WATU watatu wamekufa katika matukio
mawili tofauti jijini Dar es Salaam, wakiwemo wawili walioteketea kwa
moto baada ya nyumba kuungua, huku mwingine ambaye ni msichana wa miaka
16 akifa kwa kujinyonga. Kwa mujibu wa Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa
Ilala, Marietha Minangi, aliyejinyonga ni Milika Kusenha.
Alisema binti huyo alikutwa akiwa amejinyonga juzi saa 1:00 asubuhi maeneo ya Vingunguti Mtakuja, wilaya ya Ilala.
Alijinyonga kwa kutumia kitenge na
mtandio alivyoviunganisha na kufunga kwenye kenchi chumbani kwa mwanamke
aliyetajwa kwa jina la Naomi Milimo (24), aliyekuwa anaishi nae. Hata
hivyo sababu za kujinyonga hazijafahamika, maiti imehifadhiwa katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Katika tukio jingine, moto uliozuka
ghafla katika nyumba inayomilikiwa na Ramadhani Kambenga yenye vyumba
vinne, uliteketeza kabisa vyumba hivyo pamoja na kusababisha vifo vya
watu wawili.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke,
Engelbert Kiondo alisema moto huo ulizuka juzi saa 5:00 usiku katika
eneo la Keko Mwanga na vyumba viwili vya mpangaji aitwaye Michael David
(28) pamoja na mali zote, pia kumuunguza mtoto wake aitwaye Johnson
Michael (6) na rafiki yake aliyetajwa kwa jina moja la Abuu
anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 30 na 35.
Kutokana na miundombinu mibovu ya
barabara magari ya zimamoto yalishindwa kufika katika eneo la tukio,
moto huo ulizimwa na wananchi wa eneo hilo kwa kutumia mchanga na maji.
Chanzo cha moto huo inasadikiwa kuwa ni hitilafu ya umeme.
Maiti zimehifadhiwa hospitali ya Temeke,
upelelezi unaendelea. Katika tukio la tatu, moto ulizuka ghafla katika
nyumba ya Komba Dominick (68) mkazi wa Mtoni Mtongani na kuteketeza mali
zenye thamani ya Sh milioni 26.
Kamanda Kiondo alisema tukio la moto huo
lilitokea juzi saa 7:00 mchana Mtoni Mtongani, ambapo uliteketeza ghala
la kuhifadhia makasha matupu mali ya mpangaji Lameck Anania (55).
Pia moto huo ulishika nyumba ya jirani aitwaye Mahamudu Chibango (53) na kuunguza nyaya za umeme pamoja na vyumba viwili.
Moto ulizimwa na kikosi cha zimamoto na
uokoaji cha jiji kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo na chanzo cha
moto huo bado hakijafahamika.
No comments:
Post a Comment