KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
ametamba kuwa hawezi kuruhusu wala kumwonea aibu askari yeyote ambaye
atabainika kuhusika katika sakata la wizi wa sh milioni 150 zilizopotea
mikononi mwa askari waliokuwa wakizima tukio la ujambazi eneo la
Kariakoo jijini Dar es Salaam Desemba 14 mwaka jana.
Kova alitoa kauli hiyo jana ikiwa ni siku moja baada ya Tanzania Daima
kuripoti uwepo wa mkorogano ndani ya jeshi hilo katika sakata zima la
kuwachukulia hatua watuhumiwa.
Akizungumza kwa simu, Kova alisema kuwa yako mambo mawili yanafanyika
kwa wakati mmoja sasa katika kutafuta ukweli wa tukio zima.
Alifafanua kuwa baada ya upelelezi kukamilika, jalada la tuhuma
limepelekwa kwa wakili wa serikali wa kanda hiyo ili kupitia na
kujiridhisha kama watuhumiwa walihusika ama la.
Kamanda Kova alisema kuwa walichelewa kidogo katika hatua ya upelelezi
kutokana na baadhi ya mashahidi akiwemo mwenye mali aliyeibiwa kuwa nje
ya nchi.
“Mwenye mali kwa bahati mbaya aliondoka kwenda nje ya nchi baada ya
tukio lile, hivyo tukachelewa kidogo wakati wa upelelezi, lakini tayari
amerudi na tumemhoji, hivyo mwanasheria akikamilisha kazi yake
watakaobainika watatajwa na kufikishwa kwenye mkono wa sheria,” alisema.
Kova aliongeza kuwa wakati hatua hiyo ikiendelea, vile vile taratibu
za kijeshi nazo zinaendelea kwa kuwafungulia mashtaka watuhumiwa hao
watano ili nao wajitetee kisha watakaobainika watavuliwa uaskari na
kushtakiwa katika mahakama za kiraia.
Kwa kujiamini, Kova aliapa kuwa hakuna usiri wowote katika sakata hilo
na kwamba yeye kama kamanda hawezi kuruhusu wala kumonea aibu askari
anayevunja sheria za kijeshi.
Ni hivi karibuni Kamanda Kova alidai kuwa jeshi hilo linawashikilia
askari watano wote wakiwa wanaume ambao wanatuhumiwa katika ukwapuaji wa
fuko hilo la fedha walizotakiwa kuziokoa kwa majambazi.
Alisema dalili za awali zinaonesha kuwepo kwa hali ya ushiriki wa
askari watano katika upotevu wa fedha hizo na kwamba askari hao
wanashikiliwa huku uchunguzi zaidi ukifanyika.
Aliongeza kuwa askari wanaoshikiliwa ni stafu sajenti mmoja na wengine wanne ni makoplo.
|
No comments:
Post a Comment