facebook likes

Tuesday, October 15, 2013

WAPINZANI KUTINGA IKULU LEO

  *Lipumba: Tunaamini hoja zetu ni za msingi
*JK sasa amkumbuka Nyerere Katiba Mpya
RAIS Jakaya Kikwete leo anatarajia kukutana na viongozi wa muungano wa vyama vya upinzani, Ikulu jijini Dar es Salaam. Hatua ya Rais Kikwete kukutana na wapinzani hao, imekuja baada ya wabunge wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, kususia muswada uliowasilishwa na Serikali kuhusu sheria ya mabadiliko ya Katiba.
SOMA ZAIDI.............
Muswada huo wa marekebisho ya pili ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ulizua balaa bungeni, hali iliyowalazimu wabunge wa kambi ya upinzani kutoka nje ya Bunge. Wabunge hao walikuwa wakishinikisha Muswada huo usisomwe hadi pale yatakapopatikana maoni ya wadau kutoka Zanzibar.

Katika mkutano wa 12 wa Bunge uliofanyika Agosti mwaka huu, Mbunge wa Konde, Khatibu Said Haji (CUF), aliwaongoza wenzake vyama vya Chadema na NCCR-Mageuzi na CUF, kutoka nje huku Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP), akibaki ndani ya Bunge.

Msemaji wa kambi hiyo kwa Wizara ya Sheria na Katiba, Tundu Lissu alisema Bunge linahitaji kuangalia upya suala la uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge Maalumu, ili kutimiza matakwa ya kisheria.

 
Alisema kwa mujibu wa kifungu cha 22 (2) cha Sheria, idadi ya wajumbe wa Zanzibar katika Bunge Maalumu watakaotokana na makundi yaliyoainishwa katika kifungu cha 22(1) (c).

Kutokana na hali hiyo, iliwalazimu wapinzani kutangaza maandamano nchi nzima kama njia ya kumshinikiza Rais Kikwete, asisaini muswada huo hadi pale watakaposhirikishwa wadau kutoka Zanzibar.

Kupitia hotuba ya Rais Kikwete ya Septemba mwaka huu, alisema kuwa hoja za wapinzani zinazungumzika mezani, huku akiwataka kuacha kufanya maandamano.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Muungano huo, Profesa Ibrahim Lipumba, tayari wamepokea barua ambayo imewafikia tangu Oktoba 10.

“Tumepokea rasmi barua Oktoba 10, kwa hiyo tunaamini mazungumzo yetu yatakwenda vizuri, tunatarajia atasikiliza hoja zetu na kuzifanyia kazi.

Alisema kitendo cha Rais Kikwete kutoa mwaliko kwa viongozi hao, ameonyesha nia njema kwa ajili ya kusikiliza maoni yao juu ya matatizo yaliyopo katika Muswada wa marekebisho ya mabadiliko ya     Katiba.

“Kitendo cha Rais Kikwete kukubali tu ni kwamba ameonyesha ‘Good will’ (nia njema), kwa hiyo tunaamini mambo yatakwenda sawa na kutakuwa na mwisho mzuri,” alisema Profesa Lipumba.

Ikulu katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Oktoba 7, mwaka huu na Kurugenzi ya Mawasiliano, ilionyesha kuwa muswada huo haujamfikia na endapo utamfikia atausaini kwani umepitia taratibu zote za kikatiba ikiwemo kupita Bungeni.

Katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, Rais Kikwete alisema madai ya Kambi ya Upinzani yanazungumzika na hata baadhi yangeweza kukubalika kama wabunge wake wangekuwepo bungeni.

Rais Kikwete alisema kuandamana nchi nzima au kuchukua hatua za kutotii sheria kama Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anavyotaka, hakutaleta mabadiliko wanayoyataka katika sheria hiyo.

Rais Kikwete alitaka busara iwaongoze viongozi wa vyama hivyo, ili waweze kutumia utaratibu uliotumika mwaka jana wa kufanya mazungumzo ya kina badala ya maandamano.

Katika hatua nyingine, vyama 16 vya siasa vyenye usajili wa kudumu visivyokuwa na uwakilishi bungeni, navyo vimeomba kukutana na Rais Jakaya Kikwete Ikulu.

Vyama hivyo ni UMD, NLD, UPODP, NRA, Tadea, Demokrasia Makini, Chausta, DP, PPT-Maendeleo, Jahazi Asilia, Sau, AFP, CCK, ADC na Chauma.

Uamuzi huo wa vyama hivyo umekuja siku chache baada ya Rais Kikwete kuwaalika kwa mazungumzo viongozi wa vyama vikubwa vya upinzani nchini.

Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete, amewataka Watanzania kuzingatia hotuba na mawazo ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere kwani yatasaidia mchakato wa kupata Katiba Mpya kufikia mwisho.

Rais Kikwete alitoa wito huo jana mjini Iringa, alipokuwa akihutubia mamia ya wananchi katika maadhimisho ya kilele cha mbio za Mwenge ya Uhuru yaliyofanyika kitaifa mkoani humo.

Maadhimisho hayo yalikwenda sambamba na kilele cha Wiki ya Vijana na Kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki dunia Oktoba 14, 1999 mjini London Uingereza.

“Katika mchakato wa Katiba tusisahau kujikumbusha mawazo ya Mwalimu kuhusu umoja wetu na Muungano wa Zanzibar, hotuba zake tukizifuatilia zitatusaidia kufikia mwisho katika mchakato wa kupata Katiba Mpya.

“Tujiepushe kupuuza mawazo ya Mwalimu Nyerere, tuwe makini katika kufanya mabadiliko yatakayotupeleka mbele.

“Mwaka 2013 nchi imepita katika majaribu makubwa, lakini pepo mbaya amepita na sasa hali iko shwari, waliotaka kutufarakanisha walishindwa na wengine walidondokea pua.

“Tuwe makini wanaweza kurudia kutugawa tena, tuendelee kukataa ushawishi wa kutugawa kwa udini na vinginevyo, hakuna atakayefanikiwa nchi itakapogawanyika, bila amani hakuna maendeleo,” alisema.

Rais Kikwete alisema, Serikali italinda umoja na mshikamano na itakemea kwa uwezo wake wote vitendo vinavyosababisha chokochoko zitakazosababisha mvunjiko wa umoja.

Akizungumzia maambukizi ya UKIMWI kitaifa, alisema yamepungua kutoka asilimia 7 hadi asilimia 5.1 na kuwaasa Watanzania kupambana na ugonjwa huo, kwani unasababisha yatima wengi.

“Nina ombi kwa wanaume, wale wasiofanyiwa tohara, wajitokeze kufanyiwa. Madaktari wanasema, waliofanyiwa tohara wana nafasi kubwa ya kunusurika kuambukizwa.

Kuhusu rushwa, Rais Kikwete alisema Serikali kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), itaendelea kupambana kwani rushwa imekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo.

Alisema Serikali itaendelea kuimarisha TAKUKURU ili iweze kutimiza wajibu wake na wananchi watoe ushirikiano kwa kutoa taarifa za rushwa.

Akizungumzia dawa za kulevya, alisema Serikali inatambua hila za wafanyabiashara wa dawa hizo ambao wamekuwa wakitafuta mbinu mpya za kufanya biashara hiyo haramu.

“Dawa za kulevya zinaathari mbaya, Serikali haitachoka, haitasita kupambana, wakibadili mbinu na sisi tutabadili mfumo wa uchunguzi.

“Kuanzia Januari hadi Septemba 2013, watu 2,000 wamekamatwa na aina mbalimbali za dawa za kulevya, wakiwemo wafanyabiashara na kilo 681 za heroin zilikamatwa,” alisema.

Alisema mchakato wa kuunda chombo kipya chenye nguvu cha kupambana na dawa za kulevya nchini, umeanza na kitakuwa na nguvu kuliko TAKUKURU.

Hata hivyo Rais Kikwete alirejea kuwataka wananchi kuwataja watu wanaojihusisha na biashara hiyo, kama hatua ya kuisaidia Serikali katika vita hiyo.

“Baadhi ya watu wanawajua watu wanaojihusisha na dawa za kulevya, watajeni ili tushinde kupambana na biashara hiyo haramu,” alisema Rais Kikwete.

No comments:

COMMENTS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...