliwakumbusha Watanzania wenzangu
kwamba katika kuwakumbuka mashujaa wetu wale na sisi tulio hai, hatuna
budi kutambua wajibu wetu wa kuwa tayari kujitolea muhanga kwa ajili ya
kulinda uhuru wa mipaka ya nchi yetu. Nilisisitiza utayari wa nchi yetu
kulinda mipaka yake na kwamba mfano wa mashujaa waliolala pale ni
fundisho kwa mtu ye yote anayetamani kumega kipande cho chote cha ardhi
ya nchi yetu. Atakiona cha mtema kuni kilichomkuta Nduli Iddi Amini au
hata zaidi.
Nimesikia
kuwa kauli yangu ile imetafsiriwa visivyo na kupotoshwa na baadhi
vyombo vya habari na hata majirani zetu. Tafsiri hizo ni potofu.
Sikumtaja mtu ye yote au nchi yo yote. Nilikuwa nazungumzia wajibu wa
majeshi yetu na raia wa nchi yetu wa kulinda uhuru na mipaka yetu na
kwamba hatutamruhusu mtu au nchi yo yote kutupokonya wala kuichezea haki
yetu hiyo ya msingi. Tuko tayari kuitetea hata kama gharama yake ni
maisha yetu kama walivyofanya mashujaa waliolala Kaboya.
Mahakama Kuu
Ndugu Wananchi;
Katika ufunguzi wa Mahakama Kuu ya Bukoba nilisisitiza dhamira na
utayari wa Serikali yetu kuiwezesha Mahakama ya Tanzania kuwa na
Mahakama Kuu katika kila Mkoa. Baada ya kukamilika kwa Mahakama Kuu ya
Bukoba bado kuna Mikoa 14 hainazo. Katika bajeti ya mwaka wa fedha
2013/14 tumetenga fedha za kujenga Mahakama Kuu katika Mikoa 7 na
nilirudia ahadi yangu kuwa katika mwaka ujao wa fedha tutatoa fedha za
kumalizia Mikoa 7 iliyosalia. Niliamua tuongeze kasi ya kujenga Mahakama
Kuu hizo ili kuiwezesha Mahakama ya Tanzania kutimiza ipasavyo wajibu
wake wa kutoa haki nchini.
Maendeleo ya Mkoa wa Kagera
Ndugu Wananchi;
Nilipokuwa Kagera nilifurahishwa na utekelezaji wa shughuli mbalimbali
za maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Taarifa za Mkoa na Wilaya
zimefafanua kwa kina mambo mazuri yaliyofanyika na yanayoendelea
kufanyika Mkoani. Wameelezea furaha yao kwa mafanikio yaliyopatikana
ambayo baadhi nimeyashuhudia au hata kushiriki kuyazindua na kuweka mawe
ya msingi. Taarifa hizo pia zimelezea mambo mengi zaidi wanayotaka
yafanyike na matatizo mapya na hata ya zamani ambayo wanataka yapatiwe
ufumbuzi.
Katika
mazungumzo yangu na viongozi na wananchi, yapo mambo ambayo yako kwenye
uwezo wao kijijini, Wilayani na Mkoani kuyapatia ufumbuzi. Tulikubaliana
na kuelekezana nini kifanyike. Yapo mengine mengine ambayo yanahitaji
nguvu ya taifa tumeyachukua kuja kuyafanyia kazi. Kuna baadhi yaliwahusu
Mawaziri ambao nilikuwa nao ziarani waliyasemea na kuyafanyia kazi
palepale yalipojitokeza.
Ulinzi na Usalama
Ndugu Wananchi;
Kuna mambo matatu yahusuyo usalama ambayo yalizungumzwa na wananchi kwa
uchungu mkubwa ambayo niliamua tuyashughulikie kitaifa. Mambo hayo ni
ujambazi wa kutumia silaha kuteka magari, kupora mali na watu kuuawa.
Jambo la pili ni wahamiaji kutoka nchi jirani wanaoingia, kuishi na
kufanya shughuli nchini kinyume cha sheria. Na tatu, mifugo kuingizwa
kwa wingi nchini bila kufuata taratibu husika na mingine kuingizwa
katika hifadhi za wanyama.
Ndugu wananchi;
Nilitoa maagizo kwa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama yaani JWTZ,
Polisi, Usalama wa Taifa na Uhamiaji watengeneze mpango kabambe wa
kuyashughulikia matatizo hayo. Watayarishe na kutekeleza operesheni
maalum itakayo au zitakazokomesha ujambazi, kuondoa wahamiaji wasiokuwa
halali na kuondoa mifugo iliyoingizwa nchini kinyume na utaratibu na ile
iliyoko kwenye maeneo yasiyo stahili.
Aidha,
niliwataka majambazi wajisalimishe na wasalimishe silaha zao ndani ya
wiki mbili na siku hizo zinaanzia tarehe 29 Julai, 2013 nilipomaliza
ziara yangu Mkoani humo. Kwa wahamiaji wanaoishi nchini kinyume cha
sheria nimewataka watumie muda huo kuondoka nchini au kuhalalisha ukaazi
wao. Hivyo hivyo kwa mifugo iliyoingizwa nchini kinyume na sheria au
ile iliyoko kwenye maeneo yasiyostahili. Ndani ya muda huo watu wote
waondoe mifugo yao au wajitokeze kufuata taratibu zilizopo.
Ndugu Wananchi;
Nilisema nilipokuwa Mkoani Kagera na narudia tena leo kuwa baada ya siku
14 kupita, vyombo vya ulinzi na usalama vitaendesha operesheni maalum
ya kushughulikia matatizo hayo. Nilisema kuwa operesheni hiyo itafanyika
katika Mikoa ya Kigoma, Kagera na Geita kwa wakati mmoja. Napenda
kuwahakikishia kuwa hapatakuwa na mahali pa kukimbilia wala kujificha.
Nawashauri wale wote wanaohusika na ujambazi, uhamiaji haramu na
uingizaji haramu wa mifugo waamue kuchukua hatua muafaka sasa.
Wasisubiri operesheni iwakute, wala wasifikirie kuwa hili ni jambo la
kupita. Safari hii itakuwa endelevu.
Ndugu Zangu;
Hatuwezi kukubali hali hii niliyoikuta Mkoani Kagera ikaachwa kuendelea.
Italeta madhara makubwa zaidi siku za usoni. Haiwezekani raia katika
nchi yake, akose uhuru na usalama wa kutembea peke yake mpaka
asindikizwe na Polisi. Na, baya zaidi hata Polisi nao wanashambuliwa na
kuuawa watakavyo majambazi. Uhalifu huu lazima ukomeshwe, uishe na
usijirudie tena.
Pia,
haiwezekani hali ya watu kutoka nchi jirani kuingia nchini, kuishi na
kufanya shughuli na kutoka watakavyo. Hatuzuii watu kuingia na kuishi
Tanzania lakini wafuate sheria na taratibu za kuhamia na kuishi katika
nchi yetu. Nchi yetu ina sifa na ukarimu huo. Hakuna uthibitisho mkubwa
zaidi ya ule wa mwaka 1982, Rais Julius Nyerere wakati ule alipowaruhusu
wakimbizi wanaopenda kuwa raia wa Tanzania wafanye hivyo. Wakimbizi
30,000 tu waliitumia fursa hiyo. Mwaka 2010 tuliwapa uraia wakimbizi
160,000 wa kutoka Burundi. Kwa sababu hiyo hatuoni sababu ya watu
kufanya wanayoyafanya sasa kule Mkoani Kagera. Hatuwezi kuacha hali hiyo
iendelee ilivyo.
Ndugu Wananchi;
Nilipokuwa Mkoani Kagera nilielezea kusikitishwa kwangu na vitendo vya
baadhi ya watendaji na viongozi wa vijiji na wananchi kuwaruhusu watu
kuingia na kuishi nchini kinyume cha sheria. Nimewataka waache mtindo
huo. Nimeagiza na wao wajumuishwe katika operesheni ijayo.
Watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo haramu wachukuliwe hatua
zipasazo kisheria. Aidha, niliwataka Maafisa wa Uhamiaji watimize
ipasavyo wajibu wao. Ukweli ni kwamba, mambo haya kuendelea kwa muda
mrefu kiasi hiki ni kwa sababu ya udhaifu wa mamlaka husika. Vile vile,
nimewataka TAKUKURU nao watimize wajibu wao. Hapa kuna uthibitisho tosha
wa kuwepo kwa vitendo vya rushwa vinavyohusisha wahamiaji hao na
maofisa wa vijiji na idara husika za Serikali. Mimi naamini kama
TAKUKURU ikiwabana na Uhamiaji wakichemka vya kutosha tatizo hili
lingepungua sana au hata kutokuwepo kabisa.
Uhusiano na Nchi ya Rwanda
Ndugu wananchi;
Katika kipindi cha miezi miwili sasa hususan tangu mwishoni mwa mwezi
Mei, 2013, uhusiano baina ya nchi yetu na Rwanda unapitia katika wakati
mgumu. Kauli za viongozi wa Rwanda dhidi yangu na nchi yetu ni ushahidi
wa kuwepo hali hiyo. Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu na ndugu
zetu wa Rwanda kuwa mimi, Serikali ninayoiongoza na wananchi wa
Tanzania tunapenda kuwa na uhusiano mzuri na ushirikiano wa karibu na
Rwanda kama ilivyo kwa nchi zote jirani. Kama majirani kila mmoja
anamuhitaji mwenzake, hivyo lazima tuwe na uhusiano mwema na ushirikiano
mzuri.
Napenda
kusisitiza kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza tutakuwa wa mwisho
kufanya kitendo au vitendo vibaya dhidi ya Rwanda au nchi yo yote jirani
au yo yote duniani. Hatuna sababu ya kufanya hivyo kwani ni mambo
ambayo hayana tija wala maslahi kwetu.
Ndugu Wananchi;
Ukweli ni kwamba wakati wote tumekuwa tunajihusisha na mambo ya kukuza
na kujenga ujirani mwema na kufanya mambo ambayo yatasaidia kuimarisha
uhusiano wetu kwa maslahi ya nchi zetu. Hiyo ni moja ya nguzo kuu ya
Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania. Huo ndiyo ukweli kuhusu uhusiano wetu
na nchi ya Rwanda kabla na hata baada ya sintofahamu iliyojitokeza sasa.
Napenda kuwahakikishia ndugu zetu wa Rwanda kuwa kwa upande wetu hakuna
kilichobadilika wala kupungua katika uhusiano na ushirikiano wetu.
Mambo yapo vile vile. Kwa upande wangu, binafsi, sijasema lo lote kuhusu
Rwanda pamoja na maneno mengi ya matusi na kejeli yanayotoka kwenye
vinywa vya viongozi wa Rwanda dhidi yangu. Siyo kwamba siambiwi
yanayosemwa au sijui kusema au sina la kusema, la hasha. Sijafanya hivyo
kwa sababu sioni faida yake. Kwangu mimi sioni kama kuna mgogoro wa
aina yo yote. Busara inatuelekeza kuwa tusikuze mgogoro usiokuwepo.
Waingereza wanasema “two wrongs do not make a right”.
Ndugu Wananchi;
Kama mjuavyo uhusiano wetu na Rwanda umekuwa mzuri kwa miaka mingi.
Tunashirikiana na kusaidiana kwa mambo mengi baina ya nchi zetu kitaifa
na katika kanda yetu ya Afrika Mashariki na Nchi za Maziwa Makuu, katika
Umoja wa Afrika na hata kimataifa. Uhusiano unaelekea kupata mtikisiko
baada ya mimi kutoa ushauri kwa Serikali ya Rwanda kuzungumza na
mahasimu wao. Ushauri ule niliutoa kwa nia njema kabisa kwani bado
naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo njia
hiyo ni vyema itumike. Isitoshe, ushauri ule niliutoa pia kwa Serikali
ya Kongo na kwa Serikali ya Uganda. Katika mkutano ule Rais Yoweri
Museveni wa Uganda aliunga mkono kauli yangu. Rais wa Rwanda hakusema
cho chote pale mkutanoni. Baada ya kurudi nyumbani ndipo tukaanza
kuyasikia maneno tuliyoyasikia na tunayoendelea kuyasikia.
Kwa kweli
nimestaajabu sana na jinsi walivyouchukulia ushauri wangu na
wanayoyafanya. Havifanani kabisa, completely out of proportion and out
of context. Mimi nilifanya vile kwa kuzingatia mila na desturi zetu za
miaka mingi katika ukanda wetu. Tumekuwa tunakutana katika mikutano na
vikao mbalimbali tunazungumza na kushauriana kwa uwazi juu ya njia za
kushughulikia matatizo na masuala mbalimbali kila yanapotokea. Wakati
wote tumeyachukulia kuwa ni mambo yanayotuhusu sote hivyo kupeana
ushauri ni wajibu wetu wote. Na mara nyingi ushauri kwa wanaogombana
kuzungumza tunautumia sana. Iweje leo mtu kutoa ushauri ule lionekane
jambo baya na la ajabu. Jambo la kushutumiwa na kutukanwa! Siyo sawa
hata kidogo!! Ushauri si shuruti, ushauri si amri. Una hiyari ya
kuukubali au kuukataa. Muungwana hujibu: “Siuafiki ushauri wako”. Hakuna
haja ya kutukana wala kusema maneno yasiyostahili wala kusema
yasiyokuwepo na ya uongo.
Ndugu Wananchi;
Napenda kurudia kusema kuwa mimi binafsi na Serikali yetu ya Tanzania
hatuna ugomvi wala nia yo yote mbaya na Rwanda. Tunapenda tuendelee kuwa
na uhusiano mzuri na Rwanda. Labda wenzetu wanalo lao jambo dhidi yetu
ambalo sisi hatulijui. Maana na sisi tunasikia mengi yanayozungumzwa na
kudaiwa kupangwa kufanywa na Rwanda dhidi yangu na nchi yetu. Hatupendi
kuyaamini moja kwa moja tunayoyasikia lakini hatuyapuuzi.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza, naomba kutumia nafasi hii pia kuwatakia Waislamu wote
nchini heri na baraka tele katika kukamilisha ibada muhimu ya kufunga
mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Naomba tuendelee kuwatakia heri ili wamalize
salama na tuweze kusherehekea kwa furaha na bashasha tele siku kuu ya
Idd el Fitr pindi itakapowadia.
Mwisho
kabisa, nawaomba Watanzania wenzangu wote tuendelee kushirikiana na
kuishi kwa upendo, umoja na mshikamano kama ilivyo kawaida yetu.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Asanteni Sana Kwa Kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment