facebook likes

Thursday, October 10, 2013

HENRY JOSEPH ALETA UTATA SIMBA


Henry Joseph 
KIUNGO wa Simba, Henry Joseph, ameondolewa katika kambi ya Simba huku Ramadhan Chombo ‘Redondo’ akirudishwa kikosi cha pili.
SOMA ZAIDI.......
Habari za uhakika ambazo tumezipata, zinasema Henry ambaye amesajiliwa na Simba msimu huu huku akilipwa mshahara wa Sh1.5 milioni, alikorofishana na kocha wake, Abdallah Kibadeni, Jumatatu wiki hii katika mazoezi ya asubuhi yaliyofanyika katika  Uwanja wa Kinesi, Dar es Salaam.
Henry anayemudu kucheza nafasi ya ulinzi na kiungo, alirudi nchini mwaka huu akitokea klabu ya Kongsvinger ya Norway iliyoshuka daraja.  Kurejea kwake kumetokana na kukataa mkataba mpya wa klabu hiyo wenye pesa kiduchu baada ya timu kuyumba kiuchumi.
Jumatatu wiki hii, wakati Simba ikiwa katika mazoezi ya asubuhi kabla ya kuondoka jioni yake kwenda kambini Bamba Beach, Henry alifanya mazoezi ya kukimbia pekee yake na baadaye wachezaji wote walipofika uwanjani Kibadeni aliwataka wakimbie kwa pamoja, lakini Henry inadaiwa aligoma kwa madai kuwa alikuwa tayari ameshafanya mazoezi ya peke yake.
Hata hivyo, Henry alipozungumza na  jana Jumatano, alikanusha vikali madai hayo na kusema kuwa hawezi kufanya kitendo kama hicho maishani mwake kwani anaheshimu wajibu wake.
“Sijawahi kufanya utovu wa nidhamu kwa kocha. Nilifika pale saa 11 alfajiri, nilikuwa wa kwanza. Nikafanya mazoezi ya kukimbia pekee yangu ili kujiweka fiti kwa sababu muda mwingi nilikuwa majeruhi. Baadaye wenzangu walipofika nikajumuika nao, lakini Julio (Jamhuri Kihwelu) akaniambia nipumzike kwani nimechoka,” alisema Henry.
Alisema alivyoambiwa hivyo alimfuata Kibadeni kumwambia kuwa ameambiwa na Julio apumzike na baada ya hapo akawa amekaa nje ya uwanja huku wenzake wakiendelea na mazoezi.
“Nilishangaa wakati Kibadeni anatangaza kikosi cha kuingia kambini Bamba Beach, alisema sitakwenda na timu, badala yake nikafanye mazoezi ninayoyajua mimi na kwamba akinihitaji ataniita,” alisema Henry.
Alisema anamheshimu kila mtu na kwamba katika maisha yake amejitahidi kufuata misingi na nidhamu ya soka na ndio maana bado haelewi kisa kilichotokea mpaka Kibadeni kuamua kumuacha.
Henry alisema ili kujiweka fiti, ameendelea kufanya mazoezi asubuhi na jioni na wakati mwingine amekuwa akienda gym, lakini kwa sasa hayupo katika mazoezi ya Simba.
Tulimtafuta Kibadeni kuzungumzia hilo na alilisukuma suala hilo kwa Kocha Msaidizi, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ ambaye majibu yake hayakuwa ya moja kwa moja, lakini yalitosha kuthibitisha.
Julio alisema kila mchezaji anatakiwa kuwa na nidhamu na kujituma katika mazoezi na kwenye mechi na asiyefanya hivyo hurudishwa kikosi cha pili.
“Mbona hamsemi kuhusu Redondo, wiki mbili sasa yupo katika kikosi cha pili, mnauliza mambo mengine tu, hapa nidhamu na kiwango kwanza mengine yanafuata,” alisema Julio.
“Mchezaji ukiwaridhisha makocha kwa kiwango chako, utabaki katika kambi hii na mechi utacheza, lakini usipoturidhisha unarudi kikosi cha pili, hiyo ndio falsafa yetu.
“Lakini huyo aliyekwambia Henry kasimamishwa ni mnafiki na mzandiki, anataka kuleta chuki tu miongoni mwetu kwani sisi hatusimamishi mtu. Mchezaji mwenyewe anajisimamisha kwa kiwango chake kibovu na nidhamu mbovu.”
Simba imeanzisha mtindo mpya katika siku za hivi karibuni kwa kuwaweka kambini Bamba Beach, Kigamboni wachezaji 20 tu ambao wanaonyesha kiwango kikubwa kwenye mazoezi na kwenye mechi.
Chini ya utaratibu huo, mchezaji yeyote atakayeonyesha kiwango kibovu, hubaki kwenye kikosi cha pili cha timu hiyo ambacho huwa kinafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Kinesi.
Hata hivyo hali ndani ya Simba imekuwa si shwari katika siku za karibuni kutokana  na wachezaji wazoefu kutuhumiwa kucheza chini ya kiwango jambo linalowakosesha amani makocha wa timu hiyo.


chanzo:mwanaspoti

No comments:

COMMENTS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...