facebook likes

Monday, August 5, 2013

MJOMBA, MVUVI ALIYESOTA NA KUIBUKA MILIONEA KATIKA SANAA.



















Utunzi wa Mashairi, mikogo na staili yake ya mavazi jukwaani inaweza kuwa chanzo cha kumfanya aonekane mfano wa simba dume la Afrika linalong’ara anga za kimataifa kutoka hapa nchini.

Ni baadhi ya sifa zinazombeba msanii Mrisho Mpoto maarufu kama ‘Mjomba’, ambaye kwa asili ni Mngoni kutoka Kijiji cha Namtumbo mkoani Ruvuma.

Mpoto a.k.a Mjomba anaweza kuwa mmoja kati ya wasanii wachache barani Afrika wanaofanya vizuri katika muziki wa asili unaonogeshwa na ghani za mashairi sanjari na ushereheshaji katika kuwasilisha ujumbe jukwaani.

Alitambulika rasmi katika sanaa kupitia kibao chake cha Salamu Zangu na kuzidi kuonyesha zaidi uwezo wake katika sanaa alipotoa nyimbo za Adela, Mjomba, Chocheeni Kuni na nyinginezo, ingawa alianza kujulikana katika mataifa makubwa yakiwemo Uingereza, Marekani, Uholanzi na Ufaransa.

Uwezo wa kazi nzuri unaowavuta na kukonga nyoyo za mashabiki awapo jukwaani ndiyo chanzo cha kumfanya kuwa mmoja kati ya wasanii wachache wanaofanya vizuri nchini.

Hata hivyo, kwa maelezo yake Mjomba anasema kuwa safari ya maisha yake ilikuwa na changamoto nyingi hadi kufikia mafanikio aliyonayo sasa akimtaja kaka yake kuwa mtu wa kwanza kumkatisha tamaa katika safari yake aliyekuwa akiishi Kigoma.

“Mwaka 1995 ‘braza’ aliniita Kigoma akaniambia niachane na sanaa hii, akanitafutia vibarua vya kubeba mizigo pale Bandari ya Kigoma, baada hapo nikabobea na hatimaye nikaingia kwenye ajira ya uvuvi wa samaki,” anasema.

Anaongeza kuwa alifanya kazi hiyo kwa miaka miwili, lakini kabla ya hapo alikuwa akiishi na mama yake jijini Dar es Salaam kuanzia mwanzoni ya miaka ya 1990.

Anadokeza kuwa kipindi hicho alikuwa na hali ngumu akiishi kwa kufanya vibarua ili kupata riziki ya kila siku.

“Mama alikuwa akifanya kibarua cha kubangua dengu na korosho katika Kampuni ya ‘Mohamed Enterprises’, kwa hivyo nilikuwa naongozana naye kila siku,” anasema

Pamoja na kuwepo kwa wasanii wa Bongo Fleva wenye thamani za juu, Mpoto anaweza kuwa mmoja wa wasanii wenye kipato cha juu kutokana na kipato chake anachokipata kwa mwezi kupitia sanaa.

Pia ni mjasiriamali anayemiliki mabasi matatu ya (Daladala) yanayomwezesha kukusanya hadi Sh300,000 kila siku. Upande mwingine katika sanaa amefanikiwa jipenyeza katika soko na kupata mialiko mbalimbali kutoka taasisi, wizara, asasi na mashirika inayomwingizia wastani wa Sh75 milioni kwa mwezi.

“Kwa mwezi napata mialiko isiyopungua 15, kila mwaliko malipo hayapungui Sh5 milioni, hivyo ukipiga hesabu mwenyewe utajua,” Mpoto anaweka wazi.

Hata hivyo, anasema kuwa maonyesho ya hapa nchini hayamlipi kama ilivyo kwa mialiko na maonyesho anayopata na kufanya nje ya nchi.

“Kwa mfano mwaka huu nimekwenda Uingereza, Marekani, Burundi na Kenya. Kwa mialiko ya nje napata posho ya kujikimu Paundi 120 kwa siku na malipo ya wastani wa Paundi 1500 mpaka 3000 kwa kila shoo,” anasema.

Fedha hizo ni sawa na wastani wa Sh288,000 kama posho ya kujikimu na Sh3,600,000 hadi Sh7,200,000.

Alikotokea

Mrisho Mpoto ni moja ya vipaji vilivyoibuliwa na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM).

Anaeleza kuwa yeye aliibuliwa kupitia mfumo wa awali wa chuo kutafuta vipaji mbalimbali vya sanaa kwa ajili ya kuunda kikundi cha sanaa kilichopo chuoni hapo.

“Nilianza kuishi chuoni hapo tangu mwaka 1993, nilikuwa nakula, nalala na kuishi kama mwanafunzi pale huku nikishiriki mafunzo ya sanaa kupitia umoja wa Wanachuo DARUSO,” anasema.

Alifanikiwa kukaa chuoni hapo kwa kipindi cha takriban miaka kumi kabla ya kuwa mmoja wa waanzilishi wa Kikundi cha Parapanda, mnamo mwaka 1994. Hata hivyo hakuweza kufanya shoo zake binafsi tofauti na mialiko ya chuoni kutokana na mwongozo wa Kikundi cha DARUSO.

Anaongeza kuwa kipindi hicho pia alifanikiwa kuishi Ulaya na Marekani kwa miaka kadhaa kutokana na sanaa yake.

“Lakini pia mwaka 2000 mpaka 2002 nilipata nafasi ya kusoma kozi ya mafunzo ya ‘Theatre’ nchini Marekani, nilikuwa situlii hapa Tanzania hadi nilipokuja kutoa nyimbo ya Salamu Zangu,” anasema.

Kuhusu Bongo fleva

Mpoto ambaye ni baba wa watoto wawili na mkazi wa Jiji la Dar es Salaam anasema kuwa muziki wa Bongo Fleva haulipi.

“Wasanii wetu wa Bongo Fleva wanaonekana kama wamezaliwa kwa ajili ya kufanya muziki wa aina hiyo ni muziki usiolipa, nadhani bado hawajatambua eneo lenye mafanikio,” anasema.

No comments:

COMMENTS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...