WACHUNGAJI WA DINI SASA KUCHUNGUZWA...MAOVU, UTAPELI KWA VIVULI VYA DINI VYATAWALA!!!....HABARI KAMILI HAPA!!!!
SERIKALI
imesema itaanza kuchunguza madhehebu ya dini kutokana na migogoro na malalamiko
ya waamini dhidi ya viongozi wao kuongezeka.
SOMA ZAIDI....
Viongozi hao
ni hasa wa kigeni kutokana na vitendo vyao vya kitapeli wanavyodaiwa kuvifanya,
vikiashiria kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya kwa kivuli cha
dini.
Aidha,
baadhi ya viongozi wanaolalamikiwa ni wachungaji na wanadaiwa baadhi
yao kumiliki ardhi (mashamba) na migodi ya mamilioni ya fedha nchini
kinyume cha sheria na wamejiandikisha katika mchakato wa kupata
vitambulisho vya Taifa kama raia wa Tanzania.
Ingawa
malalamiko yapo mengi serikalini, lakini ya hivi karibuni (barua na
nyaraka za malalamiko tunazo) ni ya waamini wa Kanisa la The Bible
Believers Church (BBC Mission) la Pugu Kajiungeni linalomhusisha pia
Mchungaji wa Kanisa la Cornerstone la Tabata, yote ya Dar es Salaam.
Wanadai
pia kuwa baadhi ya wachungaji walianza kuhubiri usiku wa manane katika
mitaa ya Dar es Salaam wakidai wameagizwa na Mungu kuiteka Dar es Salaam
na muda mzuri ni usiku, jambo linalowapa wasiwasi wafuasi wao zaidi wa
aina ya Injili wanayohubiri.
Wanadai
wachungaji wao (majina tunayo), raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC) wamekuwa sababu ya migogoro ya kifedha na mali za Kanisa
isiyokwisha kwa kile walichodai wameshindwa kutoa taarifa za fedha kwa
waamini pale walipotakiwa kufanya hivyo.
Aidha,
waamini hao kwa barua zao walizoandika kwa nyakati tofauti kwenda
Wizara ya Mambo ya Ndani (nakala tunazo), wanadai na kulalamika kuwa
wachungaji hao wamejiandikisha kupata vitambulisho vya Taifa kama raia
wa Tanzania waliozaliwa Kigoma na Mbeya, wakati wakijua wazi kuwa si
raia.
Walidai
kuwa hofu kubwa ya hatima ya usalama na makanisa yao imetanda kwao na
wanaiomba Serikali ichunguze wachungaji hao haraka iwezekanavyo, kuwa
huenda wanatumia kivuli cha Kanisa kufanya utapeli nchini, kwa kile
walichodai wanahubiri usiku wa manane katika mitaa ya Dar es Salaam.
“Tunaiomba
Serikali iwachunguze watu hawa haraka, wana vibali vya kimisionari vya
kufanya kazi nchini kwa muda, lakini tunashangaa kwamba wamejiandikisha
kupata vitambulisho vya Taifa kama raia, hatujui nia yao hawa watu, sasa
hivi wanajimilikisha ardhi kutumia watoto wao, hali si shwari kabisa,”
alisema muamini mmoja ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake gazetini.
Uchunguzi
uliofanywa na gazeti hili baada ya malalamiko ya waamini hao wiki
chache zilizopita umebaini kuwa, wapo wachungaji katika makanisa kadhaa
jijini humo, wameanzisha mtindo wa kuhubiri usiku wa manane katika mitaa
ya Jiji la Dar es Salaam na kufanya vikao katika majumba ya starehe
(baa) na katika kuhubiri huko, hutumia magari wanayoyabadili rangi mara
kwa mara.
Hali
hiyo ya mashaka inahusishwa pia na matukio ya kihalifu yanayokithiri
nchini, ambayo baadhi yanahusisha mpaka viongozi wa kidini ikiwamo
biashara haramu ya kuuza dawa za kulevya, ukahaba na ujambazi.
Kwa
mujibu wa nyaraka tulizonazo, Mchungaji wa Kanisa la BBC Mission lenye
namba za usajili SA 7446 anayelalamikiwa inaonesha kuwa Kanisa hilo
humkatia vibali vya kufanya kazi vya muda mfupi wa miaka miwili, kwa
mujibu wa taratibu za Uhamiaji lakini amejiandikisha kama raia mzaliwa
wa nchini.
Askofu
wa Kanisa hilo la BBC Mission, Frank Mwangende alipoulizwa kuhusu jambo
hili, alikiri kuwepo kwa mgogoro katika Kanisa lao tawi la
Pugu-Kajiungeni na kueleza kwa ufupi kuwa, uongozi wa Kanisa unalifanyia
kazi.
Pia,
Askofu Mwangende alikiri waamini wake kuandika barua ya malalamiko
serikalini wakitaka Serikali iingilie kati suala hilo, lakini alisema
wao Kanisa, wanayafanyia kazi malalamiko hayo kwa kuzungumza na pande
zote mbili husika.
Wachungaji
wanaolalamikiwa walitafutwa kwa zaidi ya wiki tatu sasa, bila
kupatikana na baadhi yao walituma wasaidizi wao kuzungumza na kudai kuwa
malalamiko hayo yana lengo la kuwachafulia huduma yao nchini na kwamba
hakuna ardhi yoyote wala mgodi wanaomiliki kinyume cha sheria.
Lakini
nyaraka tulizonazo zinaonesha kuwa, wachungaji hao wanamiliki mashamba
Morogoro na wamejiingiza katika biashara ya kuchimba madini mkoani humo,
kwa zaidi ya miaka miwili sasa, na kwa kuwa wameoa Watanzania,
wamerithisha watoto wao ardhi baadhi zikiwa mali ya makanisa.
Aidha,
wanalalamikiwa kuwa wanatumia mgongo wa uchungaji kutapeli baadhi ya
waumini wanaowafanyia kazi majumbani bila kuwalipa, huku waumini wenye
fedha wakiwapa uongozi wa juu ndani ya Kanisa fedha na mali zao.
Namba
za simu zilizoachwa kwa gazeti hili ili kupata wachungaji hao haziwezi
kupatikana kwa takribani wiki tatu sasa na eneo la Kanisa wachungaji hao
hawapo kwa kipindi sasa wakidaiwa wapo nje ya mkoa kwa kazi ya
utumishi.
Mkurugenzi
wa Sheria wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Justus Mulokozi
akizungumza kwa niaba ya Wizara, alikiri kupokea malalamiko ya waamini
wa makanisa hayo mawili na mengine mengi, wakiwalalamikia wachungaji wao
wa ndani na nje ya nchi kuhusu masuala ya fedha na mali za makanisa.
“Ni
kweli, tumepokea malalamiko ya waamini wa makanisa hayo, lakini niseme
si hayo tu, yapo makanisa mengi wachungaji wanalalamikiwa, Serikali
tumeona ipo haja kuchunguza makanisa na madhehebu ya dini zote
yanayofanya kazi hapa, upo uhuru wa kuabudu lakini, kuna mambo yanatupa
wasiwasi juu ya mwenendo wa wanaotoa huduma hizo za kiroho,” alisema
Mulokozi.
Alisema
tayari Wizara imepeleka nyaraka hizo katika Mamlaka ya Vitambulisho vya
Taifa (NIDA) na Idara ya Uhamiaji kwa ajili ya uchunguzi zaidi kutokana
na malalamiko ya waumini kudai wachungaji hao wamejiandikisha kama raia
wakati ni wageni na alisema ikibainika, sheria itachukua mkondo wake.
Msemaji
wa Idara ya Uhamiaji nchini, Abbas Irovya aliliambia gazeti hili kuwa
idara yake inashirikiana na Wizara kushughulikia suala hilo na kwamba,
wameiandikia Wizara kuomba nyaraka muhimu, ili kufuatilia uraia wa
wachungaji hao walioatajwa na waamini wao.
chanzo-HabariLeo-
No comments:
Post a Comment