MWALIMU
Mkuu wa Shule ya Msingi Chalinze Mzee, wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani,
Elias Kapama, yuko katika wakati mgumu baada ya kuhamishia ofisi yake
kwenye vyoo vya wanafunzi kutokana na jengo la ofisi yake kuharibika
vibaya.
Hatua ya
kuhamia chooni ilitokana na mkuu huyo kutawaliwa na hofu ya ubovu wa
ofisi yake, hivyo kushindwa kufanya kazi zake kwa ufasaha unapotokea
upepo au mvua.
Novemba
2012, Kapama alihamishia ofisi yake katika jengo la vyoo vya wanafunzi
ambavyo havijaanza kutumika tangu ujenzi wake ukamilike mwaka 2011.
Akizungumzia
hali hiyo, Kapama alisema kuwa anajisikia vibaya kutumia chumba maalumu
cha kubadilishia nguo cha wavulana katika choo hicho kutokana na kukosa
msaada kutoka halmashauri ya wilaya hiyo.
Alisema
kuwa ni miezi tisa sasa tangu ahamishie ofisi yake chooni na hakuna
hatua zozote zilizochukuliwa na ngazi ya wilaya pamoja na kufahamu
mazingira hayo, hali aliyodai kuwa inamweka katika wakati mgumu.
“Sina
ofisi, nimelazimika kuomba kwa wafadhili waliotujengea vyoo kwa ajili ya
wanafunzi niweze kutumia chumba hiki cha kubadilishia nguo kama ofisi
yangu hadi pale tutakapojenga ama kufanyia ukarabati ofisi ya zamani,”
alisema.
Vyoo
hivyo ambavyo vimejengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Ebenezer Spritual
Center ya mjini Chalinze, vimegharimu kiasi cha sh milioni 70 hadi
kukamilika.
Mkuu huyo
aliongeza kuwa kwa sasa walimu wanatumia tundu moja la choo huku
wanafunzi 450 wakitumia matundu saba, matatu kwa wanawake na manne kwa
wavulana.
Hata hivyo Tanzania Daima ilishuhudia choo hicho kinachotumika sasa kikiwa hakina hadhi na usalama kwa watumiaji.
Aliuomba
uongozi wa wilaya pamoja na wizara ambao umetembelea shule hiyo na
kushuhudia mazingira hayo magumu kufanyia utekelezaji wa ujenzi wa ofisi
hiyo haraka ili aweze kuhama kutoka chooni.
No comments:
Post a Comment