Mamia ya wahamiaji haramu kutoka nchini Rwanda wakiwa na
ng’ombe zaidi 900 wameanza kuondoka nchini kurejea kwao kutokana na
agizo la Rais Jakaya Kikwete kuwataka waondoke Tanzania kabla ya siku
14.....
SOMA ZAIDI..
Aidha, imeelezwa kuwa kumekuwapo ongezeko la askari wa
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mkoani Kagera hasa wilayani Ngara
hali inayozua hofu kwa baadhi ya wananchi, huku ikiongeza msukumo kwa wahamiaji haramu kuondoka.
Akiwa katika ziara mkoani Kagera, Rais Kikwete alitoa agizo la kuwataka
wote waliokuwa wakiishi nchini kinyume cha sheria waondoke mapema jambo
lililotakiwa kuanza kutekelezwa Julai 29 na kukamilika Agosti 10 mwaka
huu.
Alisema kuwa wahamiaji haramu na wale wanaoendesha ama
kuhusika na ujambazi, uhamiaji haramu na uingizaji haramu wa mifugo
waamue kuchukua hatua mwafaka za kuondoka mapema kabla vyombo vya ulinzi
na usalama kuanza operesheni maalumu ya kuwasaka.
Tayari idadi
kubwa ya wafugaji wenye makundi ya ng’ombe imeanza kuondoka kuelekea
eneo la mpakani la Rusumo kutoka ardhi ya Tanzania ikiwa ni utekelezaji
wa agizo hilo la Rais Kikwete.
Akizungumza na Mwananchi
Jumapili kwa njia ya simu, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Costantine Kanyasu
alisema kwamba idadi kubwa ya wafugaji waliokuwa wakiishi kinyume cha
sheria, imeitikia wito wa agizo la Rais na kuanza kuondoka kwa hiyari
yao.
Hata hivyo, alisema kuwa pamoja na idadi kubwa ya
wahamiaji kuanza kuondoka, bado wapo ambao hawajaondoka kutokana na
kudai kuwa na vibali walivyovipata kutoka Ofisi ya Uhamiaji na
kubainisha kwamba vibali hivyo vitakaguliwa kwa umakini wakati wa
operesheni maalumu ili kujua uhalali wake.
“Jambo hili la
wahamiaji haramu lilikuwa kero kubwa, siyo tu kwa Wilaya ya Ngara, bali
mkoa mzima wa Kagera, lakini tunashukuru sasa wameanza kuondoka,
wamebaki hao wenye vibali. Ni lazima vibali hivyo tutavikagua maana vipo
vilivyotolewa kinamna,” alieleza Kanyasu.
Alionya kwamba
jukumu la kuwaondoa kwa nguvu wahamiaji haramu pamoja na wafugaji
linasubiri muda wa mwisho ili kuanza kutekelzwa kama Rais Kikwete
alivyoagiza.
Hofu ya Wanajeshi kuongezeka
Akizungumzia
suala la wanajeshi kudaiwa kuongezeka wilayani Ngara, Kanyasu alisema
kwamba katika wilaya yake kuna kikosi cha dharura kinachokaa katika moja
ya kambi za JWTZ kikikuwa na idadi kubwa ya askari lakini wananchi
hawakuwa na taarifa nacho ila kutokana na sababu za kiusalama.
“Unajua kuna kelele za hapa na pale na haya majibizano yanayotokea baina
ya Rwanda na Tanzania. Haya ni kama yamewastua watu na kudhani kuwa
askari wetu wa Kikosi cha Dharura waliopo hapa Ngara wameletwa maalumu
kutokana na tahadhari,” alisema na kufafanua kuwa askari hao wapo siku
zote kwa ajili ya kulinda mipaka ya Tanzania. Hata hivyo, mkuu huyo wa
wilaya aliwataka wananchi kutulia na kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo.
Rais Kikwete aliagiza operesheni hiyo ya kuwaondoa wahamiaji haramu
ifanyike katika Mikoa ya Kigoma, Kagera na Geita kwa wakati mmoja
ikisimamiwa na vyombo vya ulinzi na usalama yaani JWTZ, Polisi, Usalama
wa Taifa na Uhamiaji akiwaonya wahalifu kuwa hapatakuwa na mahali pa
kukimbilia wala kujificha
No comments:
Post a Comment