facebook likes

Saturday, July 27, 2013

NAENDA : Fabregas ataka kutua Man United


  BARCELONA,HISPANIA
CESC Fabregas amenong’ona kwa rafiki zake. Amewaambia “Ninataka kucheza Manchester United, nataka kuungana tena na Robin Van Persie”.
Jina la kiungo huyo limekuwa likitamba katika vyombo vya habari nchini England na Hispania huku Manchester United ikikataliwa dau la Pauni 30 milioni kwa ajili ya kumpeleka Old Trafford.
Kocha wa United, David Moyes, aliwaambia waandishi wa habari juzi Alhamisi nchini Japan akisema mazungumzo ya kumchukua staa huyo wa zamani wa Arsenal, yanaendelea na hayajafa kama inavyofikiriwa.
Ukweli ni kwamba Fabregas amewaambia rafiki zake kuwa anataka kwenda England huku akiachana na Barcelona kwa mara nyingine tena baada ya kuachana nayo utotoni alipotimkia Arsenal.
Inasemekana Fabregas amefurahishwa na ahadi aliyopewa na Manchester United ya kucheza katika kikosi cha kwanza huku pia akifurahia kuungana tena na rafiki yake, Robin Van Persie.
Katika kikosi cha sasa cha Barcelona, Fabregas, hana uhakika wa namba ya kudumu. Ujio wa staa wa Brazil, Neymar, katika kikosi chao unaweza kumaliza kabisa matumaini yake ya  kupata nafasi kikosi hapo.
Fabregas pia anaamini kuwa anaweza kutwaa taji la Ligi Kuu England akiwa na United kama vile alivyotwaa taji la Ligi Kuu  Hispania msimu uliopita. Staa huyo alitwaa Kombe la FA na Ngao ya Jamii tu katika kipindi chote alichocheza Arsenal.
Barcelona bado imesisitiza kwamba staa huyo wa timu ya taifa ya Hispania hauzwi ingawa inaeleweka kwamba hatima yake itaamuliwa na kocha mpya, Gerrard ‘Tata’ Martino, aliyetua klabuni hapo mapema wiki hii akitokea Argentina.
Arsenal ingekuwa katika nafasi nzuri ya kumsajili staa huyo kutokana na kipengele cha mauzo yake kwenda Barcelona kuwapa fursa ya kuweza kumsajili kwa kiasi cha Pauni 25 milioni.
Lakini haionekani kama kocha, Arsene Wenger, ana hamu ya kumsajili staa huyo kutokana na utajiri alionao katika sehemu ya kiungo ambapo Jack Wilshere na Santi Cazorla wameikamata vema.

No comments:

COMMENTS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...