facebook likes

Thursday, September 5, 2013

BUNGE LACHAFUKA TENA: WABUNGE WA VYAMA VYA UPINZANIA WATOKA NJE KUIPIGANIA ZENJI

-WABUNGE CHADEMA, CUF, NCCR WATOKA NJE WAKIPIGANIA ZANZIBAR

MUSWADA wa marekebisho ya pili ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 umezua balaa bungeni, baada ya wabunge wa Kambi ya Upinzani, bila kujali itikadi za vyama kutoka nje ya Bunge.
SOMA ZAIDI...........
Wabunge waliotoka nje ya Bunge ni wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, ambao walikuwa wakishinikiza Muswada huo usisomwe hadi maoni ya wadau kutoka Zanzibar yapatikane.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza kwa siku ya jana, Mbunge wa Konde, Khatibu Said Haji (CUF), aliwaongoza wenzake kutoka Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF kutoka nje, huku Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP), yeye akibaki ndani ya Bunge.
Dalili za wabunge hao kutoka nje ya Bunge, kama njia ya kuwasilisha hisia zao kwa Watanzania zilianza kuonekana, baada ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani wa Wizara ya Sheria na Katiba, Tundu Lissu, kusema ili kutimiza matakwa ya Sheria na kwa kuzingatia mapendekezo ya Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Bunge linahitaji kuangalia upya suala la uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge Maalum.
Alisema kwa mujibu wa kifungu cha 22(2) cha Sheria, idadi ya wajumbe wa Zanzibar katika Bunge Maalum watatokana na makundi yaliyoainishwa katika kifungu cha 22(1)(c).
Alisema hali hiyo, ina maana kwamba uchache wa wajumbe Zanzibar, hawatapungua 55 ambapo Rasimu ya Katiba itakayojadiliwa na Bunge Maalum inahusu Katiba ya Jamhuri ya Muungano peke yake.
Rasimu hiyo, imependekeza masuala yote yasiyo ya Muungano ya Washirika wa Muungano, yaani Tanzania Bara na Zanzibar, yashughulikiwe na Katiba za Washirika hao.
Lissu, alisema kwa sasa wabunge wanaotoka Zanzibar katika Bunge la Muungano ni 83, wakati Baraza la Wawakilishi Zanzibar lina wajumbe 76.
“Kwa ujumla, ili kutekeleza matakwa ya kifungu cha 22(1) na (2) cha Sheria, Zanzibar itakuwa na wajumbe 219 katika Bunge Maalum lenye wajumbe 604, sawa na takriban asilimia 36 ya wajumbe wote.

“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kujua kama ilikuwa busara na sahihi kwa nusu ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoka Zanzibar, kwa nini isiwe busara na sahihi vile vile kwa nusu ya wajumbe wa Bunge Maalum litakaloijadili na kuipitisha Katiba Mpya hiyo kutoka Zanzibar?

“Au ndio kusema hoja za usawa kati ya nchi Washirika wa Muungano huu ni kelele za majukwaani tu? Kwa sababu hiyo, na kwa kuzingatia mapendekezo ya ‘hadhi na haki sawa’ baina ya Washirika wa Muungano yaliyoko katika Rasimu ya Katiba,” alisema Lissu.

Alisema hali hiyo inawezekana kwa kuongeza idadi ya wajumbe waliotajwa katika kifungu cha 22(1)(c) hadi 354, kama ilivyopendekezwa katika maoni ya Kambi ya Upinzani.

Alisema kwa kurekebisha kifungu cha 22(2) ambacho kitasomeka kwamba, idadi ya wajumbe kutoka Zanzibar haitapungua asilimia 55 ya wajumbe hao kama pendekezo hilo litakubaliwa na Bunge.

Alisema wajumbe wa Bunge Maalum kutoka Zanzibar, wataongezeka kutoka 214 kwa mujibu wa Sheria ilivyo sasa, hadi 323.

Rais apingwa

Katika maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani, imepinga vikali mapendekezo ya kumwezesha Rais kuteua Wajumbe wa Bunge Maalum wasiotokana na Bunge lako tukufu na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

“Wajumbe wanaopendekezwa kuteuliwa kwenye Bunge la Katiba kwa mujibu wa ibara ya 20(2)(e) na (4) ya Muswada Mpya sio, na hawawezi kuwa, wawakilishi wa wananchi.

“Kwanza, hawajachaguliwa na mtu yeyote na wala taasisi zao kuwawakilisha katika Bunge la Katiba kwa sababu Muswada Mpya unapendekeza wateuliwe na Rais.

“Kwa sababu ya upinzani huo, mapendekezo ya kumfanya Rais kuwa mteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum wasiokuwa wabunge na Wawakilishi yaliondolewa katika Muswada huo wa Sheria hii.

“Badala yake, kifungu cha 22(1)(c) cha Sheria iliyotungwa na Bunge lako tukufu kiliweka wazi kwamba “wajumbe mia moja sitini na sita watateuliwa kutoka kwenye taasisi zilizotajwa,” alisema Lissu.

Hata hivyo Kambi hiyo ya Upinzani iliingiwa na hofu na Serikali ya CCM kudhibiti muswada huo kutokana na wingi wabunge kutoka chama tawala.

CHANZO: MTANZANIA SEPTEMBA 05, 2013

No comments:

COMMENTS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...