facebook likes

Wednesday, October 9, 2013

Mabasi yaungana na malori kugoma

mgomo-mabasi_490_280
BAADHI ya mabasi yanayofanya safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa mbalimbali nchini, jana yaligoma kusafirisha abiria kwa saa kadhaa.
SOMA ZAIDI.....
Yalifanya hivyo kushinikiza Serikali isitekeleze Sheria ya Barabara inayotaka mzigo ukizidi tani 56, mmiliki atozwe faini. Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), kinataka Serikali isitoze faini magari yenye uzito usiozidi asilimia tano, juu ya tani 56 zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.
Kutokana na msimamo wa Serikali uliotangazwa mwanzoni mwa mwezi huu kuwa atakayezidisha uzito atatozwa faini, Taboa kiliamua kusitisha usafiri kwa abiria, wakiwemo wagonjwa na waliokuwa wakisafiri kwa ajili ya shughuli mbalimbali, ikiwemo misiba.
Abiria waliokuwa katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo (UBT), walijikuta wakikumbana na adha ya kukosa usafiri iliyodumu kwa zaidi ya saa tatu kuanzia Saa 12.00 asubuhi hadi saa 3.21.
Wenye biashara zao Wakati mgomo huo ukiendelea, baadhi ya mabasi ya Kampuni za Dar Express, Taqwa, Metro East African, Tawaqal, Tahmeed, Raha Leo, Smarts, Ratco Express na Modern, yaliendelea na safari zao.
Mabasi hayo yaliondoka na abiria kituoni hapo, huku wakiacha gumzo kwa baadhi ya viongozi wa Taboa, waliokuwa wakidai kuwa wamesalitiwa.
Mabasi hayo yakiongozwa na Metro East African No. KBV 664E, lililokuwa likielekea Kampala nchini Uganda, yalianza kutoka kituoni hapo Saa 1.38 kwa kutumia geti la kuingilia. Polisi ilikuwa imeimarisha ulinzi dhidi ya baadhi ya watu, waliokuwa wakitishia kuzuia mabasi kutoka getini.
*Mazungumzo, ruhusa
Wakati mabasi hayo yakiendelea na mgomo, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Barabara kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra), Gilliad Ngewe alikuwa katika kikao cha dharura na Ofisa Mfawidhi wa Sumatra Kanda ya Mashariki, Conrad Shiyo na viongozi wengine wa mamlaka hiyo.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama wa Barabarani, Mohammed Mpinga na uongozi wa Taboa, wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Severine Ngaro.
Baada ya kikao hicho saa 3.21 za asubuhi, mabasi yalianza kutoka mfululizo kwa kutumia milango yote miwili. Viongozi hao kwa pamoja walikubaliana mabasi yote kwa jana, yasafiri bila kupima katika mizani, ili kuwaondolea usumbufu zaidi abiria kwa jana wakati suala hilo likitafutiwa ufumbuzi.
Akizungumzia suala hilo, Ngewe alisema wamiliki wa mabasi walistahili kuchukuliwa hatua pale pale kwa kuwaandikia faini, lakini waliamua kutumia busara kwa lengo la kunusuru tatizo lililokuwepo.
“Kwa kitendo hiki Taboa wamekiuka masharti ya leseni, wao wana mkataba na abiria, hawakupaswa kugoma kwa kuwa tayari walishawakatia tiketi abiria kwa ajili ya safari. “Ili kuwaondolea usumbufu walioupata abiria kwa zaidi ya saa tatu, tuliwasiliana na Tanroads (Wakala wa Barabara) na Waziri John Magufuli, ambaye ametoa idhini kwa mabasi kusafiri bila kupima katika mizani kwa leo tu,” alisema Ngewe.
Mgomo wa leo
Ngaro alipongeza uamuzi wa kuruhusu mabasi kusafiri bila kupima kwa jana. Alidai kuwa mgomo huo ni endelevu hadi madai yao yatakapofanyiwa kazi.
“Tunawaomba abiria na wananchi wanaotarajia kusafiri kesho (leo), wasikate tiketi kwa kuwa hatutarajii kuendelea kutoa huduma hadi pale tutakapowatangazia, vinginevyo hatutahusika na usumbufu watakaoupata.”
Arusha
Mkoani Arusha mabasi yanayofanya safari zake kwenda mikoa ya Tanga na Dar es Salaam, yaligoma kuondoka Kituo Kikuu cha Mabasi kwa zaidi ya saa tatu na kusababisha abiria kushindwa kujua hatma yao.
“Tutaondoka hapa, lakini hatujuwi tutawapeleka wapi abiria na safari yetu itakapokwamia ni hapo hapo, lakini huku ni kutesa abiria, bora tungeacha kuwachukua hapa kituoni, mpaka mgomo umalizike,” alisema mmoja wa madereva hao, Swalehe Amuri.
Madereva hao waliomba Serikali kufuata utaratibu kama wa nchi jirani ya Kenya na Uganda, ambao walidai hawana sheria hiyo ya mizani.

No comments:

COMMENTS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...