New York. Muda wa saa 48 wa kusalimisha
silaha kwa waasi wa March 23(M23), Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Congo umemalizika na wakati wowote mapigano yanaweza kuanza.
Misheni ya Kutuliza Amani ya Umoja wa
Mataifa(Monusco) , ilitoa saa hizo zinazomalizika leo na Jeshi la UN
litaanza kutumia nguvu kunyang’anya silaha waasi hao.
Taarifa iliyotolewa na Monusco
iliyotolewa na Msimamizi wa Misheni hiyo, Luteni Jenerali Carlos Alberto
dos Santos Cruz na kusambazwa na Idara ya Mawasiliano ya Umoja wa
Mataifa jana, inaeleza kwamba, watu binafsi katika eneo la Kivu ya
Magharibi ambalo linajumisha Goma na Sake na ambao hawahusiki na vyombo
vya usalama wamepewa saa 48 kuanzia saa kumi jana (juzi) kwa saa za Goma
(Jumanne) kuzisalimisha silaha zao.
Taarifa ilisema, “Baada ya saa 10 jioni
ya Alhamisi, Agosti Mosi, wale wote ambao watakuwa hawajasalimisha
silaha zao watachukuliwa kama tishio kwa usalama wa wananchi na Monusco
itachukua hatua zote muhimu kuwapokonya silaha hizo ikiwa ni pamoja na
kutumia nguvu kama ilivyoainishwa katika mamlaka na sheria za ushiriki
za Monusco.”
Kwa mujibu wa taarifa hiyo zaidi ya
wananchi milioni moja wanaishi katika eneo dogo la Goma na Sake na
kandokando ya barabara ambayo inawaunganisha na kambi ya wakimbizi ya
Mugungu ambayo ni makazi ya muda ya watu karibu 70,000 ambao
wameyakimbia makazi yao kutokana na mapigano.
Kwa mujibu wa Monusco,tangu katikati ya
Mei eneo hilo limeshuhudia mapigano ya mara kwa mara kutoka kwa Kundi la
M23 dhidi ya Majeshi ya Serikali ya FARDC ikiwa ni jaribio la wazi la
kutaka kusonga mbele kuelekea Goma na Sake. “Katika mashambulizi
hayo,likiwamo la hivi karibuni la Julai 14, M23 walitumia kiholela
silaha zao za moto zikiwamo silaha nzito ambazo zimesababisha wananchi
kujeruhiwa.”
Taarifa hiyo imeongeza kwamba kundi hilo la M23 katika mashambulizi hayo limelenga pia Vituo vya Umoja wa Mataifa.
Taarifa hiyo inabainisha kwamba eneo
hilo maalumu la usalama (security zone)litasaidia kudhibiti tishio la
moja kwa moja mbali na eneo la nje ya Goma na pengine eneo hilo linaweza
kupanuliwa na kurudiwa sehemu nyingine kutakako hitajika.
Tamko hilo la kutoa saa 48 kwa waasi
kusalimisha silaha zao linafuatia kuwasili katika eneo la Goma kwa
Kamanda Mkuu wa Monusco, Luteni Jenerali Carlos Alberto dos Santos Cruz
ambaye alitangaza kwamba Misheni ya Monusco itaunga mkono Jeshi la
Serikali(FARDC) katika kuanzisha eneo la usalama kuzunguma eneo la Goma
na vitongoji vyake.
No comments:
Post a Comment