facebook likes

Sunday, August 11, 2013

NIZAR NA NIYONZIMA WANG'ANG'ANIA JEZI ZA NGASSA, ARITHI YA OMEGA ALIYETOLEWA KWA MKOPO MBEYA

KABLA ya kuondoka Yanga SC kwenda Azam FC mwaka 2010, Mrisho Khalfan Ngassa alikuwa anavaa jezi namba nane (8)- na baada ya kurejea sasa amelazimika kuhamia katika namba tisa (9).
Ngassa amerejea Yanga SC wakati ambao jezi namba nane anavaa Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima ambaye amegoma kuiachia.
Namba tisa; Mrisho Ngassa sasa anavaa jezi namba 9 Yanga SC
.....SOMA ZAIDI....Akiwa Azam FC alikuwa anavaa jezi namba 16 na aliendelea kuvaa jezi hiyo hata alipohamia Simba SC, ambako mwishoni akawa anavaa namba nane, lakini aliporejea Yanga SC amekuta namba 16 anavaa Nizar Khalfan, ambaye naye amegoma kuiachia. Imekuwa bahati yake Ngassa amechukua jezi namba tisa, ambayo msimu uliopita ilikuwa inavaliwa na Omega Seme aliyetolewa kwa mkopo Prisons ya Mbeya msimu huu. Naye mshambuliaji mpya, Hussein Javu aliyesajiliwa kutoka Mtibwa Sugar, amechukua jezi namba 21, ambayo iliachwa na Didier Kavumbangu tangu mwanzoni mwa mzunguko wa pili katika Ligi Kuu msimu uliopita.
Yanga SC jioni ya leo itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na SC Villa ya Uganda, ambayo jana ilichapwa mabao 4-1 na Simba SC. Huo utakuwa mchezo wa pili kwa Ngassa tangu arejee Yanga SC, baada ya awali kucheza dhidi ya 3Pillars ya Nigeria, Wana Jangwani wakishinda 1-0, bao pekee la Javu. Pamoja na hayo, Ngassa yupo hatarini kutocheza Ligi Kuu msimu ujao, kutokana Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuthibitisha bado ana Mkataba na Simba SC. Katika mchezo wa jana uliokwenda sambamba na sherehe za Simba Day, Ngassa alitambulishwa kama sehemu ya wachezaji wa kikosi cha Wekundu hao wa Msimbazi msimu huu.

Yanga SC baada ya kuingia Mkataba na Ngassa, haijajisumbua kumalizana na klabu yake, Simba SC maana yake hataruhusiwa kucheza msimu ujao- vinginevyo ithibitike kama anavyodai mwenyewe hana Mkataba na Msimbazi. 

No comments:

COMMENTS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...