facebook likes

Friday, August 30, 2013

Majambazi wapora Sh. bilioni moja benki Dar

Watu wanane wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za moto mmoja kati yao akiwa amevalia sare za Jeshi la Polisi na mwingine akiwa na simu ya upepo wamevamia Benki ya Habib Kariakoo jijini Dar es Salaam na kupora zaidi Sh. bilioni moja.
SOMA ZAIDI...........

Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema tukio hilo lilitokea jana saa 3:00 asubuhi katika benki hiyo iliyopo mtaa wa Livingston Kariakoo na majambazi hao walifika katika benki hiyo wakiwa na gari aina ya Toyota Noah namba  T 817 BPZ.

Kova alisema fedha zilizoporwa ni Sh. milioni 781 na Dola za Marekani 181,885 (Sh. milioni 294.6) na kufanya idadi ya fedha zote zilizoporwa kuwa Sh. 1,076,653,700.

“Majambazi hayo yalipofika katika benki hiyo wakijifanya ni wateja wa kawaida waliosindikizwa na askari polisi aliyevaa sare waliingia kimyakimya na kuwaweka chini ya ulinzi wafanyakazi wa benki hiyo pamoja na wateja wanne waliokwenda kupata huduma,” alisema Kova .

Alisema majambazi hao walikuwa wakizungumza Kiingereza na wakati mwingine Kiswahili japo kwa taabu na mmoja wao alikuwa na asili ya kiasia na wote walikuwa na silaha ndogo na walianza kuchukua fedha kwa mtunza fedha na kisha kuvunja milango miwili ya ofisi na mlango wa kuelekea chumba cha kuhifadhia fedha.

Kova alisema baadaye walimwamuru Meneja wa benki hiyo, Daniel Matemba, na  wasaidizi wake wawili kufungua chumba cha kuhifadhia fedha na kuchukua fedha zote zilizokuwemo.

Aliongeza kuwa inawezekana mchezo huo ulipangwa na wafanyakazi wa benki hiyo kutokana na majambazi hayo kufahamu kwa majina wafanyakazi waliokuwa na funguo za kuhifadhia fedha.

Alisema watu watakaosaidia kupatikana kwa majambazi hao ambao hadi jana jioni walikuwa hawajakamatwa watazawadiwa Sh. milioni 100.

Meneja Matemba, mlinzi mmoja na wafanyakazi wengine kadhaa wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano

Awali mlinzi mmoja wa benki hiyo wa kampuni ya ulinzi ya SGA ambaye aliomba  jina lake lisitajwe ambaye amekuwa zamu baada ya wenzake waliokuwa zamu kushikiliwa, alisema majambazi hao walipofika kwa walinzi wa nje walisema wanakwenda kuchukua fedha.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

COMMENTS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...