UMOJA wa vyama vya upinzani vya NCCRMagaeuzi, CUF na Chadema, umesitisha maandamano yaliyokuwa yafanyike kesho.
Maandamano hayo yalikuwa ya kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete, asisaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013, uliopitishwa hivi karibuni na Bunge.
Vyama hivyo viliungana hivi karibuni kupinga kusainiwa kwa muswada huo, kwa madai una vipengele vinavyohitaji mabadiliko na umepitishwa kinyume na taratibu.
Akitoa tamko hilo kwa niaba ya wenyeviti wenzake, Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema wamefikia uamuzi huo baada ya Ikulu, kutoa taarifa kuwa iko tayari kukutana na viongozi wa upinzani, kuzungumzia suala hilo.
“Tumesikia kupitia vyombo vya habari ambavyo navyo vimenukuu taarifa kutoka Ikulu, inayobainisha kuwa Rais Jakaya Kikwete amepanga kukutana na viongozi wa upinzani kati ya Oktoba 13 na 15 ili kujadili na kupata muafaka wa suala hili la Katiba. “Tunaamini kuwa taarifa hizi ni sahihi kabisa, hivyo tumeamua kusitisha maandamano yetu, yaliyolenga kushinikiza nguvu ya umma kuungana nasi katika kudai mchakato wa kuipata Katiba shirikishi, na kushinikiza Rais kutosaini kabisa muswada huo wa sheria kwa kuwa una upungufu,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema umoja huo ulishasikia na kuitambua nia ya Rais Kikwete aliyoionesha katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, ambapo alibainisha wazi kuwa atakutana na viongozi wa vyama hivyo, kuzungumzia suala hilo la Muswada wa Katiba.
Kutokana na nia hiyo, alisema vyama hivyo havina budi kusitisha kwanza mchakato mzima wa maandamano na mikutano hiyo ya hadhara hadi mazungumzo na Rais, yatakapokamilika na kutoa dira ya kinachoendelea.
“Pamoja na kuahirisha maandamano haya, tunapendekeza huo mkutano ulioahidiwa na Rais, ufanyike mapema ili mchakato wa Katiba unaosuasua kwa sasa, uendelee kwa ufanisi na kuwezesha kupatikana kwa Katiba iliyoandaliwa na Watanzania wote,” alisema.
Madai yao
Alisema madai ya umoja huo ni kutaka mchakato wa Katiba shirikishi, utakaoheshimu matakwa ya Watanzania wote wa Tanzania Bara na Zanzibar ili kupata Katiba iliyotengenezwa na wananchi wenyewe.
Vyama hivyo kupitia umoja huo, vilipanga kufanya maandamano makubwa kesho, yaliyokuwa yaanzie Tazara na Mwenge hadi Jangwani jijini Dar es Salaam, kushinikiza kutosainiwa kwa muswada huo wa sheria.
Polisi Hata hivyo, pamoja na umoja huo kusitisha maandamano hayo, tayari Polisi kupitia Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alishapiga marufuku maandamano hayo, kwa madai kuwa yatasababisha usumbufu kwa wasafiri wengine na kupendekeza wafuasi wa vyama hivyo wakutane Jangwani bila maandamano.
Juzi Ofisi ya Rais, Ikulu, ilitoa taarifa na kubainisha kuwa inaangalia uwezekano wa kuitisha mkutano huo wa Rais na viongozi wa upinzani siku ya Jumapili ya Oktoba 13 ama Jumanne ya Oktoba 15, mwaka huu kujadili suala hilo.
Aidha ofisi hiyo kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilifafanua kuwa bado muswada huo haujamfikia Rais, na kwamba ukimfikia inatarajiwa kuwa atautia saini.
Taarifa hiyo ya Ikulu, ilifafanua kwamba Rais atasaini muswada huo kuwa Sheria, kwa kuwa umepitia katika mchakato sahihi na halali wa Kikatiba kwa maana ya kufikishwa bungeni na Serikali, kujadiliwa na kupitishwa na Bunge.
Hata hivyo taarifa hiyo ilifafanua kuwa kusainiwa kwa muswada huo, hakumaanishi kwamba hautafanyiwa marekebisho kama yapo.
“Kama yapo marekebisho ambayo yanaonekana yanafaa kufanywa katika Sheria hiyo, basi yatafanywa na Bunge baada ya Rais kuwa ametimiza matakwa ya Kikatiba ya kutia saini muswada ambao umepitishwa na Bunge kutokana na mchakato sahihi na halali wa Kikatiba,” ilieleza taarifa hiyo.
Hoja ya Lisu
Wakati huo huo, wanasheria wameunga mkono utaratibu wa Rais kutia saini muswada huo kwa hoja kwamba umepitia mchakato sahihi na halali wa Kikatiba.
Wanasheria hao wameshangaa mwanasheria mwenzao na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), kwa ushauri wake alioutangaza kwa umma, kumtaka Rais asisaini muswada huo.Walifafanua kwamba ushauri huo ni wa kisiasa zaidi, usio na tija kwa uongozi, unaofuata utaratibu na sheria.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, walisema Muswada huo kama ilivyo miswada mingine ya sheria, una nafasi ya kusainiwa na kama kuna marekebisho, unarudishwa bungeni kujadiliwa na kufanyiwa marekebisho.
Wakili wa kujitegemea, John Mapinduzi alisema kuwa Lissu ni mwanasiasa na anachofanya ni kujaribu kupotosha umma. “Lazima muswada huo usainiwe ndipo urudishwe bungeni kwa marekebisho, Lissu ni mwanasiasa tu anapotosha umma… sasa utarudishwaje bungeni wakati ulishapita?” Alihoji Mapinduzi.
Mwanasheria mwingine wa kujitegemea, Jerome Msemwa alisema kusainiwa muswada huo ni njia sahihi ;na inafanyika mara nyingi na kama kuna marekebisho, yanafanyika baadaye.
“Wabunge kama Lissu waliamua kutoka wenyewe bungeni wakati muswada unajadiliwa… hakuna aliyewafukuza, sasa iweje leo watake usisainiwe? Haina maana leo hii kumshauri Rais kutosaini. “Ushauri wa Lissu, kisheria hauna maana yoyote, hawezi kumshauri Rais leo asisaini wakati anafahamu kuwa hata baada ya kusainiwa, kuna nafasi ya kurudishwa bungeni na kujadiliwa kwa marekebisho yoyote,” alisema Msemwa.
Msemwa alisema Rais asiposaini muswada huo na kuurudisha bungeni, maana yake vikao vya wabunge vilivyokaa Dodoma kujadili muswada huo, vilipoteza muda na fedha za wananchi bure.
Lissu katika taarifa yake, alisema kama Rais anataka wamuamini, asisaini muswada huo ;na akiusaini, atakuwa ameendeleza mambo ya ki-CCM. Imeandikwa na Halima Mlacha na Regina Kumba
No comments:
Post a Comment