Kana kwamba alisikia kilio cha
wakazi wa Dar es Salaam waliokuwa na shauku ya kumwona lakini
ikashindikana, Rais Barack Obama wa Marekani amewaomba radhi kwa hali
hiyo.
Akizungumza juzi wakati wa dhifa iliyoandaliwa kwa ajili yake na ujumbe wake na Rais Jakaya Kikwete katika Ikulu ya Dar es Salaam, Obama alisema akirudi nchini siku zijazo, atapita mitaani akiwa katika gari la wazi.
"Niliona
wananchi walivyojitokeza kwa wingi kutupokea barabarani, nilifarijika
sana lakini hawakuweza kutuona vizuri kwani tulikuwa ndani ya gari
maalumu-The Beast.
"Miaka ya sitini Rais John Kennedy alipokuja hapa,
alipita na gari la wazi mitaani wananchi wakamwona, naomba radhi nikija
tena nitaonekana," alisema Obama.
Watu wengi waliozungumza na
vyombo vya habari walionesha dhahiri kiu ya kutaka kumwona Rais huyo wa
kwanza mweusi wa Marekani, lakini wakaishia kuona gari lake ambalo hata
hivyo, lilipita kwa kasi barabarani kwenda Ikulu na kurudi Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Kama ilivyokuwa imezoeleka huko
nyuma, Rais wa nchi ambaye amekuwa akifika nchini kwa mara ya kwanza,
amekuwa akipita mitaani kwa gari la wazi sambamba na mwenyeji wake
akisalimiana na wananchi, hiyo imekuwa ikifanyika pia kwa wasanii wa
kigeni.
Hata hivyo, safari hii ulinzi ulionekana kuwa mkali katika ujio wa Rais Obama na kusababisha wenye kiu ya kumwona moja kwa moja kushindwa kufanya hivyo isipokuwa waliokuwa na uwezo wa kufika uwanjani na katika shughuli alizofanya maeneo kadhaa jijini.
Mapema, Rais
Kikwete alimhakikishia Rais Obama kwamba kuanzia sasa Afrika itapenda
kuona ongezeko la uwekezaji na uhusiano wa kibiashara baina yake na
Marekani.
Kikwete alisema hayo juzi usiku katika Ikulu ya Dar es
Salaam katika dhifa ya kitaifa aliyomwandalia Rais Obama ambaye
alimalizia ziara yake jana.
"Hii inaweza kuwa katika ngazi ya mataifa mawili au Taifa la Marekani na eneo la Jumuiya ya Afrika Mashariki," alisema Kikwete.
Alimwambia
uzinduzi wa Mpango wa Nishati ya Umeme kwa Afrika wenye lengo la
kusaidia nchi za Kiafrika kukabiliana na upungufu wa nishati hiyo ni
msaada ambao umekuja kwa wakati mwafaka.
Alisema Afrika imekuwa
ikilenga kuwa na uchumi mkubwa na hatimaye kujiletea maendeleo, lakini
kikwazo kikubwa kimekuwa ni tatizo la umeme wa kutosha.
"Hatua hii ya
Marekani kusaidia katika eneo hilo, itakwenda sambamba na kuwezesha
mataifa ya Afrika kuibua uwezo wao wa kukuza uchumi na kuboresha maisha
ya watu wao," alisisitiza Kikwete.
Alisema hatua hiyo itaimarisha
ushindani, itakuza maendeleo ya viwanda na kufanya nchi za Afrika
kushiriki vizuri katika uchumi wa dunia na kuwa wabia katika biashara ya
kimataifa badala ya kuwa wapokeaji wa misaada ya kigeni.
"Tunakupongeza
kwa uongozi wako katika kukabiliana na changamoto za maendeleo na
usalama zinazolikabili bara la Afrika. Umekuwa kishawishi kikubwa kwetu,
tunaoamini katika demokrasia, uhuru wa mtu, fursa sawa, kutokuwa na
ubaguzi na kuwa na Afrika isiyo na migogoro.
"Wewe ni rafiki wa kweli
wa Tanzania na Afrika, siku zote tutaenzi amali hizo katika nyoyo na
fikra zetu,"Kikwete alimwambia Obama.
Alieleza matumaini ya
Watanzania kwamba Obama atapata fursa nyingine ya kuja nchini na kukaa
angalau kwa muda mrefu kidogo ili ajionee mengi nchini; nchi ambayo ina
vivutio kama Mlima Kilimanjaro, hifadhi za Serengeti na Ngorongoro na
kisiwa cha marashi cha Zanzibar.
Rais Kikwete alimshukuru Rais
Obama na Serikali yake na watu wa Marekani kwa msaada wao endelevu kwa
Serikali na watu wa Tanzania.
"Msaada wenu katika chakula, elimu, afya, barabara, umeme na maji umesaidia kuboresha maisha ya watu wengi nchini Tanzania.
"Naamini
uendelevu wa msaada huo utamaanisha watu wengi kuondokana na umasikini.
Kauli yako ya kutuhakikisha kwamba Serikali yako itaendelea kuisaidia
Tanzania katika maendeleo imepokewa nasi kwa mikono miwili na
unyenyekevu mkubwa," alisema Kikwete.
Akiwa Symbion, Rais Obama
aliihimiza Serikali kuhakikisha miradi ambayo itaanzishwa chini ya
mpango wa Power Africa utekelezaji wake uharakishwe ili kutoa fursa kwa
wananchi kuona manufaa yao katika kujipunguzia umasikini.
Alisema
katika mpango huo ambao Serikali yake imeahidi kutoa dola za Marekani
bilioni 7, alisema sekta binafsi ambayo itahusishwa kwa kiasi kikubwa
katika utekelezaji wake itatoa dola za Marekani bilioni 9.
Alisema
kutakuwa na manufaa makubwa iwapo mpango huo utahusisha Serikali na
sekta binafsi kwa upande mwingine akiongeza kuwa dhamira ya sekta
binafsi katika kutoa kiasi hicho cha fedha inaonesha nia ya Marekani
kuinua Afrika yenye nuru," alisema Rais Obama akionesha matumaini ya
mpango huo ambavyo unaweza kunufaisha nchi nyingi za Afrika.
Obama
ambaye aliitumia hotuba hiyo kuaga Watanzania, alisema Symbion ni mfano
wa miradi ambayo Marekani imedhamiria kuitekeleza Afrika ya kuongeza
maradufu uzalishaji wa nishati ya umeme ambayo lengo ni kupunguza
umasikini katika bara hilo.
Alisema ili miradi hiyo iwe na manufaa
kwa nchi husika kote alikopita, alitoa mwito kwa viongozi kuhakikisha
utekelezaji unaharakishwa ili kunufaisha nchi na kwa watu.
Alikemea
tabia ya ucheleweshaji wa miradi katika Afrika ikiwamo ya umeme lakini
akasema ana imani na uongozi wa Rais Kikwete kuwa mpango huo
utatekelezwa kwa kasi. "Ni lazima tuongoze katika utekelezaji wa miradi
hii na naamini chini ya Rais Kikwete hili linawezekana."
Alisema ili
kufanikisha kuwa na umeme wa uhakika ni vema kupunguza urasimu katika
kuhudumia wawekezaji wa sekta ya umeme ili wapate nafasi ya kuongeza
kasi ya utekelezaji wa miradi.
Aliongeza kuwa ufanikishaji wa mpango
huo utakuwa ni hatua ya ushindi kwa pande zote; yaani kwa Tanzania
ambayo itapata umeme wa uhakika ambao utasaidia kupunguza umasikini,
lakini pia kwa Marekani ambako wafanyabiashara watapata fursa ya
kuwekeza nchini.
Pia alitaka sheria na taratibu zifuatwe na
kuheshimiwa katika masuala yote ya uwekezaji ambao utahusisha miradi
itakayoanzishwa chini ya mpango wa Power Africa.
Alipoingia ndani ya mitambo ya Symbion, Rais Obama alikabidhiwa mpira wenye uwezo wa kuzalisha umeme wa gesi.
Mpira
huo ambao umebuniwa na vijana wa Kimarekani, unafaa kwa matumizi
vijijini kwani unaweza hata kuchaji vifaa vya umeme kama simu ambapo pia
gesi hiyo ina uwezo wa kuwasha taa inayoweza kutumika kumulika ndani ya
nyumba.
Rais Obama alizindua mipira hiyo ambayo itapatikana hivi
karibuni nchini kwa kumpasia Rais Kikwete na kueleza matumaini yake kuwa
inaweza kuwa na manufaa makubwa katika maeneo ambako hayajafikiwa na
umeme.
Kampuni ya Symbion yenye makao yake makuu Washington, Marekani
imeajiri Watanzania 1,000 na Rais Obama jana alitangaza kuwa ni kampuni
pekee ambayo itasimamia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umeme
inayofadhiliwa na Serikali ya watu wa Marekani.
Symbion kwa sasa
inatekeleza miradi yenye uwezo wa kuzalisha umeme katika nchi za Afrika
Mashariki na Magharibi ambayo imepangwa kukamilika mwishoni mwa mwaka
huu.
Katika miaka mitano, kampuni hiyo imepanga kuwekeza kiasi cha Sh
trilioni 3 katika uzalishaji umeme na njia za kuusafirisha.
Kati ya
miradi hiyo, umo wa gesi unaojengwa Mtwara wenye uwezo wa megawati 400
na unaendeshwa kwa kushirikiana na kampuni nyingine ya Marekani ya
General Electric (GE) itakayotoa vifaa vya ujenzi katika mradi huo ambao
unahusisha ujenzi wa njia ya umeme yenye umbali wa kilometa 650.
Nchini,
kampuni hiyo kwa sasa inamiliki vituo vitatu vya kuzalishia umeme wa
jumla ya megawati 217 ambavyo vipo Dar es Salaam, Dodoma na Arusha.
Kituo cha Ubungo cha Symbion kinazalisha megawati 112 kwa gesi na ndiyo
kampuni inayozalisha umeme mwingi unaoingizwa kwenye gridi ya Taifa.
Mitambo
hiyo imetengenezwa mjini Houston, Texas na inaelezwa kuwa ya kisasa
zaidi yenye uwezo mkubwa wa kufua umeme kwa kasi kama ilivyo injini ya
ndege. Mitambo hiyo awali ilikuwa ya Dowans ambayo iliileta nchini baada
ya kupewa zabuni ya kufanya hivyo na Kampuni ya Richmond.
Awali
baadhi ya wabunge walishauri inunuliwe na Serikali, lakini baadhi yao
walikataa kuwa ni mitumba na sheria ya manunuzi hairuhusu. Lakini
mitambo hiyo ambayo baadhi ya Watanzania waliikejeli leo ndiyo kimbilio
la Serikali kutokana na vyanzo vya kufua umeme wa maji kupungua uwezo
wake.
Kutokana na mapenzi mengi waliyonayo Watanzania kwa Obama,
jana maelfu ya watu walikusanyikwa Ubungo ili kumwona Rais huyo mweusi
wa Marekani.
Tangu saa mbili asubuhi Ubungo ilishafurika watu na hadi
anawasili eneo hilo saa 5 asubuhi umati huo ulishaongezeka hali
inayoonesha kuwa Rais huyo ni kipenzi cha Watanzania.
Baada ya
kukagua mitambo ya Symbion, Rais Obama alisindikizwa na mwenyeji wake,
Rais Kikwete hadi uwanja wa ndege na akapanda ndege yake ya Air Force
One na kurejea Marekani.
No comments:
Post a Comment