facebook likes

Saturday, July 27, 2013

Ukatili gani huu-Mama abanika mikono ya mwanae motoni


Mtoto Bryton Evarist (9) mkazi wa Temeke, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, amejeruhiwa vibaya baada ya kuunguzwa mikono kwa kubanikwa kwenye jiko la mkaa na mama yake mzazi.
Mwanamke aliyefanya unyama huo ni Asa Barnaba (24), ambapo inadaiwa baada ya tukio hilo alimfungia ndani kwa muda wa wiki mmoja na kumlazimisha kula na kuoga kwa kutumia mikono aliyomuunguza.
Tukio hilo linadaiwa kufanywa wiki tatu zilizopita majira ya usiku, baada ya mtoto huyo kudaiwa kula samaki wa kitoweo.
Akisimulia mkasa huo akiwa Hopitali ya Temeke, mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu Shule ya Msingi Kibasila, alisema mama yake alichukua hatua hiyo baada ya kukasirishwa na kitendo hicho.Kusoma zaidi bofya
Alisema siku ya tukio, alirudi nyumbani mapema akitokea shuleni, alipofika nyumbani kwao alikuta chakula pamoja na mboga mbili aina ya maharage na samaki.
Bila ya kutambua kwamba samaki hao waliwekwa kwa ajili ya kitoweo cha usiku, aliamua kula na kuyaacha maharage.
“Mama aliporudi na kukuta nimekula samaki, aliniuliza kwa nini nimekula, lakini nilikataa kwa kuogopa kupigwa,” alisema.
Hata hivyo, baada ya kubanwa sana, mtoto huyo aliamua kukubali kula ndipo mama yake alipochukua jiko la mkaa lenye moto na kumuweka mikono yake juu ya moto uliokuwa unawaka.
“Alichukua mikono yangu na kuniweka kwenye jiko, nilihisi maumivu makali sana,” alisema.


SIRI YABAINIKA
Akiongea na NIPASHE Jumamosi, Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Temeke, Sharifa Ally, alisema mtoto huyo aligundulika kufanyiwa unyama huo baada ya wiki moja akiwa katika hali mbaya.
Alisema aligundulika baada ya kutoroka na kwenda kuomba msaada kwa wapita njia ili wamsaidie kumpeleka hospitali.

“Inashangaza sana kuona mama mzazi akiwa na moyo wa kikatili, muda wote alikuwa akienda kazini na kumuacha mtoto wake ndani akioza mikono,” alisema Sharifa.
Sharifa, alisema hatua hiyo ilisaidia mtoto huyo kupelekwa kituo cha Polisi cha Chang’ombe na kisha kufikishwa Hospitali ya Temeke.
“Akiwa hospitalini, sisi Ustawi wa Jamii na Jeshi la Polisi tulisimamia kwa karibu matibabu yake pamoja kuangalia namna na kumfungulia kesi mhusika,” alisema.

MAMA AKIRI
Mama wa mtoto huyo alipoulizwa sababu ya kufanya kitendo hicho, alisema aliamua kumchoma moto mtoto wake baada ya kuchoshwa na tabia yake ya wizi kwa muda mrefu.
“Huyu mtoto ana tabia ya wizi, mwanzo alikuwa akiniibia hela ndani, nilimuonya sana na wakati mwingine nilimpiga lakini hakusikia, ndipo alipokula mboga niliamua kumchoma moto ili asirudie,” alisema Asa.
Hata hivyo, alisema anajutia kufanya tukio hilo na hakufikiria kwamba mtoto wake angepata majeraha kama aliyonayo kwa sasa.
Baba wa mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Evarist akiongea kwa simu kutoka mkoani Kigoma, alisema bado hajapata taarifa ya tukio hilo na alionyesha kusikitishwa kwake.
“Aisee! sijapata kabisa taarifa ya jambo hilo, nasikitika sana,” alisema na kukata simu.
Alipotafutwa Kamanda wa Mkoa wa Polisi wa Temeke, Engelbert Kiondo kwa njia ya simu, hakupatikana baada ya mtu aliyepokea kueleza yupo nje kikazi.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

COMMENTS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...