KABLA YA KODI YA LAINI ZA SIMU KUELEWEKA,SERIKALI YAANZISHA KINYEMELA KODI YA KUHAMISHA FEDHA KUTOKA BENKI...
Wakati mvutano kati ya Serikali na wadau
mbalimbali kuhusu pendekezo la kufutwa kwa tozo ya kodi ya laini za
simu ‘Simcard tax’ ya Sh1,000 ukiwa haujapoa, Chama cha Wenye Mabenki
nchini (TBA) kimeibuka na kuitupia lawama Serikali kwa kuanzisha
kinyemela sheria ya kodi ya kuhamisha fedha kutoka benki.
Taarifa iliyotolewa jana na kusainiwa na Mwenyekiti wa TBA, Dk Charles
Kimei imesema kuwa Serikali kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2013 (The
Financial Act 2013) ilitangaza ongezeko la tozo hiyo ya kodi kwa
asilimia 0.15.
Kutokana na tozo hizo, gharama za kibenki kwa wateja zitaongezeka na
kumlazimisha mteja aliyekuwa anatuma Sh 10 milioni kwa njia ya Mfumo wa
Malipo Makubwa na ya Haraka (TISS) kwa gharama ya Sh10,000, sasa
atalazimika kutumia Sh25,000 kutuma kiwango hicho cha fedha.
Alipoulizwa kwa njia ya simu jana jioni kuhusu tozo hizo Waziri wa
Fedha, Dk William Mgimwa aliomba atafutwe baadaye kwa maelezo kuwa yupo
katika kikao.
Hata hivyo, alipotafutwa tena simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila
majibu.
Tayari Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imethibitisha kupitishwa kwa
sheria hiyo, huku Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka
hiyo, Richard Kayombo akilieleza gazeti hili jana kuwa walitoa barua
kwa TBA tangu Julai 16, kuwataka kuanza utekelezaji wa sheria hiyo.
Sheria hiyo inasema; Kutakuwa na tozo ya kodi kwa fedha zinazohamishwa
kupitia benki, taasisi ya fedha au kampuni ya simu kwa tozo ya asilimia
0.15 kwa kiwango cha fedha kinachozidi shilingi 30,000… Tozo hiyo
haitahusu uhamishaji wa fedha kutoka benki moja kwenda nyingine, taasisi
za fedha, Serikali na shughuli za kibalozi.”
TBA inasema, Serikali imeingiza tozo hiyo kinyemela kwenye sheria na
kwamba haikuwemo kwenye hotuba ya bajeti ya Wizara ya Fedha mwaka
2013/2014 wala kwenye mapendekezo ya muswada wa sheria ya fedha, kwamba
ilitolewa kama mabadiliko kwenye sheria.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa iwapo tozo iliyopendekezwa itatumika kama
ilivyo, kutakuwa madhara makubwa katika mzunguko wa fedha kwa kuwa
asilimia 12 pekee ya watu wote nchini, ndiyo wanaotumia huduma ya benki.
Shirikisho hilo lilifafanua kuwa mabenki yanatumia mfumo wa kuhamisha
fedha kwa njia ya simu ili kupunguza pengo lililopo baina ya watu
wanaotumia benki na wasiotumia huduma hiyo.
“Tozo hilo itaongeza ufisadi na changamoto nyingine za kiuendeshaji kwa
kuwa zitawapa watu nafasi ya kutafuta njia ya kukwepa kodi hiyo mpya”
inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Shirikisho hilo limebainisha kuwa limeshaiandikia barua TRA na Waziri wa
Fedha, kuwataka wakutane kuzungumzia suala hilo na kwamba iwapo
Serikali haitaondoa tozo hiyo wananchi wajiandae kulipa kodi hiyo mpya.
No comments:
Post a Comment