MBINU mpya za usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), zimeanikwa baada ya kubainika kuwa mbwa wanaotakiwa kuchunguza dawa za kulevya kuondolewa sehemu husika.
SOMA ZAIDI...........
Habari za uhakika ambazo MTANZANIA Jumatatu limezipata, zinasema hatua ya kuwaondoa mbwa katika maeneo husika, kulisababisha kutoa mwanya kwa wasafirishaji wa ‘unga’ kupita kirahisi bila kushtukiwa.
Mbali na kitendo hicho, imebainika kuwa baadhi ya watumishi wa uwanja huo, wamekuwa wakitumia kila mbinu kuhakikisha dawa hizo zinapitishwa ama kwa maslahi ya wasafirishaji au wao.
Moja ya mbinu iliyobuniwa na watu hao ni kutumia misafara ya viongozi wa kitaifa, ambapo mbwa maalumu wa kunusa dawa za kulevya huondolewa katika maeneo ya ukaguzi wa mizigo ya abiria na kupelekwa katika misafara hiyo.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, hata kibanda cha mbwa kilichojengwa ndani ya uwanja huo kwa zaidi ya miaka mitano sasa, kimebaki pambo la uwanja kwa kuwa hakitumiwi kuhifadhia mbwa hao.
Chanzo hicho, kilisema kibanda hicho kilijengwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kipindi ambacho biashara hiyo ilishika kasi, huku lengo likiwa ni kuwezesha mbwa kuwapo mahali hapo muda wote.
“Hapa kuna tatizo kwa sababu hata polisi ambao wana jukumu la kupambana na kudhibiti dawa za kulevya hawana meno juu ya jambo hili.
“Mbwa wa kugundua dawa za kulevya ni muhimu sana, lakini wako chini ya Idara ya Usalama wa Taifa ambao ili wafike hapa, lazima wawe wamepewa taarifa za mzigo unaotiliwa shaka.
“Lakini kama mbwa hao wangekuwa chini ya Jeshi la Polisi, ingekuwa rahisi kufanya kazi tofauti na ilivyo sasa.
“Mbinu nyingine inayotumiwa ni mbwa wanaotumika kutambua mabomu, ndio wanaoletwa kunusa dawa za kulevya, sasa hapa unadhani kuna uwezekano wa kudhibiti dawa hizo,” kilihoji chanzo chetu.
Kwa upande wake, aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege Tanzania, Deusdedit Kato kabla ya kuondolewa katika nafasi hiyo, alikiri kuwapo kwa kibanda hicho na kueleza kuwa mbwa waliokuwa chini ya jeshi hilo, walichukuliwa na Idara ya Usalama wa Taifa.
“Siwezi kueleza moja kwa moja kwanini mbwa walichukuliwa, bali kulitokea tatizo. Hatuwezi kufanya kazi kwa kujibagua, tunafanya kazi kwa kushirikiana na idara nyingine,” alisema Kato.
Akizungumzia umuhimu wa kuwapo kwa kibanda hicho, alisema mbwa waliopo kiwanjani hapo wapo katika gari la watu wa Idara ya Usalama wa Taifa, hivyo kibanda hicho kinaweza kutumika kama gari hilo litaharibika.
“Hakuna haja ya kukibomoa, kinaweza kutumika kwa dharura kama gari la usalama wa taifa linalotumika kubebea mbwa limeharibika,” alisema Kato.
Hivi karibuni, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alihoji kesi 36 zinazohusiana na dawa za kulevya ambazo Jeshi la Polisi limekaa kimya kwa kutoeleza hatua zilipofikia, hali inayotia shaka na kudhoofisha vita dhidi ya biashara hiyo haramu.
Dk. Mwakyembe alisema Watanzania wafahamu nini kinachoendelea kuhusiana na kesi hizo na kuahidi kuzifuatilia ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na biashara hiyo.
Kuhusu baadhi ya vigogo kudaiwa kujihusisha na biashara hiyo, alisema kama yupo mtu ambaye anawafahamu kwa majina vigogo hao, ampelekee taarifa kwa kuwa suala hili lilipofikia sasa halihitaji usiri.
Kuhusu maofisa wa uwanja huo wa ndege waliodaiwa kula njama za kupitisha kilo 150 za dawa za kulevya zilizokamatwa Afrika Kusini, alisema atashangaa iwapo atasikia kuwa wamepeleleza na ushahidi haujajitosheleza.
Agosti 15, 2013, Dk. Mwakyembe, aliwataja maofisa usalama wanne wanaodaiwa kuhusika katika njama za kusafirishwa kwa dawa za kulevya kutaka wafukuzwe kazi na kufunguliwa mashitaka ya jinai chini ya sheria ya kuzuia dawa za kulevya.
Gazeti hili hivi karibuni lilinasa nyaraka mbalimbali ambazo zilionyesha mchezo mchafu uliofanywa JNIA, uliowawezesha wasichana wawili wa Kitanzania na mshirika wao, Said Mangunga, kupenya na kilo 150 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh bilioni 6.8.
Wasichana hao ni Agnes Gerald (25) na Melisa Edward (24), waliokamatwa Julai 5, mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Thambo, Afrika Kusini.
chanzo:mtanzania
No comments:
Post a Comment