Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limetangaza dau
la Sh100 milioni kwa mtu atakayewezesha kupatikana kwa taarifa za kundi
la uhalifu linalojihusisha na vitendo vya kuwamwagia maji baadhi ya
watu yanayodhaniwa ni tindikali.
Hatua hiyo inatokana na vitendo hivyo kushamiri maeneo mbalimbali nchini.
Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Suleiman Kova,
alisema vitendo hivyo havipaswi kuvumiliwa na kuwaomba wananchi kutoa
ushirikiano kwa kuwafichua watu hao.
“Nimeamua kuomba fedha hizi serikalini ili nimpe
mtu atakayewezesha kupatikana kwa taarifa hizo, hatimaye kukomesha
vitendo hivi. Kemikali hii imekuwa na madhara makubwa,” alisema Kova.
Hivi karibuni Mkurungezi wa Maduka ya Home
Shopping Center, Mfanyabiashara wa Lebonon na raia wawili wa Uingereza
walimwagiwa maji yanayodhaniwa ni tindikali.
Wakati huohuo, polisi linamshikilia raia wa
Uingereza kwa tuhuma za kukutwa na nyara mbalimbali za Serikali zenye
thamani ya zaidi ya Sh100 milioni, vikiwamo vipande vinane vya meno ya
tembo.
Kova alisema mtuhumiwa huyo ambaye ni Mkurugenzi
wa Kampuni ya Usafirishaji Mizigo (TALL), alikamatwa juzi saa 2:00 usiku
maeneo ya Mbezi Beach, wilayani Kinondoni.
Alisema alipopekuliwa nyumbani kwake alikutwa na
meno 20 na kucha 22 za Simba, shanga mbalimbali zilizotengenezwa kwa
meno ya tembo, Kasuku na nyara nyingine ambazo hairuhusiwi kumiliki bila
kibali.
Alisema uzito wa nyara hizo ni kilo 25, walimkuta
na mawe mbalimbali yanayodhaniwa ni madini sambamba na ganda moja la
bomu lenye ukubwa mita 130.
No comments:
Post a Comment