MAUAJI
ya wafanyabiashara wakubwa ‘mabilionea’ yameshika kasi nchini ambapo
baada ya tajiri mkubwa Arusha, Erasto Msuya kuuawa kwa risasi hivi
karibuni, Agosti 3, 2013 bilionea Elia Daniel Endeni (49) naye aliuawa
kwa kupigwa risasi nje kwa mwanamke anayedaiwa kuwa ni mke wake mdogo
aitwaye Juliana Labson (28).
....SOMA ZAIDI....Tukio hilo lilijiri siku hiyo saa 2 usiku
maeneo ya Temeke Mikoroshini jijini Dar es Salaam ambako ni nyumbani kwa
Juliana.Elia alikuwa na kampuni iitwayo Elia Herdons Ltd ya kupakua na
kupakia mizigo ya makontena bandarini, maduka na majumba ambapo polisi
walikuta shilingi 151,000,000 taslimu ofisini kwake akiwa amezihifadhi.
Ilidaiwa kuwa muda huo, Elia alikuwa amefika nyumbani kwa mwanamke huyo
lakini kabla hajashuka katika gari lake, Pick-up lenye namba za usajili T
319 AFJ alichomolewa kwenye gari na kupigwa risasi na watu wawili
wasiojulikana.
Taarifa zilieleza kwamba waliotekeleza unyama huo walikuwa wakimfuata marehemu huyo kwa nyuma wakiwa kwenye pikipiki.
Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili walisema marehemu alikuwa na
kawaida ya kufika nyumbani kwa Juliana nyakati za usiku na kabla ya
kushuka kwenye gari, alikuwa akimpigia simu mwanamke huyo ili afungue
mlango.
“Ilikuwa wakati anapiga simu ndipo alivamiwa na watu hao ambao walivunja
kioo cha gari kwa kutumia kitako cha bastola kisha kutoa ‘loki’ ya
mlango na kumchomoa.
“Walimdhibiti bila kutoa sauti, wakati huo sisi tulikuwa tumekaa nje
tukishuhudia lakini tuliamini kwamba huenda walikuwa wamegongana
barabarani kwani hata marehemu hakusikika akiomba msaada,” alisema
mwanamke mmoja jirani ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Mwanamke huyo aliendelea kusema kwamba hakukusikika mlio wa risasi, bali marehemu alianza kulia ghafla akiomba msaada.
Aliongeza kuwa watu walipokaribia eneo la tukio, wauaji hao walipiga
risasi mfululizo hewani, kitendo kilichowafanya watawanyike kuokoa
maisha yao na majambazi hayo yakatoweka.
Inadaiwa majirani walipofika, walimkuta tajiri huyo akiwa amelala katika
dimbwi la damu huku ameishiwa nguvu kiasi kwamba alishindwa kuongea
chochote.
Habari zinasema mke huyo mdogo aliyezaa naye watoto wawili, alipotoka
ndani alizimia baada ya kuona Elia akiwa katika dimbwi la damu.
Muda mfupi baadaye, polisi walifika eneo la tukio na kumchukua majeruhi
kumpeleka Hospitali ya Temeke ambapo alifariki dunia akiwa njiani.
Taarifa zinadai kwamba Julai 28, mwaka huu marehemu Elia alikoswa na
risasi akiwa njiani kwenye gari akitokea msibani Same, Kilimanjaro.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, ACP Engelbert Kiondo amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kusema kwamba walifika katika eneo hilo wakiwa
na wasiwasi kwamba huenda watu hao walimnyang’anya bastola.
“Ilitubidi twende ofisini kwake Kurasini na kupekua, tukaikuta bastola.
Hili suala linaonekana ni kisasi kwa sababu wamemuua bila kuchukua kitu
chochote, tunaendelea na upelelezi,” alisema Kamanda Kiondo.
Mazishi ya Elia yalifanyika Jumatano iliyopita, Same ambapo Juliana
alikuwa miongoni mwa waombolezaji. Mke mkubwa wa marehemu aishiye Kimara
King’ong’o jijini Dar ndiye aliyekuwa ameongoza msiba huo.
No comments:
Post a Comment