facebook likes

Tuesday, July 30, 2013

Hizi ndizo sifa za kiungo bora mshambuliaji

 
‘ Jesus Love You’, ni maandishi ambayo kwa mara ya kwanza yalionekana katika t-shirt ya ndani ya kiungo, Mbrazil Ricardo Kaka’ wakati wa mchezo wa fainali wa michuano ya kombe la fifa la mabingwa wa mabara dhidi ya waliokuwa wenyeji wa michuano hiyo, timu ya Ujerumani, Juni 2005.
Baada ya kuisaidia Brazil kushinda na kutwaa ubingwa huo, Kaka’ alisema, ” Nilipokuwa mdogo nilitaka kuwa mchezaji wa kulipwa katika timu ya Sao Paulo, na kuichezea Brazil walau kwa mchezo mmoja tu. Lakini Mungu amenipa zaidi ya nilichomuomba”
Kaka’ aliyepata mkataba wake wa kwanza wa soka la kulipwa akiwa na umri wa miaka 15 katika timu ya Sao Paulo, mahali ambako alijifunza soka tangu akiwa na umri wa miaka nane. Juini, 2003 mara baada ya AC Milan kutwaa ubingwa wa ligi ya mabingwa Ulaya, Kaka’ alisajiliwa klabuni hapo na kocha Carlo Ancelotti kwa ada ya uhamisho, euro million nane.

Akatangaza zaidi jina lake klabuni hapo kwa mchezo wake wa ‘ macho, maangavu’ na kuwa kiungo mchezesha timu bora wa Ulaya. Akatwaa mataji ya Serie A, L igi ya mabingwa, Klabu bingwa ya dunia na tuzo nyingi binafsi na ile kubwa zaidi, mwaka 2007 alipotwaa tuzo ya mwasoka bora wa dunia. Wakati wa majira ya kiangazi, 2009 Kaka’ akajiunga na timu ya Real Madrid kwa ada ya euro million 66 na kuwa miongoni mwa wachezaji watatu ghali zaidi kuwahi kutokea duniani, nyuma ya Cristiano Ronaldo na Zinedine Zidane. Hadi sasa Kaka’ amecheza jumla ya mechi , 515 na kufunga mabao 171, na amepiga pasi zaidi ya 80 za mabao.

Yeye ni namba kumi hasa anapokuwa uwanjani na katika mfumo wa 4-4-1-1 chni ya kocha Carlo katika uwanja wa San Siro alifunga mabao 70 katika michezo 193, huku akikumbwa na majeraha ya mara kwa mara katika kipindi chake chote cha uchezaj, Kaka’ anapokuwa na uwezo wa kukimbia bila maumivu, anabaki kuwa kiungo bora mshambuliaji mwenye mtazamo wa kusonga mbele hata pale nafasi inapokuwa inaonekana ndogo. Kaka’, anauwezo mkubwa wa kupiga pasi za kupenyeza, na ukitazama kwa umakini kwa sasa utagundua hakuna kiungo bora mshambuliaji mwenye kupiga pasi hizo, labda pale anapopata nafuu katika kikosi cha Real na kuonesha uwezo huo. Si, bora sana katika kuzuia na ndiyo maana kocha, Ancelotti aliwafanya kina Clarence Seedorf, Rinno Gattuso, Massimo Ambrosini na Andrea Pirlo kumzunguka Mbrazil huyo ili kumpa uhuru zaidi wa kupiga pasi za hatari kwa wapinzani wake.
Kiungo bora mshambuliaji ni Yule mwenye mtazamo wa kusonga mbele na kupiga pasi timilifu kwa safu ya mashambuliji. Kiungo bora wa ushambuliaji ni Yule mwenye uwezo wa kuusoma mchezo na kutafuta njia ya kupitisha pasi sahihi kwa wenzake. Mtazame vizuri, Kaka’ anapokuwa ‘ fit’, huwa hapendi kupiga pasi za kurudi nyuma na hilo ndilo ambalo kocha wake wa zamani, Carlo amesema analihitaji kutoka kwa kiungo huyo katika timu ya Real Madrid msimu ujao. Carlo anasema anataka ‘ kufufua’ kipaji cha Kaka’ ambacho kocha Jose Mourinho alikaribia kukizika. Akiwa amecheza michezo 85 tukatika kikosi cha ‘ Los Blancos’ , Kaka’ ameweza kufunga mabao 23, wakati Mesut Ozil akiwa amecheza michezo 102 na kufunga mabao 19 tu. Kaka’ ni kiungo ambaye sit u ni mfungaji bali pia anauwezo wa kuisaidia timu yake kujilinda mchezoni kwa kuwa ni mchezaji ambaye anauwezo wa kumiliki mpira kwa muda mrefu katika himaya yake. Alitengeneza mabao 46 akiwa na Milan, na ametengeneza mabao 32 akiwa na Real. Kama unataka kiungo bora mshambuliajki katika timu yako basi mpatie sifa za uwezo wa Kaka’.

No comments:

COMMENTS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...