facebook likes

Tuesday, October 15, 2013

MAMA WA MTOTO ALIYEKUFA NA KUFUFUKA AVAMIWA NA MAJAMBAZI NA KUMJERUHI VIBAYA

Siku tatu baada ya mtoto Shaban Maulid (15) aliyedaiwa kufariki kisha kuonekana akiwa hai mwishoni mwa mwezi jana, kuruhusiwa hospitalini alikokuwa amelazwa,watu wasiojulikana wanaosadikiwa kuwa majambazi wamevamia nyumbani kwao mtaa wa 14 Kambarage mjini hapa na kumjeruhi mama wa mtoto huyo baada ya kumpora fedha aliyokuwa amechangiwa na wasamaria wema wakati akimtibisha mwanaye.

Picha: Bi.Aziza Ramadhani akiwa na jeraha baada ya kuvamiwa na majambazi
 SOMA ZAIDI.....
Mama wa mtoto huyo Aziza Ramadhan (45) alivamiwa usiku wa manane wa kuamkia leo kisha kuporwa fedha taslimu tsh 210,000 ambayo ilikuwa michango aliyopewa na wasamaria wema wakati akimuuguza mtoto wake katika hospitali ya wilaya ya Geita.


Imedaiwa na majirani wa mama huyo ambao hawakutaka kutajwa majina yao gazetini kuwa majambazi hao walivamia nyumbani kwa mama huyo majira ya saa tisa usiku ambapo walipiga mlango kwa jiwe kubwa maarufu kama fatuma kisha kuingia ndani.

Watu wao waliokuwa na siraha za jadi walimweka mama huyo chini ya ulinzi huku wakimtaka awape pesa alizokuwa akichangiwa hospitali ndipo alipowapa kiasi laki mbili na elfu kumi ambacho walidai ni kidogo mno na kumtaka aongeze.

Baada ya kujitetea kwao kuwa hana pesa nyingine walimjeruhi kichwani kwa kitu chenye ncha kali na kusababisha jeraha kichwani na kulazimika kukimbazwa hospitali kwa matibabu zaidi.

Akizungumzia tukio hili Afisa mtendaji wa kata ya Kalangalala Bw.Hamad Hussen amesema usiku wa kuamkia leo familia zipatazo kumi zimevamiwa na watu hao na kuporwa fedha pamoja na vitu mbalimbali

Aliwataja baadhi ya watu waliovamiwa na kujeruhiwa kuwa Peter Kulwa(24) Maneno Sungura(32) wote wakazi wa mtaa wa 14 Kambarage ambao walitibiwa hospitali na kuruhusiwa

Akiongea na mwandishi wa habari hizi Kaimu mganga mfawidhi Dr,George Rweyemera alisema walifikishwa watu watatu hospitalini hapo alfajiri ambapo walitibiwa kisha waliruhusiwa kurudi nyumbani kutokana na hali zao kutokuwa mbaya.

"Aziza alifika hapa majira ya saa kumi na moja alfajiri akiwa na jeraha kichwani,alihuhumiwa na kupatiwa dawa na tumemruhusu maana hakuwa ameumia sana" alisema Dr.George

Hata hivyo baadhi ya majirani walioongea na mwandishi wa habari hizi walionesha wasiwasi wao kuwa huenda watu hao walilenga kumdhuru mtoto huyo ambaye alikuwa ameruhusiwa kutoka hospitali juzi .

"Inawezekana hawa watu walikuja kumchukua Shaban ila wakamkosa ndio wakadai pesa kama lengo la uvamizi huo" alisema mmoja wa majirani.

Hata hivyo mtoto Shaban hayupo nyumbani kwao akidaiwa kuondoka na baba yake Maulid Shaban na kuhifadhiwa sehemu ambayo imedaiwa ni siri ya familia wakati wakisubiri majibu vinasaba (DNA) kutoka kwa mkemia mkuu wa serikali.

Shaban alifariki Januari Mosi 2011 na kuzikwa kisha kuonekana akiwa hai baada ya kukutana na mama yake Septemba, 30 mwaka huu tokea wakati huo alikuwa akipata huduma ya kitabibu na ya kisaikolojia katika hosipitali ya wilaya ya Geita hadi Okitoba 10 aliporuhusiwa kwenda nyumbani.

Jitihada za kumtafuta kamanda wa polisi mkoa wa Geita Leonard Paulo hazikuzaa matunda na alipopigiwa simu kupitia simu yake ya kiganjani ili kuthibitisha tukio hilo alisema hayuko sehemu nzuri.

"siko sehemu nzuri kwasasa haloo.....eeeh siko sehemu nzurii!" alijibu Kamanda

Aidha jeshi la polisi wilaya ya Geita wamekiri kutokea kwa tukio hilo na kudai uchunguzi wa tukio hilo unaendelea

No comments:

COMMENTS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...