Kibaha/Tanga. Hata kabla ya maziko askari wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), waliouawa Darfur, Sudan hayajafanyika, mchumba wa mmoja
wa wapiganaji hao, Amina Juma ameonja chungu nyingine baada ya
kutimuliwa kwenye nyumba aliyokuwa akiishi na marehemu mwenza wake.
Amina
ambaye inadaiwa kuwa alikuwa akiishi na Fortunatus Msofe aliyekuwa
askari katika Kambi ya Msangani, 36KJ Pwani alisema jana: “Kumekuwa na
mzozo wa hali ya juu na ndiyo maana tumeshindwa hata kufika Uwanja wa
Ndege kuupokea mwili na hata kesho (leo) sidhani kama nitakwenda... kuna
mtafaruku mkubwa wakifamilia.”
Baada ya kutimuliwa, Amina ambaye
hawakuwahi kupata mtoto na marehemu Msofe, alilazimika kuondoka kwenye
nyumba hiyo na kwenda Mlandizi kwa wazazi wake.
“Nimeishi na
Msofe kwa miaka mitatu, akiwa kambini mimi niko hapa na wakati mwingine
alikuwa analala huku... lakini leo wamenitimua,” alisema huku akilia.
Habari zilizothibitishwa na baadhi ya waombolezaji waliokuwa nyumbani
kwa marehemu Visiga, Kibaha zinasema baadhi ya wanandugu walimkana Amina
siku chache baada ya kutangazwa vifo hivyo.
Ilidaiwa kwamba
Amina alitimuliwa katika nyumba hiyo Ijumaa iliyopita, saa saba mchana
baada ya ndugu watatu wa marehemu kufika hapo wakitokea Tanga.
Walipofika inadaiwa kuwa walitangaza kusitishwa msiba huo katika nyumba
hiyo na kutangaza kutomtambua mke huyo.
Watu hao waliwaeleza
waombolezaji kuwa walitumwa na baba mzazi wa marehemu, Willbad Msofe
kutoka Kange, Tanga kufika Kibaha kusitisha msiba uliokuwa ukiendelea
nyumbani kwa mtoto wake huyo.
Inadaiwa pia kuwa katika msafara huo, alikuwapo mdogo wa marehemu ambaye aliwahi kuishi kwa miaka miwili na Amina hapo Visiga.
Ilidaiwa
kuwa walipofika nyumbani hapo walionana na mfiwa, Amina na wazazi wake
ambao pamoja na majirani na watu wengine wengi, walikuwa wakimfariji
binti yao huyo.
Mmoja wa waombolezaji alisema baada ya salamu
wanandugu hao walianza kuulizia mali za marehemu na walikuwa wakimuuliza
Amina ambaye aliwaleza kila kitu kilipo na baada ya hapo ndipo
walipomweleza kuwa wametumwa na baba wa marehemu kuwa watu hawatakiwi
kuomboleza kwenye eneo hilo kwani msiba upo Tanga tu ambako ndiko iliko
familia yake.
Alipoulizwa baba wa marehemu, Mzee Msofe alisema:
“Mimi ndiye niliyeagiza nyumba ifungwe na ukweli ninamfahamu Amina,
lakini simtambui kama mkewe kwa kuwa hawajafunga ndoa... Hata wewe si
unayafahamu haya? Uchumba si ndoa na ukifunga ndoa ndipo unatambulika
rasmi,” alisema.
Akiwa kwa wazazi wake Mlandizi jana, Amina alisema:
“Namwachia
Mungu maana hayo yote nashangaa yanatokea wakati huu mume wangu ‘Fortu’
amekufa, mbona kipindi chote cha miaka mitatu iliyopita familia ya
Tanga dada zake na mdogo wake tuliishi nao vizuri kwangu nilipokuwa na
marehemu? Nimeishi na ndugu wote lakini hawakuwahi kuhoji, hata
nilipokwenda na mume wangu Kange baba na mama Msofe nilikaa nao zaidi ya
wiki na hawakunikana, ila nashangaa,” alisema na kulia kwa uchungu.
Akizungumzia
kitendo hicho, baba yake Amina, Juma Juma alisema: “Nimeshangaa hizi
taarifa. Tulikuwa tunajiandaa kupokea msiba wa mwanetu, lakini leo
yanakuja mengine kwa kweli imetushangaza sana.”
“Nasubiri baada
ya kumzika marehemu, nitazungumza nao... Kinachonishangaza ni kwamba
walituandikia barua ya kumposa binti yangu na tukawajibu na gharama
zilikuwa Sh1.2 milioni... Tutazungumza, ngoja hili lipite kwanza,”
alisema mzee Juma.
Maisha ya Amina na ‘Fortu’
Akisimulia
maisha yao, Amina alisema: “Tulianza kuishi Mbezi Luis mwaka 2010 katika
nyumba ya kupanga na nikamshawishi tununue kiwanja na kwa kuwa mimi ni
mwenyeji wa Kibaha, niliwatumia marafiki wa familia yangu Mlandizi
wakatafutia eneo na mwaka 2011 tulipata na tukaanza ujenzi.
“Tukiwa
Mbezi, tulianza kufyatua matofali kisha ujenzi ukaanza Visiga mwaka
2012 mwanzoni na Septemba mwaka huo tulihamia kwenye nyumba yetu na hapo
ndiyo ilikuwa makazi yetu hadi marehemu anaondoka kwenda Darfur.
“Wakati
wote huo ‘Fortu’ alikuwa keshaniposa na hata barua zote za posa zipo na
tulikuwa tukisubiri utaratibu wa kijeshi marehemu kukamilisha miaka
sita ya kukaa kambini kisheria ndipo aruhusiwe kuoa.
“Fortu
alikamilisha miaka hiyo mwaka 2012 mwishoni na wakati akijiandaa kwa
kufunga ndoa ndipo ikatokea safari ya Darfur mwanzoni mwa mwaka huu na
tukakubaliana tusitishe kwanza akirudi tukamilishe, lakini haikuwa....
Halafu wananifukuza wanasema hawanijui,” alieleza huku akiangua kilio.
CHANZO : MWANANCHI
No comments:
Post a Comment