NGULI wa sanaa za maigizo na uchekeshaji nchini, Amri Athumani,
maarufu kama ‘King Majuto’, amemwomba Rais Jakaya Kikwete amsaidie
trekta ili ajikite zaidi kwenye kilimo cha kisasa mkoani Tanga.
Mzee Majuto alimwomba Rais Kikwete trekta hilo juzi alipohojiwa kwenye
kipindi cha ‘Mkasi’ kinachorushwa na kituo cha runinga cha EATV, na
kuongeza kuwa, anamiliki ekari 10 za shamba ambazo hawezi kulima kwa
jembe kutokana na umri wake.
“Najua Rais Kikwete anawajali wasanii na sasa ananisikiliza, naamini
atanisaidia, namwomba Rais Kikwete anisaidie kupata trekta ili nami
nilime kisasa, bei ya trekta moja ni sh milioni 25, mimi uwezo huo kwa
kweli sina… shamba langu lina ekari 10, umri wangu huu kulima kwa jembe
mabega yatashuka.
“Nataka kuwekeza kwenye kilimo cha kisasa kule kwetu, hata mtu
akinitaka nifanye filamu yake lazima anifuate kijijini, anikute na kazi
yangu, najua hata malipo yatakuwa mazuri,” alisema.
Awali mwigizaji huyo alieleza masikitiko yake kwa serikali kushindwa
kuendeleza viwanda, mashamba, bandari na reli vilivyokuwapo awali mkoani
Tanga.
Kadhalika, Mzee Majuto ameishukuru serikali kwa kukubali kutambua kazi
za wasanii na kuziweka stika za Mamlaka ya Mapato (TRA), huku
akisisitiza umoja na mshikamano miongoni mwao.
|
No comments:
Post a Comment