WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ameunga mkono hoja binafsi ya Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia kuhusu udhaifu wa elimu nchini akisema, kuna udhaifu mkubwa katika sekta hiyo.
Lowassa alisema hayo jana katika Mahafali ya 13 ya
Kidato cha Sita ya Shule ya Sekondari Benjamini William Mkapa, jijini
Dar es Salaam ambapo alieleza kuwa sekta ya elimu inahitaji kufanyiwa
marekebisho ili kuweza kuzalisha wahitimu wenye tija kwa taifa.
”Kuna tatizo la hali ya elimu nchini, tushirikiane
wazazi, jamii, wanasiasa na wataalamu, tuangalie jinsi ya kusaidia
sekta ya elimu kwa maana tutasaidia watoto wa nchi yetu,”alisema
Lowassa.
Katika mahafali hayo, Lowassa ambaye pia ni Mbunge
wa Monduli mkoani Arusha kupitia (CCM) aliwakabidhi vyeti jumla ya
wahitimu 330, kati yao wavulana 263 na wasichana 67 .
“Wabunge wengi bungeni tunakubaliana kwamba ipo
haja ya kutazama upya suala zima la mitalaa ya elimu katika nchi yetu
kwani elimu iliyopo inawaandaa watafuta kazi na siyo wanaotaka
kujiajiri,”alisema Lowassa.
Alisema kuwa kukiwa na mfumo mzuri wa elimu wenye
kuwaandaa wahitimu walio na uwezo wa kujiajiri wenyewe na kutokutegemea
kuajiriwa taifa litapiga hatua.
Alihamisi wiki hii, Mbatia aliwasilisha bungeni
Hoja Binafsi kuhusu Udhaifu wa Elimu Tanzania, akitaka mfumo mzima
unaosimamia elimu nchini ufumuliwe, hoja iliyogeuka ‘kaa la moto’ kwa
Serikali.
Baada ya majadiliano marefu kuhusu kuundwa kwa
kamati ya kuchunguza mitalaa, sera na mihutasari ya elimu, hoja
mbalimbali zilitolewa, huku baadhi ya wabunge wakitaka Kamati ya Bunge,
wengine wakitaka iundwe tume huru ya kufuatilia suala hilo.
Mjadala huo uliendelea juzi asubuhi kwa Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kusimama na kutetea
mfumo wa elimu uliopo na kusisitiza kuwa Serikali inayo mitalaa, kabla
ya wabunge kuchangia na Mbatia kuhitimisha akitaka kuiondoa hoja yake
hadi Serikali itakapowasilisha mitalaa hiyo ya elimu bungeni.
Hata hivyo, Naibu Spika, Job Ndugai alikataa
pendekezo la Mbatia na kutumia kanuni za Bunge za kuipitisha hoja hiyo
kwa kuwahoji wabunge.
Baada ya hoja hiyo kupitishwa kwa kuungwa mkono na
wabunge wengi wa CCM, hali hiyo iliwaudhi wabunge wa upinzani, ambao
waliamua kutoka nje ya ukumbi.
Baadaye walikubaliana kumshtaki Waziri Kawambwa
kwenye Kamati ya Bunge ya Mamlaka ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge,
wakimtaka ajiuzulu kwa kulidanganya Bunge, ikishindikana watalipeleka
suala hilo kwa mamlaka zilizomteua.
No comments:
Post a Comment