Mshambuliaji aliyetokea kukonga mioyo ya
mashabiki wa Simba kwa kufumania nyavu, Betram Mwombeki amekwaa kisiki
katika usajili wake kuichezea timu hiyo baada ya kuwekewa pingamizi na
klabu yake aliyoichezea msimu uliopita, Pamba ya Mwanza.
Mwenyekiti wa Pamba, Kazimoto Miraj Muzo
aliiambia Mwananchi kuwa Mwombeki alikuwa Marekani miaka ya nyuma na
mwaka jana alijiunga na Pamba wakati wa dirisha dogo la usajili na
kucheza mechi kadhaa tofauti na taarifa kuwa ametokea Marekani.
Muzo alisema kuwa hakuweza kucheza mechi
nyingi kutokana na kukabiliwa na maumivu ya goti. "Si kweli kuwa
ametokea Marekani, tupo hapa na aliichezea timu yetu. Tuliwaambia Simba,
wakabisha na sasa tutakutana mbele ya sheria," alisema Muzo.
Alifafanua kuwa walizungumza na Makamu
Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang'are kuhusiana na usajili wa mchezaji
huyo, lakini hakuonyesha kujali taarifa hiyo.
"Tumewasilisha vielelezo vyetu TFF,
tunasubiri matokeo ya kikao cha Kamati ya Alex Mgongolwa kutoa uamuzi
wake, tumedhamiria kupigania haki yetu mpaka mwisho" alisema.
Alisema kuwa kiasi gani cha fedha
watakachoidai Simba iwalipe ni siri, kwani daima wao huwa hawapendi
kuweka hadharani masuala ya fedha, hasa za kumuuza mchezaji.
Itang'are alipoulizwa kuhusiana na sakata
hilo alithibitisha kuongea na Pamba na kuahidi kulifanyia kazi. "Pamba
ni ndugu zetu, miaka ya nyuma walitupa wachezaji wengi kama Hussein
Marsha, John Makelele, George Masatu, Juma Amir na wengine, na kwa hili
sidhani kama tutashindwana," alisema Itang'are.
Wakati Simba inakabliwa na kikwazo
kuhusiana na Mwombeki, Yanga inaelekea kupeta kwa mchezaji, Mrisho
Ngassa kutokana na ukweli kuwa Simba hajawasilisha taarifa nyingine
zaidi ya mkataba tu.
No comments:
Post a Comment