Maji ya kunywa ya chupa. |
Shirika la Viwango Tanzania(TBS), limesitisha leseni za alama za ubora ya TBS, katika bidhaa za kampuni 48, zikiwamo za maji ya kunywa, magodoro, taulo za wanawake, mvinyo na vifaa vya magari.
Tangazo lililotolewa jana na TBS, lilieleza kuwa kampuni hizo ni za Tanzania Bara, Zanzibar na nje ya nchi zikiwamo za India, Misri na China.
Bidhaa za maji ya kunywa ya chupa ambazo leseni ya ubora imesitishwa ni pamoja na maji ya Great Zone ya kampuni ya Great Zone Investment na Raha ya kampuni ya Raha Pure Drinking Water zote za Dar es Salaam.
Mengine ni maji ya Uzima ya Kampuni ya Uzima Beverages Co. Limited na AAMFA Beverage Limited ya Dar es Salaam, maji ya Uluguru ya kampuni ya Uluguru Fountain ya Morogoro na maji ya Siha, ya kampuni ya Siha Beverages Limited ya mkoani Kilimanjaro.
Pia TBS imesitisha leseni ya bidhaa za karatasi laini ya Soft Facial Tissue ya kampuni ya Alawy Supplies Limited ya Zanzibar, biskuti za Milki Marie, zinazotengenezwa na kampuni ya Britania Products na nyavu za samaki za Nylon Fishing Twine & Fishing za Imara Fishnet (T) Limited zote za Dar es Salaam.
Bidhaa zingine ni fulana zinazotengenezwa na kampuni ya Kibo Trade, matofali ya GM Gross Africa Limited na taulo za kike, zinazotengenezwa na kampuni ya Hengan Sanitary & Baby Products Limited.
Zipo pia bidhaa za rangi za kampuni ya Chui Paints, mifuko ya plastiki ya kampuni za Centaza Plastics, Tropical Plastics za Dar es Salaam na Roto Flex Packaging ya Moshi.
Katika bidhaa za betri zimo betri za Dry Cell (Euro Cell) za kampuni ya Euro Solo Energy ya India na Dar es Salaam, na betri za kampuni ya 777 Battery Factory ya China.
Bidhaa za magodoro zilizonyang’anywa nembo hiyo ni ya Jumbo Foam ya kampuni ya Sabira Investment ya Arusha na Foam ya Olyform (T) ya Dar es Salaam.
Pia sabuni za Laundry’s na za Jamii za kampuni ya Mbasira Investment ya Shinyanga, mbegu za korosho za Frabho Enterprices ya Dar es Salaam na Munawar Cashewnut ya Mbeya.
TBS pia imenyang’anya nembo yake kwa mafuta ya alizeti ya Sun Shine ya kampuni ya Mardona Edible Oil Millers ya Moshi, na ya A to Z Oil Mills ya Dar es Salaam.
Zipo pia bidhaa za mtindi uliosindikwa wa ladha ya nanasi, vanilla na strawberry, unaotengenezwa na kampuni ya Morani Dairy ya Tanga, jibini na mtindi vya kampuni ya Kyaka Milk Processing ya Bukoba.
Nyingine ni bidhaa za mvinyo Pineapple Wine ya kampuni ya Kivumbui ya Arusha, Fruit Wine (Golland Banana wine) ya kampuni ya Victoria Food ya Mara na juisi inayotengenezwa na Unnat Fruits Processing ya Morogoro.
Akizungumza na mwandishi jana kuhusu uamuzi huo, Msemaji wa TBS, Roida Andusumile, alisema kanuni za TBS zinataka kampuni husika kuomba leseni ya kutumia nembo hiyo kila mwaka.
Alifafanua kwamba sababu za kuzuia leseni hizo ni pamoja na baadhi ya bidhaa kusitishwa kuzalishwa na kampuni husika au viwanda kufungwa.
No comments:
Post a Comment