facebook likes

Saturday, July 27, 2013

MKULIMA AUWA WANAWE WAWILI HUKO KIGOMA.....BANGI YATAJWA KUWA CHANZO...!!

JESHI la Polisi mkoani Kigoma linamshikilia mkulima mkazi wa kijiji cha Mvugwe, Kasulu, Thobias Majuto kwa kuua watoto wawili kwa makusudi. Akizungumza na gazeti hili mjini hapa juzi Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Fraiser Kashai alisema mkulima huyo inadaiwa alifanya mauaji hayo Jumatano saa mbili asubuhi nyumbani kwake

Akieleza tukio hilo, Kamanda Kashai alisema mtuhumiwa alimchukua mtoto wake mkubwa, Loyce Majuto (2) na kumchoma kisu kifuani na kukishindilia hadi alipokata roho. Kama vile haitoshi alimchukua mtoto mwingine mwenye umri wa miezi mitatu ambaye hakuwa amepewa jina na kumbamiza chini mara tatu hadi kufa.

Wakati akifanya vitendo hivyo mkewe alikuwa nje akipika na baada ya kusikia vilio alikimbilia ndani kujua kulikoni, ndipo akakuta mtuhumiwa amefanya unyama huo wa kutisha. Kutokana na mauaji hayo mwanamke alipiga yowe na umati wa watu kijijini hapo kujitokeza na kumkamata mtuhumiwa na kumpiga na baadaye kumfikisha Polisi Makere.

Kamanda alisema sababu kuu ya vitendo hivyo ni matumizi ya dawa za kulevya aina ya bangi kwa muda mrefu na hivi sasa anashikiliwa Polisi wilaya ya Kasulu wakati upelelezi wa shauri hilo ukiendelea.

Mauaji Sumbawanga, Habari kutoka Sumbawanga, zinasema Polisi inashikilia wanandoa kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mtoto wao wa kike mwenye umri wa miaka miwili wakati wanapigana kwa kilichoelezwa ni wivu wa kimapenzi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda jana akizungumzia tukio hilo alisema lililotokea saa 5:30 usiku wa kuamkia Julai 22, baada ya wanandoa hao Livinus Choma (31) na Grace Choma (28), wakazi wa Malangali mjini hapa, kurejea nyumbani wakiwa wamelewa.

Alisema baada ya kurejea nyumbani wakitoka katika kilabu cha pombe za kienyeji, ulizuka ugomvi kutokana na mke kumtuhumu mumewe kuwa na uhusiano kimapenzi na wanawake wengine hali iliyomkera mume na kupigana.

Ilielezwa kuwa wakiwa wanapigana, mume alimsukuma mkewe, akamwangukia mtoto wao huyo aitwaye Esther na kupoteza fahamu, hali iliyochanganya wazazi wakiamini amekufa.

Kwa mujibu wa Kamanda Mwaruanda, wanandoa hao walimchukua mtoto huyo katika hali hiyo na kwenda kumtelekeza katika nyumba jirani wakiamini amekufa, kisha wakapiga simu kwa Diwani wa Kata hiyo wakidai kuwa mtoto wao amepotea katika mazingira ya kutatanisha.

Diwani Anthony Choma wa Kata ya Malangali, aliuarifu uongozi wa Serikali ya Mtaa na kwa pamoja walishirikiana na wazazi hao kumtafuta mtoto huyo na kumkuta hana fahamu pembeni mwa nyumba ya jirani yao.

Kwa mujibu wa Diwani Choma, ili kunusuru maisha ya mtoto huyo, walimkimbiza katika hospitali ya mkoa mjini hapa, lakini alifariki dunia muda mfupi baada ya kuanza matibabu. Kamanda Mwaruanda alisema mama wa mtoto huyo alipohojiwa Polisi, alikiri wao kuwa chanzo cha kifo hicho.

Pia alikiri kumtelekeza karibu na nyumba ya jirani ili isijulikane kuwa wao ni wahusika, na kutaka ijulikane kuwa jirani yao ndiye aliyemwiba na kumwua.

Alisema baada ya uchunguzi wa awali kukamilika, wanandoa hao watafikishwa mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Imeandikwa na Fadhil Abdallah, Kigoma na Peti Siyame, Sumbawanga.

SOURCE: HABARI LEO

No comments:

COMMENTS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...