Vyama
vya upinzani jana vilifanya mkutano mkubwa kuwashawishi wananchi
kupinga kile walichokiita kuhujumiwa kwa mchakato wa Katiba Mpya,
wakitangaza Oktoba 10 kuwa siku ya Watanzania wote kushiriki katika
maandamano kushinikiza wapewe haki ya kuandaa Katiba yao.
soma zaidi.....
Wakizungumza
kwa kupokezana katika Viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam jana,
wenyeviti wa vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF, walieleza kuwa
wataendelea kushirikisha taasisi za kiraia kupinga hujuma dhidi ya
mchakato wa Katiba Mpya na kwamba hawatakubali endapo Rais Jakaya
Kikwete atasaini Muswada wa Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba Mpya.
Akizungmza
katika mkutano huo Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba alisema chama
chake hakitakubali endapo Rais Kikwete atasaini muswada huo kwa kuwa una
lengo la kupata Katiba Mpya isiyokuwa na tija kwa taifa. Alisema kuwa
Katiba inayoandaliwa ni kwa ajili ya Watanzania wote na siyo kundi la
watu, hasa CCM na kwamba mchakato wa kuwapata wajumbe 166 wa Bunge la
Katiba kutoka makundi mbalimbali siyo sahihi.
“Haiwezekani
kila taasisi ikateuwa wajumbe tisa ambao majina yao yatakwenda
kuchakachuliwa na usalama wa taifa, kisha kupata majina ya watu
wanaowataka wao, kitu hiki kama CUF hatutakubali,” alisema Profesa
Lipumba na kuongeza:
“Hatutarudi
nyuma na kukubali kuendelea na mchakato huu endapo Rais atasaini
muswada huu. Tutaendeleza harakati za kupinga kwani bila hivyo tutapata
Katiba Mpya isiyokuwa na tija.”
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kuwa ni
wakati wa kukaa meza moja ya mazungumzo kuondoa tofauti zilizopo ili
kulinusuru taifa kuingia katika machafuko.
Alisema
kama taifa, linatakiwa kujifunza kutoka mataifa mengine yalivyotokea
maafa katika michakato ya kuandikwa kwa Katiba Mpya.
“Ni
wakati wa kukaa meza moja, kwa kushirikisha wadau mbalimbali kwani
Katiba inayotafutwa ni ya Watanzania wote na siyo ya CCM,” alisema
Mbatia na kuongeza:
“Lazima
tupate Katiba Mpya kwa gharama yoyote ile, iwe ndani au nje ya Bunge
ili kuhakikisha tunapata Katiba ya Watanzania wote.”
Mwenyekiti
wa Chadema Freeman Mbowe alisema kosa kubwa katika kudai haki ni woga
na hatutapata Katiba Mpya kama tutaendelea kuwa taifa la watu wenye
hofu. Tunataka kukutana na makundi mbalimbali katika jamii ambayo ni
viongozi wa dini, wasomi na watu wa makundi mengine kuwaeleza
kinachoendelea sasa hivi.
Hata
migogoro ya kiimani baina ya Wakristo iliyotokea nchini imesababishwa
na katiba iliyopo sasa, kama Rais atasaini wao hawatashiriki Bunge la
Katiba na watatumia kila mbinu iliyopo duniani kuueleza umma nini
kimetokea na hawataendelea kunyenyekea vitisho vya Jeshi la Polisi.
Tunalaani
mchakato wa katiba kuhodhiwa na chama kimoja na tunatangaza Oktoba 10,
mwaka huu kuwa ni siku maalumu ya kudai katiba na sasa hawataenda tena
Ikulu kwani inaaminika huko ni kwenda kunywa chai na watatangaza
maandamano nchi nzima.
Tumemwambia
IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema) kuwa
hatutaomba ruhusa bali tutampa taarifa.Tunaomba walio makanisani na
misikitini kutafuta katiba mpya na jambo la mwisho Jumatato tutaenda
kufanya mkutano kama huo Zanzibar,” alisema Mbowe.
Mwenyekiti
wa Chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema chama chake kinapinga
namna mchakato wa Katiba ulivyoendeshwa kwasababu kilichopelekwa bungeni
kilikuwa Muswada wa Katiba Mpya, lakini kilichopo mitaani ni Mchakato
wa Rasimu ya Katiba Mpya.
“Tunawaambia
CCM hawatengenezi Katiba Mpya, wanachofanya ni danganya toto kwa kuwa
wanatakiwa kuirudisha Katiba ile ile ya awali.
Naye
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zacharia
Kakobe aliyefika katika viwanja hivyo alisema kuwa Rais Kikwete akisaini
muswada huo, Watanzania watajua kuwa hana nia njema na taifa kwa kuwa
wengi wanaipinga.
“Mimi
natega masikio kusikia kama utasaini au la ili kujua kama unawatega na
kuwahadaa Watanzania. Tunakuomba usikubali mtego huo,” alisema Kakobe
akimwambia Rais Kikwete.
Alisema
tangu awali CCM ilikuwa ikipinga kuandaliwa kwa Katiba Mpya, ingawa
Rais Jakaya Kiwete alijitosa na kukubali mchakato huo kuanza nchini.
“CCM
ilikataa katakata Katiba isianzishwe. Jakaya Kikwete pekee yake
alijipiga kifua akakubali ingawa alishambuliwa kuwa amefanya makosa,”
alisema Kakobe.
Mhadhiri
mstaafu wa Chuo Kukuu cha Dar es Salaam(Udsm), Dk Azaveli Lwaitama
alisema kuwa duniani kote shinikizo la kuundwa kwa Katiba Mpya hutoka
nje ya Bunge na Serikali iliyopo madarakani.
“Tangu
mwaka 1992 vyama vya upinzani vilikuwa vikitaka Katiba Mpya... Katiba
Mpya huzaliwa na wanamapinduzi waliopo nje ya Bunge,” alisema Dk
Lwaitama.
Akizungumzia
ushirikiano wa vyama kumzuia Rais asisaini Sheria ya Rasimu ya Katiba,
alisema: “ Ukifanya jeuri kwa sababu upo madarakani, watu uliodhani
wamegombana watashirikiana.”
Mbunge wa Ubungo John Mnyika, alisema Mahakama ya wananchi ndiyo itakayotoa uamuzi wa mwisho.
“Ninyi ndiyo Mahakama yenye uamuzi wa mwisho, tunasubiri mwongozo wenu, mtakachosema tutafanya,” alisema Mnyika.
Kabla
kuwasili kwa viongozi wakuu wa vyama hivyo vya siasa kwenye Viwanja vya
Jangwani, jana wafuasi wao walikuwa kwenye makundi wakichambua baadhi
ya mambo yaliyoonekana kuleta utata kwenye mchakato wa Katiba Mpya.
Rangi
za bluu, nyekundu na nyeupe zinazotumiwa na vyama vilivyoshiriki
kumtaka Rais Jakaya Kikwete kutosaini Muswada wa Marekebisho ya
Mabadiliko ya Katiba Mpya zilionekana kuzagaa katika viwanja hivyo.
Magari ya Polisi yalionekana kuzunguka maeneo ya viwanja hivyo kuhakikisha ulinzi unaimarika wakati wote wa mkutano.
Nao
wafuasi wa vyama hivyo waliokuwa wamevaa suti nyeusi, miwani na mashati
meupe waliimarisha ulinzi katika eneo la mkutano, wengine wakiingia
Viwanja vya Jangwani kutoka eneo la Barabara ya Morogoro, huku wakibeba
mabango, bendera za vyama hivyo na picha za viongozi wao wakiimba nyimbo
mbalimbali.
Wengi
wa wafuasi hao walifika uwanjani hapo kwa kuletwa na mabasi madogo aina
ya Coaster na wengine wakija kwa makundi kutokana Jeshi la Polisi
kuzuia kufanyika kwa maandamano.
source:bongo newss24
No comments:
Post a Comment