Timu
ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania ya umri chini ya miaka 20 inaanzia
moja kwa moja raundi ya kwanza Kanda ya Afrika kutafuta tiketi ya
kucheza Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Canada.
Kwa
mujibu wa ratiba iliyotolewa jana (Agosti 18 mwaka huu) na Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Tanzania imepangiwa kucheza na Msumbiji
ambapo mechi ya kwanza itachezwa Dar es Salaam kati ya Oktoba 25, 26 au
27 mwaka huu.
Mechi
ya marudiano itachezwa wiki mbili baadaye nchini Msumbiji. Mechi hiyo
inatakiwa kuchezwa kati ya Novemba 8,9 au 10 mwaka huu. Iwapo
itafanikiwa kuitoa Msumbiji itacheza raundi ya pili na mshindi wa mechi
kati ya Botswana na Afrika Kusini.
Raundi
ya Tatu ambayo ndiyo ya mwisho, mechi zake za kwanza zitachezwa kati ya
Januari 10, 11 au 12 mwakani wakati zile za marudiano zitakuwa kati ya
Januari 24,25 au 26 mwakani.
Sudan
Kusini na Uganda ndizo timu pekee kwa Kanda ya Afrika zinazoanzia
raundi ya mchujo ambapo katika mechi ya kwanza zitapambana kati ya
Septemba 13,14 au 15 mwaka huu na kurudiana kati ya Septemba 27, 28 au
29 mwaka huu.
Nchi
17 za Afrika zimeingia kwenye michuano hiyo. Nchi hizo ni Afrika
Kusini, Botswana, Burkina Faso, Equatorial Guinea, Ghana, Guinea Bissau,
Ivory Coast, Misri, Morocco, Msumbiji, Namibia, Nigeria, Sudan Kusini,
Tanzania, Tunisia, Uganda na Zambia.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment