facebook likes

Thursday, August 1, 2013

MIAKA 50 YA AU BALOZI AMINA SALUM ALI ANENA


0-23Balozi Amina Salum Ali. 0-24Washiriki wa mkutano.
Umoja wa Afrika mwaka huu 2013 umetimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na kilele cha maadhimisho hayo yalifanyika mwezi Mei katika makao makuu ya Umoja wa Afrika yaliyopo jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Katika mwendelezo kwa kuchambua ajenda za kimaendeleo na mafanikio ya Umoja huo, taasisi ya Utafiti na uchambuzi wa maswala ya jamii, uchumi na siasa ya Brookings iliyo jijini Washington Marekani, iliandaa kongamano fupi juu ya mustakabali na mwelekeo wa Umoja wa Afrika kwa miaka 50 ijayo.
Akiongea katika kongamno hilo lililojumuisha wakurugenzi toka Benki ya Dunia, Mabalozi wanaowakilisha nchi za Afrika hapa Marekani pamoja na wadau na wasomi wa siasa na uchumi, mwakilishi wa umoja wa Afrika kwa nchi ya Marekani Balozi Amina Salum Ali, alisema kuwa Afrika imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo ukilinganisha na miaka 50 iliyopita.
Balozi Amina alieleza washiriki wa kongamano hilo kuwa licha ya hatua za ukombozi na kimaendeleo zilizofikiwa na Umoja wa Afrika, bado changamoto zinazohitaji uwajibikaji wa nchi wanachama katika kutekeleza maazimio yanayofikiwa na umoja huo ikiwemo kuimarisha demokrasia na utawala bora. Kusoma zaidi bofya
Naye mkurugenzi wa Sera ya uchumi na mpango wa kupunguza umaskini Afrika kutoka Benki ya Dunia Bwana Marcelo Giugale alisema licha ya Benki ya Dunia kuwa mdau mkubwa katika kusaidia Umoja wa Afrika, changamoto zilizopo kwa sasa ni pamoja na upanuzi wa teknolojia isiyofungamana na unyonyaji wa rasilimali za Afrika, swala la elimu ya uvumbuzi na ubunifu, swala la vifo vya mama na mtoto hasa kwa wazazi , ukuzaji wa miundombinu inayoendana na mahitaji ya sasa na matumizi ya ardhi kwa makazi na maendeleo. Licha ya changamoto hizo, Bwana Giugale alisisitiza kuwa Afrika ndio kivutio kikubwa cha uwekezaji na hivyo Benki ya Dunia haina budi kuendelea kusaidia Umoja wa Afrika kwa miaka ijayo kwa manufaa ya kukuza uchumi na uwekezaji.
Akijibu maswali ya washiriki wa kongamano hilo, Balozi Amina kwa upande wake alifafanua juu ya kuwa na demokrasia madhubuti yenye kuheshimu utawala bora akitilia mkazo Changuzi huru na haki. Umoja wa Afrika kwa kipindi cha nyuma, ilikuwa haina mamlaka ya kwenda kusimamia uchaguzi wa nchi yeyote ndani ya Afrika bila kibali cha mwaliko wa nchi hiyo. Kwa ajili ya kuwa na dhamira ya kweli ya kuwa na demokrasia madhubuti, Umoja wa Afrika uliidhinisha na kuipa Umoja wa Afrika mamlaka ya kuingia na kusimamamia uchaguzi katika nchi zote za Afrika kabla na baada ya uchaguzi bila kungoja kibali chochote. “Hatua hii inaipa Umoja wetu kuwa huru kuhoji na kuota maelezo thabiti juu ya zoezi la uchaguzi ilivyoendeshwa na nini kiboreshwe kwa changuzi zijazo” alisema Balozi Amina.
Kongamano hilo pia liliambatana na utoaji wa majarida na santuri zinazoonesha na kuelekeza dira ya Umoja wa Afrika kwa miaka 50 ijayo ikiwemo mkazo kwa uwezeshwaji wa Vijana nguvu kazi ya bara la Afrika, kupambana na magonjwa sugu kukuza demokrasia ya utawala bora na kubwa zaidi kuimarisha Umoja wa shirikisho la kiuchumi ndani ya bara la Afrika kwa kukuza jumuiya za kikanda ikwemo SADC EAC COMESA na kadhailika.

No comments:

COMMENTS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...