José Mourinho aliona ni kitu gani kingetokea kwa timu
yake ya Real Madrid kabla ya mechi yao ya ugenini dhidi ya Granada. Na hicho
ndicho kilichomfanya atumie dakika kadhaa kwenye vyumba vya kuvalia kabla ya
kuchezwa kwa mechi hiyo waliyolala 1-0, akiwakumbusha wachezaji wake kuwa kadri
wanavyocheza vizuri katika La Liga, Ligi Kuu ya Hispania ndivyto wanavyojiwekea
mazingira mazuri ya kufanya vyema katika mechi yao ijayo ya Ligi ya Klabu Bingwa
Ulaya dhidi ya Manchester United na pia ya marudiano kwenye Kombe la Mfalme dhidi
ya Barçelona.
"Mnapaswa kuzingatia fahari ya weledi wenu kwa
kucheza katika kiwango chenu cha juu katika kila mechi. Mnapaswa kujituma sana
na siyo kubweteka, tena katika kila michuano."
Huo ndiyo ujumbe alioutoa Mourinho kwa wachezaji wake bila
kupindisha maneno, muda mfupi kabla ya mechi yao dhidi ya Granada.
"Kuwa wa pili ni bora kuliko kushika nafasi ya tatu,
na kuwa nyuma ya Barca kwa pointi tano au sita ni bora kuliko kuachwa kwa pointi
15 au 16", ulikuwa ni ujumbe mwingine wa kocha huyo Mreno kwa wachezaji
wake.
Kwahiyo, kuhuzunika kwa Mreno huyo kufuatia kichapo
walichopata kutoka kwa Granada kilitokana zaidi na namna timu ilivyocheza na
siyo matokeo.
"Matokeo hayakunisumbua sana, lakini kiwango cha timu
katika kipindi cha kwanza hakikunifurahisha kabisa; kilikuwa cha hovyo. Tulitawala
katika kipindi cha pili na kupata nafasi chache za kufunga na kusawazisha, lakini
hilo peke yake halikutosha kunipa furaha," alisema Mourinho.
Real Madrid watashuka dimbani Jumatano ijayo kucheza
nyumbani mechi yao ya kwanza ya hatua ya 16-bora ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya
dhidi ya Man U na Februari 27 watarudiana na Barcelona katika mechi yao ya ugenini
ya nusu fainali ya Kombe la Mfalme kwenye Uwanja wa Camp Nou. Katika mechi yao
ya kwanza dhidi ya Barca, matokeo yalikuwa sare ya 1-1.
No comments:
Post a Comment