SOMA ZAIDI....
Ametoa kauli hiyo jana asubuhi
(Jumanne, Septemba 24, 2013) mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati
akizungumza na wakazi wa kijiji cha Samunge, wilayani Ngorongoro mkoani
Arusha wakati msafara wa Waziri Mkuu uliposimama nyumbani kwake ili
kumsalimia akiwa njiani kurejea mjini Arusha.
Mchungaji Mstaafu Mwaisapila
maarufu kama Babu wa Samunge alisema kuna mambo mengi ambayo yameandikwa
kwenye Biblia lakini hayakutokea Israeli na sasa yatafanyika hapa
Samunge. “Mungu ametupenda sana, yanakuja mambo makubwa na wala hayako
mbali. Kama mimi ni mzee na nitayaona, kwa hiyo mtarajie kuwa hayako
mbali kutokea,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema katika mafunuo aliyopewa
na Mungu ameonyeshwa kwamba watu wengi zaidi watafurika kijijini Samunge
kuliko ilivyokuwa hapo awali. Alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali
kwa misaada iliyotoa wakati wa ‘kugawa kikombe’ ikiwemo mahema, maji na
ulinzi.
Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani
Arusha kwa ziara maalum ya kusikiliza matatizo ya ardhi yanayowakabili
wakazi wa wilaya ya Ngorongoro, katika tarafa za Ngorongoro, Loliondo na
Sale alisema anakubaliana na utabiri wa Mch. Mwaisapila kwani Tanzania
imejaliwa gesi nyingi na mafuta mengi ambavyo vitabadili sura ya Taifa
hili.
“Mungu ametupa gesi nyingi sana,
katika miaka miwili tutakuwa na umeme kila mahali. Tuna makaa ya mawe
ambayo ni nishati kubwa na sasa tuna fursa ya kupata nishati ya umeme
kutoka ardhini (geo-thermal) katika Ziwa Natron,” alisema.
Alisema Tanzania imekuwa kimbilio la kila mwekezaji na sababu kubwa ni amani na utulivu uliopo nchini.
Aliwaeleza wakazi wa Samunge
kwamba mapema mwakani mkandarasi wa barabara atakuwa katika eneo lao kwa
ajili ya ujenzi wa barabara ya lami ambapo awamu ya kwanza itaanzia
Wasso hadi Mto wa Mbu kupitia Samunge.
Akitoa ombi maalum kwa niaba ya
vijana mbele ya Waziri Mkuu, Bw. Elias Kalumbwa alisema wanaomba
kuchimbiwa bwawa ili waweze kujiajiri kupitia kilimo cha mbogamboga na
matunda.
Bw. Kalumbwa ambaye amesomea
masuala ya wanyamapori alisema eneo la kuchimba bwawa lipo katika mto wa
msimu unaopita kijijini hapo. “Eneo la kuchimba bwawa lipo katika mto
wetu, vijana tunaweza kujiajiri endapo tutapata bwawa ili tufanye kilimo
cha umwagiliaji maji,” alisema huku akishangiliwa.
Naye Bibi Martha Sereri (70)
alimweleza Waziri Mkuu kwamba wanaomba jimbo la Ngorongoro ligawanywe
kwa sababu ni kubwa sana kiasi kwamba inamuwia vigumu mbunge wao kufika
maeneo yote. Aliomba pia wapatiwe walimu wa sayansi na hisabati kwa
ajili ya shule 10 za sekondari zilizopo kwenye tarafa yao.
Aliomba wapatiwe mikopo ya
matreka ili waweze kuongeza ukubwa wa mashamba yao. “Tunaomba mikopo ya
matrekta na plau, haya mashamba umeyaona njiani yamelimwa na Wakenya.
Ukikodisha trekta kila ekari unatozwa sh. 100,000/-. Je tutafika wapi?
Mkitukopesha matrekta mtakuwa mmetusaidia zaidi,” alisema.
Akijibu hoja hizo, Waziri Mkuu
alisema hoja zao ni za msingi na kwamba suala la vijana kupatiwa bwawa
ni jambo linalowezekana kupitia mipangpo ya maendeleo ya kilimo ya
wilaya (DADPS).
“Andaeni andiko lenu, inabidi
litoke kwa wananchi na siyo Serikalini. Mkituletea ni jambo
linalowezekana kwani liko ndani ya mipango ya wilaya.”
Akijibu hoja kuhusu ukubwa wa
jimbo, Waziri Mkuu aliwaambia wakazi hao kwamba inawezekana kuongeza
jimbo isiwe suluhisho la matatizo yao kwa sababu ya jiografia ya eneo
lao.
“Kuongeza jimbo inaweza isiwe
jibu la kila kitu kwani matatizo mnayopata yanatokana na jiografia ya
eneo lenu, kutoka Ngorongoro, Loliondo hadi huku Sale. Mimi nadhani
tuangalie pia uwezekano wa kuwapa Halmashauri ili kusogeza huduma kwa
wananchi. Tutaangalia njia zote mbili na kuona ipi italeta majibu ya
haraka kwenu,” alisema.
No comments:
Post a Comment